Vini Jr, Mourinho wazua jambo Hispania
Muktasari:
- Winga huyo wa Brazil alidhani amefunga bao la pili kwa Real Madrid na kuungana na wenzake kushangilia, huku kocha Jose Mourinho naye akishangilia pembeni mwa uwanja.
MADRID, HISPANIA: VINICIUS JR alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kuvuta nywele za Nathan Saliba katika ushindi mwembamba wa Real Madrid dhidi ya Villarreal, katika mchezo uliojaa mabishano na uamuzi ya waamuzi.
Winga huyo wa Brazil alidhani amefunga bao la pili kwa Real Madrid na kuungana na wenzake kushangilia, huku kocha Jose Mourinho naye akishangilia pembeni mwa uwanja.
Hata hivyo, bao hilo lilikataliwa baada ya mwamuzi kupitia marudio ya tukio kwenye kifaa cha video pembeni mwa uwanja, yaliyomwonyesha Vinicius akivuta nywele za Saliba kabla ya kufunga.
Mwamuzi alimwonyesha Vinicius kadi nyekundu dakika ya 72 kwa kitendo cha utovu wa nidhamu wa kutumia nguvu dhidi ya mpinzani, dakika 20 tu baada ya kuingia akitokea benchi kuchukua nafasi ya beki wa England, Trent Alexander-Arnold.
Uamuzi huo uliwaacha Real Madrid wakiwa na hasira, huku Mourinho akikosa mkutano wa lazima na waandishi wa habari baada ya mchezo.
Real walikuwa tayari wanaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na kijana Yan Diomande, aliyefunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na klabu hiyo akitokea RB Leipzig mwezi Agosti kwa ada inayoweza kufikia pauni120 milioni.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19 alifunga dakika ya 62 kwa shuti la chini lililoelekezwa kona ya mbali, lakini awali bao hilo lilikataliwa kwa sababu ya kuotea kabla ya uamuzi kubadilishwa baada ya mapitio ya mfumo wa mwamuzi msaidizi wa video (VAR).
Baada ya vinara Barcelona kuichapa Getafe mabao 3-0 mapema siku hiyo, Real walihitaji ushindi huo kupunguza pengo la pointi dhidi ya mabingwa watetezi. Hata hivyo, walishindwa kuonyesha makali ya kutosha kabla ya bao la Diomande.
Baada ya michezo minane, kikosi cha Mourinho kiko nyuma kwa pointi sita dhidi ya vinara hao, kikitarajiwa kukutana na Barcelona Oktoba 25.
Ilikuwa siku ngumu pia kwa Kylian Mbappe, aliyopoteza nafasi mbili nzuri za kufunga na kuzuiwa na kipa Peter Gulacsi, huku kiungo wa England, Jude Bellingham, akionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea rafu mpinzani.
KWA NINI MOURINHO HAKUZUNGUMZA?
Real Madrid si timu inayojulikana sana kwa kuwapeleka wachezaji wake kuzungumza na vyombo vya habari, hata baada ya ushindi mnono. Hata hivyo, baada ya mchezo huo, ilitarajiwa mmoja wa viongozi wa timu hiyo kujitokeza kueleza ushindi wao na kutoa maoni kuhusu maamuzi ya waamuzi.
Lakini hilo halikutokea.
Kilichokuwa cha kushangaza zaidi ni Mourinho kukosa mkutano na waandishi wa habari kwa mara ya kwanza tangu aanze kuinoa timu hiyo.
Waandishi wa habari walisubiri kwa muda, lakini hakujitokeza. Baadaye, taarifa zilienea kwamba kocha huyo aliamua kutotoa maoni akihofia kauli zake zingeweza kumsababishia adhabu ya kufungiwa.
Hasira za Mourinho dhidi ya waamuzi zilionekana wazi muda wote wa mchezo. Alionyeshwa kadi ya njano na mara kadhaa wafanyakazi wa benchi lake la ufundi walilazimika kumzuia kimwili, huku akionekana kushindwa kudhibiti hisia zake.
Tukio lililochochea zaidi hali hiyo ni uamuzi wa kumwondoa Vinicius kwa kadi nyekundu baada ya bao lake kukataliwa. Mourinho alikuwa amekimbia uwanjani kushangilia pamoja na mchezaji wake, lakini muda mfupi baadaye hali ilibadilika na kuwa ya vurugu.
Waamuzi walipokuwa wakielekea nje ya uwanja, walikabiliwa na malalamiko makali huku wachezaji wa Real Madrid wakiwazunguka.
Mchezo uliokuwa wa kawaida na usio na msisimko mkubwa uligeuka kuwa wa mabishano na matukio mengi katika kipindi cha pili. Kadi nyekundu ya Vinicius ilikuwa ya pili mfululizo kwa Real Madrid katika michezo yao ya karibuni, baada ya Dean Huijsen kutolewa nje dhidi ya Atletico Madrid.
Hata hivyo, mbali na mabishano kuhusu maamuzi ya waamuzi, kikosi cha Mourinho kilionyesha kiwango kisichoridhisha.
Pamoja na utata uliojitokeza, Real hawakuonyesha kiwango cha kuwafanya waonekane kama timu yenye uwezo wa kupambana kwa dhati kuwania ubingwa.
SHERIA ZINASEMAJE KUHUSU KUVUTA NYWELE?
Kwa mujibu wa Sheria ya 12 ya mchezo wa soka, inayosimamiwa na Bodi ya Kimataifa ya Soka (IFAB), kitendo cha mchezaji kuvuta nywele za mpinzani kinaweza kuainishwa kama matumizi ya nguvu kupita kiasi, yanayostahili kadi nyekundu.
Sheria zinaeleza kuwa mchezaji ambaye hafanyi jitihada za kucheza mpira anaweza kutolewa nje kwa kadi nyekundu akionyesha kitendo cha wazi cha kuvuta nywele za mpinzani kwa nguvu.
Hata hivyo, waamuzi wa Ligi Kuu England wamebadili namna wanavyotathmini matukio ya kuvutana nywele msimu huu, baada ya wachezaji watatu kutolewa kwa kosa hilo katika msimu wa 2025/26.
Kuanzia msimu huu, si kila tukio la mchezaji kuvuta nywele za mpinzani litamaanisha kadi nyekundu moja kwa moja. Waamuzi wanapaswa kuzingatia kiwango cha nguvu kilichotumika na dhamira ya mchezaji.
Pamoja na mabadiliko hayo, kitendo cha makusudi cha Vinicius kumvuta Saliba nywele kingeweza pia kusababisha kadi nyekundu nchini England.
Mwezi Septemba, wachezaji wawili wa Antigua na Barbuda walitolewa kwa kadi nyekundu kutokana na kuvuta nywele za wapinzani katika mchezo wa Ligi ya Mataifa ya Shirikisho la Soka la Amerika Kaskazini, Kati na Karibiani (CONCACAF), dhidi ya Anguilla.