Hali mbaya! Vipigo, kadi vyamwandama Pochettino
Muktasari:
- Man United na Pochettino iliingia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Sporting ikiwa na hasira kutokana na kutolewa kwa beki Leny Yoro kwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Liverpool, ikiamini uamuzi huo haukuwa sahihi na ulichangia kipigo cha mabao 4-0.
LISBON, Ureno: NI mwaka wa tabu! Mechi mbili, hakuna ushindi. Kadi mbili nyekundu, mabao mawili ya kufunga na sita ya kufungwa. Bao moja limekataliwa. Huo ndio mwanzo wa Kocha Mauricio Pochettino Manchester United, lakini je, amejifunza nini katika wiki yake ya kwanza yenye misukosuko mikubwa?
Man United na Pochettino iliingia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Sporting ikiwa na hasira kutokana na kutolewa kwa beki Leny Yoro kwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Liverpool, ikiamini uamuzi huo haukuwa sahihi na ulichangia kipigo cha mabao 4-0.
Hasira za viongozi wa klabu hiyo zilizidi baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Sporting jijini Lisbon. Safari hii ni mwamuzi Szymon Marciniak, aliyechezesha fainali ya Kombe la Dunia la 2022, ndiye aliyekuwa kwenye lawama.
Marciniak alipuliza filimbi kabla ya Amad Diallo kufunga bao la kichwa katika kipindi cha kwanza, hatua iliyozuia mfumo wa VAR kuchunguza kama uamuzi wake wa kuamuru Youri Tielemans alimchezea rafu Goncalo Inacio kabla ya mpira kumfikia winga huyo wa Ivory Coast ulikuwa sahihi.
Hata hivyo, winga wa zamani wa United, Ashley Young hakukubaliana na uamuzi huo na aliutaja uchezeshaji wa Marciniak kuwa wa aibu.
Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Tielemans kuonyeshwa kadi ya njano iliyochangia kutolewa kwa kadi nyekundu dakika za mwisho. Hiyo imeifanya United kuwa na jumla ya wachezaji wanne waliotolewa kwa kadi nyekundu katika mechi zao tano zilizopita. Kutokana na adhabu hiyo, kiungo huyo wa Ubelgiji atakosa mchezo wa marudiano dhidi ya RB Leipzig utakaochezwa Old Trafford Desemba 8.
Katika kipindi kifupi, Marciniak alikataa madai ya kufanyiwa rafu kwa makipa wa timu zote mbili, Senne Lammens wa Manchester United na Kaique wa Sporting, kabla ya kufungwa mabao. Mabeki wa timu hizo walilalamikia uamuzi huo, huku VAR ikimwita mwamuzi huyo kwenda kutazama marudio ya tukio la pili pekee na alibadili uamuzi wake.
Kwa upande wa United, watu wa ndani ya klabu hiyo waliamini tukio la Tielemans halikuwa rafu na bao la Amad lilipaswa kuhesabiwa. Pia waliona mguso wa Patrick Dorgu kwa kipa Kaique haukuwa mkubwa kiasi cha kustahili bao lao kukataliwa.
Pochettino alilazimika kuwa makini katika kutoa maoni yake, akitambua kauli kali dhidi ya mwamuzi ingeweza kumwingiza kwenye matatizo na hata kutozwa faini.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mechi, alijibu swali kuhusu uamuzi wa Marciniak kwa kutikisa kichwa kuashiria kukubaliana na hoja hiyo. Hata hivyo, alipokuwa akizungumza na kituo cha televisheni cha TNT dakika chache kabla, alikuwa na maelezo zaidi.
“Ni vigumu kupata mchezo ambao unaadhibiwa kwa kiwango kikubwa namna hii. Tumeadhibiwa sana katika matukio muhimu ya mchezo,” alisema.
POCHETTINO ATAFUTA USHINDI WA KWANZA
Si mara ya kwanza msimu huu kwa Man United kutawala sehemu kubwa ya mechi, lakini ikashindwa kupata ushindi.
