Vigogo wa Liverpool wampigia hesabu Olise
Muktasari:
- Inaelezwa vigogo wa Liverpool wanamuona kuwa mbadala sahihi wa Mohamed Salah ambaye kuna uwezekano mkubwa akatimkia Saudi Arabia mwisho wa msimu huu.
LIVERPOOL imepanga kutumia takriban Pauni 80 milioni kwa ajili ya kumsajili winga wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa, Michael Olise katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Inaelezwa vigogo wa Liverpool wanamuona kuwa mbadala sahihi wa Mohamed Salah ambaye kuna uwezekano mkubwa akatimkia Saudi Arabia mwisho wa msimu huu.
Baadhi ya taarifa zinadai mkataba wa Olise una kipengele kinachoeleza kuwa anaweza kuondoka kwa kiasi maalumu cha pesa na suala hilo ndilo limeivutia Liverpool ambayo hivi karibuni imekuwa ikitumia pesa kuhakikisha inasajili wachezaji mahiri.
Inaelezwa Olise mwenyewe anatamani kurudi England ingawa dili lolote litakalofanyika ili kumrudisha huenda likawa la mkwanja mrefu.
Mchezaji huyo ambaye ana uraia pacha wa Uingereza na Ufaransa mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2029.
William Saliba
ARSENAL imempa ofa ya mkataba mpya wa miaka mitano beki kisiki wa Ufaransa, William Saliba, ambaye mkataba wa sasa unamalizika 2027. Mabosi wa Arsenal wamempa Saliba ofa hiyo ili kuzima tamaa za Real Madrid ambayo imekuwa ikimfuatilia kwa karibu tangu mwaka jana. Mbali ya kumpa miaka mitano Arsenal pia inataka kumpa mshahara unaodaiwa kufikia Pauni 250,000 kwa wiki.
Marc Guehi
LIVERPOOL ya kuinasa saini ya beki kisiki wa Crystal Palace na England, Marc Guehi, 25, katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani pale mkataba wake utakapomalizika. Awali ilielezwa Liverpool ambayo iliikosa saini yake katika siku ya mwisho ya dirisha la usajili ilikuwa inataka kuwasilisha ofa ili kumsajili Januari, lakini baadaye ilipotezea na kusisitiza kwamba itasubiri hadi mwisho wa msimu kumsajili akiwa huru.
Harry Maguire
MANCHESTER United inawafanyia tathmini mabeki Harry Maguire, 32, na Luke Shaw, 30, kabla ya kuwauza majira ya baridi mwakani. Mashetani Wekundu wanataka kuwauza Shaw na Maguire ili kupata pesa za kuimarisha zaidi safu ya ulinzi. Maguire si mchezaji tegemeo kikosi cha kwanza, lakini Shaw hupewa nafasi mara kwa mara pale anapokuwa fiti.
Jota Silva
WINGA wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya Ureno, Jota Silva, 26, anakaribia kutua Besiktas kwa uhamisho wa Euro 10 milioni. Staa huyo ambaye alijiunga na Forest mwaka jana kwa Euro 7 milioni katika msimu wake wa kwanza alicheza mchi 32 na kufunga mabao matatu. Hadi kufikia jana alidaiwa kuwasili Istanbul ili kukamilisha mchakato wa uhamisho.
Manu Kone
INTER Milan imeanza kumnyemelea kiungo wa AS Roma na timu ya taifa ya Ufaransa, Manu Kone, 24, baada ya Roma kutangaza kuwa inahitaji kuuza wachezaji kutokana na sheria za Financial Fair Play. Roma ilikataa ofa kutoka Inter Milan msimu uliopita, lakini sasa inajiandaa kusikiliza mapendekezo kwa ajili ya mchezaji huyo ambaye ipo tayari kumuuza. Kone amekuwa katika rada za Inter muda.
Ademola Lookman
JUVENTUS inaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Atalanta na timu ya taifa ya Nigeria, Ademola Lookman, 27, kuelekea dirisha lijalo la majira ya baridi. Mabosi wa Juventus wanamwangalia kuwa mbadala wa straika wa kimataifa wa Serbia, Dusan Vlahovic ambaye kuna asilimia kubwa akauzwa katika dirisha la majira ya baridi.
Anthony Martial
MSHAMBULIAJI wa AEK Athens na Ufaransa, Anthony Martial, 29, anadaiwa kuwa katika hatua za mwisho kujiunga na Monterrey ya Mexico. Martial aliyejiunga na AEK 2024 kwa mkataba wa miaka mitatu, alivunjiwa mkataba na timu hiyo ambayo inashiriki Uefa Conference League. Awali alikuwa akifanya mazungumzo na Pumas ya huko huko Mexico, lakini walishindwa kufikia mwafaka.