Vitorinha: Nataka kuiheshimu jezi namba 10 ya Marta
Muktasari:
- Vitorinha alionyesha kiwango bora katika mechi mbili za mwanzo za Brazil na Canada kwenye michuano hiyo, akifunga bao zuri la mpira wa adhabu katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Tanzania kwenye mchezo wao wa kwanza.
Kiungo wa Brazil, Vitorinha, amesema anataka kuendelea kuiheshimu jezi namba 10 ambayo imewahi kuvaliwa na nyota wakubwa wa nchi hiyo, akiwemo malkia wa soka la wanawake, Marta Vieira da Silva, huku akifichua malengo yake ya kuondoka Poland akiwa na ubingwa wa Kombe la Dunia la Wanawake la U-20 mwaka 2026.
Vitorinha alionyesha kiwango bora katika mechi mbili za mwanzo za Brazil na Canada kwenye michuano hiyo, akifunga bao zuri la mpira wa adhabu katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Tanzania kwenye mchezo wao wa kwanza.
Kiungo huyo anavaa jezi maarufu namba 10 ya Brazil, ambayo imewahi kuvaliwa na magwiji wa soka kama Pele na wachezaji wengine akiwemo Marta kwa upande wa wanawake.
Vitorinha alisema hana presha na ukubwa wa jezi hiyo na anaichukulia kama motisha ya kufanya vizuri zaidi.
“Kuna jukumu linalokuja pamoja na jezi hii, lakini mimi naliona kama jambo chanya,” alisema Vitorinha.
“Najua kuhusu wachezaji wote wakubwa waliowahi kuvaa jezi hii namba 10, kama vile malkia wetu Marta. Nitaendelea kuiheshimu jezi yake na, Mungu akipenda, tutaondoka hapa tukiwa mabingwa.”
Hata kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia la U-20, Vitorinha alisema kila mchezaji wa kikosi cha Brazil anaingia uwanjani kwa ajili ya timu pamoja na historia kubwa ambayo timu hiyo imeibeba.
Kwa upande wake, alisema anapocheza anahisi pia jukumu la kuheshimu historia ya jezi namba 10, huku akifanya hivyo sambamba na safari yake binafsi ya soka. Ninaposherehekea uwanjani, huwa nafikiria karibu kila jambo tangu nilipokuwa msichana mdogo,nataka kuiheshimu familia yangu na kila mtu ambaye amekuwa pamoja nami tangu mwanzo.
Ni wale waliokuwa nami tangu mwanzo pekee wanaojua jinsi nilivyofanya kazi kwa bidii hadi kufika hapa nilipo leo. Brazil inaongoza kundi B ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili ikiifunga Tanzania kwa mabao 4-1 na Canada ikiitandika mabao 3-0.