Vita ya Ballon d’Or yamtesa mkewe Kane
Muktasari:
- Kane angependa kujua kuanzia sasa kama ameshinda tuzo ya Ballon d’Or, kwa sababu kutokuwa na uhakika na maswali ya mara kwa mara kunaisumbua familia yake.
MUNICH, UJERUMANI: MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa England na Bayern Munich, Harry Kane amesema kusubiri kujua kama ameshinda Ballon d’Or hadi Jumatatu, Oktoba 26, 2026 kunamfanya mkewe kuwa na msongo wa mawazo sambamba na familia nzima.
Kane angependa kujua kuanzia sasa kama ameshinda tuzo ya Ballon d’Or, kwa sababu kutokuwa na uhakika na maswali ya mara kwa mara kunaisumbua familia yake.
Hata hivyo, mshambuliaji huyo wa Bayern Munich na timu ya taifa ya England anakubali kuwa hali ya kusubiri kabla ya mshindi kutangazwa katika ukumbi wa London Palladium, England, Jumatatu usiku, ni sehemu ya burudani ya hafla hiyo.
Kane ndiye anayependekezwa zaidi kushinda tuzo hiyo kubwa ya mchezaji bora kutokana na kiwango chake kizuri cha ufungaji mabao.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alifunga mabao 61 akiwa na Bayern Munich msimu uliopita na mabao 12 akiwa na timu ya taifa ya England. Msimu huu, tayari amefunga mara 10 kwa Bayern na sita akiwa na England.
Nyota huyo alifunga kwa mkwaju wa penalti katika sare ya mabao 2–2 dhidi ya Arsenal kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumatano, katika Uwanja wa Allianz Arena. Hata hivyo, tukio lake lililoonekana zaidi lilikuwa pasi nzuri ya kupenya safu ya ulinzi iliyomuwezesha Alphonso Davies kufunga bao la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 1–1.
Katika vita ya kuwania tuzo hiyo Lamine Yamal wa Barcelona ndiye anayeshika nafasi ya pili kwa mastaa wanaodaiwa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kushinda Ballon d’Or, huku Kylian Mbappe wa Real Madrid akifuata nafasi inayofuata.
MSIKIE KANE
Akizungumzia kimuhemuhe kuhusiana na tuzo hiyo, Kane alisema: “Nadhani mke wangu angependa kujua, na familia yangu pia… hali hii inaleta msongo mkubwa wa mawazo kwa kila mtu.
“Naelewa kwa nini hawawaambii watu mapema. Wanataka kila mtu ahudhurie, pamoja na majina makubwa ya soka, na watu wengi zaidi watafuatilia hafla hiyo ikiwa hawajui mshindi. Kwa hiyo, ninaelewa sababu yao.
“Kwa upande wangu, ningependa kujua mapema ili nijue hali ilivyo na nisilazimike kusubiri hadi mwisho wa hafla nzima. Lakini huo ni uamuzi wao, siwezi kuudhibiti. Tutalazimika kufurahia hafla hiyo na kujaribu kutokuwa na msongo mkubwa wa mawazo.
“Ninajaribu kutofikiria sana kuhusu hilo. Ni wazi kwamba ni vigumu kutolifikiria. Kuna uvumi na habari mbalimbali zinazozunguka kila wakati, kwa hiyo unajaribu kujiepusha nazo.”
YAMAL, MBAPPE
Wakati Kane na familia yake mapigo ya mioyo yakiwaenda mbio, nyota wa Barcelona, Lamine Yamal ameshamalizana na kampuni moja ya ndege za kukodi akikodi usafiri wa kumpeleka Londona familia yake kwenda kushuhudia hafla hiyo.
Hata hivyo, Mbappe alikuwa bado hajaamua juu ya usafiri atakaoutumia keshokutwa kufika London, ingawa watu wake wa karibu walikuwa wameshaanza maandalizi ya kumsindikiza kwenda jijini humo.
Kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba Mbappe anafikiria zaidi kuhusiana na mchezo wa kesho wa El Clasico dhidi ya Barcelona kuliko suala la Ballon d’Or akiamini kwamba nafasi yake kutwaa tuzo hiyo ni ndogo sana msimu huu.