Fanya hivi uwe na miguu laini
Muktasari:
- Usijifiche tena bana! Miguu nayo ni sehemu ya urembo wako na inahitaji kupewa muda kama unavyoufanyia uso. Kama visigino vimekuwa vigumu, ngozi inachubuka na miguu imekauka mpaka hauna raha kuvaa viatu vya wazi, kuna mambo rahisi unaweza kuanza kuyafanya ili kuirudisha kwenye ulaini.
WE’ dada unayependa kuvaa sketi fupi, gauni au hata kaptula halafu ukifika kwenye miguu unaanza kujisitiri, vipi tena? Hivi kweli uso umepangiliwa, nywele zimekaa, kucha ziko safi, lakini miguu yenyewe imejaa magaga mpaka mtu akikuangalia anaweza kudhani umetoka kuchimba kisima?
Usijifiche tena bana! Miguu nayo ni sehemu ya urembo wako na inahitaji kupewa muda kama unavyoufanyia uso. Kama visigino vimekuwa vigumu, ngozi inachubuka na miguu imekauka mpaka hauna raha kuvaa viatu vya wazi, kuna mambo rahisi unaweza kuanza kuyafanya ili kuirudisha kwenye ulaini.
Na usifikiri ni lazima uwe na pesa nyingi kwenda saluni kila wiki. Wakati mwingine tatizo ni kutokuwa na utaratibu wa kuitunza miguu yako.
Sasa kama umechoka kuitazama miguu yako na kusema, “Hii nayo miguu au ganda la nazi?” kaa hapo. Haya ndiyo mambo unayoweza kufanya ili uwe na miguu laini, safi na yenye mwonekano wa kuvutia.
MAJI YA UVUGUVUGU
Kabla ya kuanza kuisafisha miguu, loweka kwenye maji ya uvuguvugu kwa dakika 10 hadi 15. Hii husaidia kulainisha ngozi iliyokauka na kufanya iwe rahisi kuondoa ngozi zilizokufa. Usitumie maji ya moto kupita kiasi kwa sababu yanaweza kuifanya ngozi izidi kukauka. Maji ya kawaida yenye uvuguvugu yanatosha. Baada ya kuloweka, kausha miguu taratibu kwa taulo safi, hasa sehemu za kati ya vidole.
ONDOA NGOZI
Kama una magaga kwenye visigino au sehemu nyingine za miguu, unaweza kutumia jiwe maalumu la kusugulia miguu waswahili wenzangu mnavijua au kifaa salama cha kuondoa ngozi ngumu. Fanya hivyo kwa upole baada ya kuloweka miguu. Usisugue kwa nguvu ukifikiri ukiondoa ngozi nyingi utapata ulaini wa haraka. Kusugua kupita kiasi kunaweza kujeruhi ngozi na kufanya mwili utengeneze ngozi ngumu zaidi. Mara moja au mbili kwa wiki inaweza kutosha kwa watu wengi.
PAKA MAFUTA
Baada ya kuoga au kuloweka miguu, usiiache ikiwa imekauka kabisa. Tumia mafuta au krimu inayosaidia kuongeza unyevu kwenye ngozi.
Zingatia zaidi visigino na sehemu ambazo huwa zinakauka haraka. Kwa ngozi iliyokauka sana, bidhaa zenye viambato kama mafuta ya maji au mgando zinaweza kusaidia kulainisha ngozi ngumu.
USISAHAU VISIGINO
Watu wengi wanatunza sehemu ya juu ya mguu lakini wanasahau visigino. Kumbe hapa ndipo magaga na mipasuko hujitokeza kwa urahisi.
Kila unapomaliza kuoga, paka mafuta ya kutosha kwenye visigino. Hilo ni eneo ambalo linakutana na vumbi mwa urahisi ukioga juu tu ukapasahau basi lazima utapata majanga ya mipasuko.
VAA SOKSI USIKU
Kipenzi usiku wakati unakwenda kulala jitahidi sana uvae soksi ukipata zile laini ‘silcon’ ni vizuri zaidi ili kutunza unyevu ambao unatokana na mafuta uliyopaka.
Kulala na miguu mitupu bila soksi alafu ukategemea kuwa na miguu milaini ni sawa na kutwaga maji kwenye kinu.
VIATU VISIVYOKUBANA
Viatu visivyokaa vizuri vinaweza kuongeza msuguano kwenye miguu na kusababisha maeneo fulani kuwa magumu au yenye ngozi nene (visugu). Pia usikae muda mrefu na miguu yenye jasho ndani ya viatu bila kuiosha na kuikausha vizuri. Usafi wa miguu ni sehemu muhimu ya mwonekano.
USIKATE MAGAGA
Hili ni kosa ambalo wengine hulifanya wakitaka miguu iwe laini haraka. Kukata ngozi ngumu kwa wembe au kitu chenye ncha kali kunaweza kusababisha jeraha, maambukizi na kuongeza tatizo.
Kama ngozi imekuwa ngumu sana au visigino vina mipasuko mikubwa, ni bora kupata ushauri wa mtaalamu wa afya au mtaalamu wa utunzaji wa miguu badala ya kujitibu kwa njia hatarishi.
WEKA RATIBA
Usisubiri miguu iwe imejaa magaga mpaka inachana neti ndio uhangaike kuisugua. Tengeneza utaratibu rahisi. Osha miguu kila siku, kausha vizuri, paka unyevu na mara moja au mbili kwa wiki fanya utunzaji wa ngozi ngumu kwa upole.
Jamani wewe kama ni mwanamke au mwanaume usikubali kujificha kwenye kichaka cha viatu vya kufunika, siku litakukuta jambo la aibu useme Aunty yako sikukwambia. BADILIKA KABLA HUJAAIBIKA.