Vigogo wapambana Grealish asalie mazima Everton
Muktasari:
- Taarifa zinadai Everton imevutiwa na Grealish na kwamba ipo tayari kutoa kiasi cha pesa ambacho kitakuwa ni chini ya Pauni 50 milioni.
EVERTON inatamani kumsainisha mkataba wa moja kwa moja staa wa Manchester City anayecheza kwa mkopo katika timu yao, Jack Grealish ifikapo mwisho wa msimu huu.
Taarifa zinadai Everton imevutiwa na Grealish na kwamba ipo tayari kutoa kiasi cha pesa ambacho kitakuwa ni chini ya Pauni 50 milioni.
Grealish ambaye alijiunga na Everton katika dirisha lililopita, amekuwa akipambana kuhakikisha anaonyesha kiwango bora ili kuitwa katika kikosi cha England kitachoshiriki Kombe la Dunia mwakani.
Mabosi wa Everton wanataka kumsainisha mkataba wa kudumu staa huyu kutokana na kiwango bora ambacho ameonyesha tangu ajiunge nao msimu huu.
Hadi sasa Grealish amecheza mechi nne za michuano yote na ametoa asisti nne, akiwa sehemu muhimu ya ushindi wa Everton dhidi ya Wolves katika mchezo uliopita ambapo alitoa asisti mbili.
Mkataba wake na Man City unaisha 2027 na matajiri hao wa Jiji la Manchester wanaonekana wapo tayari kumwachia aondoke jumla.
Adam Wharton
MANCHESTER United ni kati ya klabu zinazofikiria kuwasilisha ofa kwenda Crystal Palace kwa ajili ya kumsajili kiungo wa timu hiyo, Adam Wharton katika dirisha la usajili la Januari.
Mbali ya mashetani wekundu, huduma ya Wharton pia inawindwa na Liverpool na Chelsea.
Wharton mwenye umri wa miaka 21, amekuwa na kiwango bora tangu msimu uliopita jambo lililovutia vigogo mbalimbali.
Mohamed Kudus
CHELSEA ilikuwa ni kati ya timu zilizojaribu kumsajili mshambuliaji wa West Ham na timu ya taifa ya Ghana, Mohammed Kudus, 25, kabla hajajiunga na Tottenham katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Inaelezwa sababu kubwa iliyosababisha Chelsea isifanikishe mchakato huo ni ofa ambayo waliiwasilisha. Chelsea ilikuwa inataka kutoa pesa kidogo pamoja na mchezaji wakati West Ham ikihitaji pesa tu.
Douglas Luiz
NOTTINGHAM Forest itakuwa na wajibu wa kumnunua moja kwa moja kiungo wa Juventus, Douglas Luiz, 27, kwa ada ya Euro 25 milioni katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani ikiwa staa huyo wa kimataifa wa Brazil atacheza dakika 45 katika kila mechi 15 za EPL msimu huu. Luiz amejiunga na Forest kwa mkopo wa msimu mmoja katika dirisha lililopita baada ya kuona nafasi yake Juventus inazidi kuwa finyu.
Jorthy Mokio
LIVERPOOL na Manchester United zinapigana vikumbo kuiwania saini ya kiungo wa kati wa Ajax, Jorthy Mokio, 17, ambaye tayari ameshachezea timu taifa ya Ubelgiji.
Kinda huyu mwenye uwezo wa kucheza kama beki na kiungo wa kati, ni miongoni mwa vipaji vilivyoibuliwa na Ajax inayodaiwa kuwa tayari kumuuza lakini kwa kiasi cha pesa kisichopungua Pauni 40 milioni.
Aaron Anselmino
BORUSSIA Dortmund inataka kufanya mpango ili kumnunua beki wa Chelsea na Argentina, Aaron Anselmino, 20, ambaye amejiunga nao kwa mkopo wa msimu mmoja katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Hata hivyo, mpango huo wa kumsainisha mkataba wa kudumu utafanyika wapo tu Anselmino ataonyesha kiwango bora msimu huu.
Marc Bernal
CHELSEA, Everton na Brighton bado zinaendelea kuangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Barcelona, Marc Bernal, 18, na timu ya taifa ya vijana ya Hispania kuelekea dirisha lijalo baada ya kushindwa kumsajili katika dirisha lililopita la majira ya baridi.
Kiungo huyu ilishindikana kuondoka katika dirisha lililopita kutokana na majeraha aliyokuwa nayo.
Kenan Yildiz
CHELSEA ina mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Juventus na timu ya taifa ya Uturuki, Kenan Yildiz, 20, lakini itahitajika kulipia Pauni 86 milioni kama sehemu ya ada ya uhamisho. Licha ya kiasi hicho kuonekana kikubwa, Chelsea bado haijakata tamaa na inapanga kufungua mazungumzo rasmi ifikapo Januari mwakani.
Kenan mwenyewe anadaiwa kutamani sana kutua kwa matajiri hao wa Jiji la London.