Mabao waliyofungwa dhidi ya Sporting katika Uwanja wa Jose Alvalade yalikuwa ya kushangaza, yakichangiwa na makosa ya wachezaji wake wenyewe.
Dakika 75 tu baada ya kuokoa penalti kwa ustadi mkubwa, kipa Lammens alifanya kosa na kusababisha penalti nyingine ambayo ilizaa bao.
Kipa huyo alihusika pia katika bao la pili baada ya kuudondosha mpira mbele ya mshambuliaji wa Sporting, Luis Suarez aliyefunga kwa staili ya tikitaka ‘overhead kick’.
Pochettino alisisitiza timu yake ilicheza vizuri na ilistahili ushindi, lakini makosa yaliigharimu.
“Naamini tulitawala mwchi na tulistahili kushinda, lakini hatukufanikiwa kutokana na mazingira tofauti.
“Kila timu hufanya makosa, lakini makosa tunayofanya sisi yanaambatana na adhabu kubwa sana. Klabu nyingine nazo hufanya makosa au hukumbana na mazingira magumu, lakini wakati mwingine mambo huwa upande wao. Hata hivyo, huo ndio ukweli wetu. Tunapaswa kuwajibika,” alisema.
United bado haijapata ushindi ugenini katika mashindano yoyote msimu huu. Pia imefanikiwa kushinda mara moja pekee katika mechi zake 13 zilizopita.
Katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, United inashika nafasi ya 19 ikiwa na pointi mbili zaidi ya Roma, ambayo ipo nje kidogo ya nafasi 24 za juu zinazohakikisha timu inasonga mbele katika hatua inayofuata.
POCKETTINO AMLINDA LAMMENS
Licha ya makosa ya Lammens, Pochettino amesimama upande wa kipa huyo, huku Ashley Young akiamini huenda kosa jingine likamfanya apoteze nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza.
Uchezaji wa kipa huyo wa Ubelgiji haukuwa mzuri na makosa yake yameanza kuongezeka.
Hata hivyo, Pochettino alionyesha wazi bado ana imani na Lammens licha ya makosa yake.
“Mambo kama haya hutokea. Huo ndio mpira wa miguu. Soka linahusu pia kufanya makosa.
“Mimi siku zote nataka kumuunga mkono mchezaji wangu. Nafikiri tunapaswa kuzungumzia suala la uwajibikaji. Katika matukio kama haya, safu yetu ya ulinzi inapaswa kumsaidia zaidi kipa kwa sababu ilikuwa hali ngumu sana kwake.
“Sikusudii kuilaumu safu ya beki, lakini kuna mambo mawili tunayopaswa kuyaboresha. Ni maelezo madogo tunayopaswa kuyafanyia kazi ili tuweze kukabiliana vizuri zaidi na mazingira ya aina hii,” alisema.
Imekuwa wiki yenye matukio mengi kwa Pochettino, ambaye Jumatano iliyopita asubuhi kwa saa za Uingereza alikuwa bado kocha wa timu ya taifa ya Marekani.
Pamoja na misukosuko hiyo, kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 amesema anafurahia kukubali changamoto ya kuiongoza United. “Nina furaha kuwa hapa. Nina msisimko mkubwa wa kuwa mwakilishi wa klabu hii.
“Tupo hapa kwa sababu hali ya timu haikuwa kama ambavyo mashabiki na watu wengine walivyotarajia. Tumekuja kubeba jukumu la kubadilisha hali hiyo na nina uhakika tutafanya vizuri zaidi.
“Itakuwa kazi ngumu, bila shaka. Hakuna jambo rahisi. Lakini tuna nguvu na uwezo wa kufanya hivyo. Muhimu zaidi, tuna wachezaji na nguvu kubwa kutoka kwa mashabiki wetu, jambo ambalo ni muhimu sana,” alisema.