Bondia adaiwa kuuawa kwa kuchomwa moto Sauzi
Muktasari:
- Bondia huyo alikuwa ameoa mwanamke raia wa Afrika Kusini na alikuwa baba wa mtoto mmoja. Pia alikuwa akifahamika kama mshirika wa mazoezi (sparring partner) wa bondia maarufu Junior Makabu.
TAARIFA kutoka Afrika Kusini zinadai kwamba, Bondia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Roméo Katompa Kaboya, maarufu kwa jina la "Bololo", ameripotiwa kuuawa kwa kuchomwa moto ndani ya nyumba yake katika tukio linalodaiwa kuhusishwa na chuki dhidi ya wageni (xenophobia).
Bondia huyo alikuwa ameoa mwanamke raia wa Afrika Kusini na alikuwa baba wa mtoto mmoja. Pia alikuwa akifahamika kama mshirika wa mazoezi (sparring partner) wa bondia maarufu Junior Makabu.
Picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha nyumba iliyoteketea kabisa kwa moto kuanzia ghorofa ya chini hadi ya juu. Ndani ya chumba cha kulala, mwili wa Katompa ulipatikana ukiwa umelala kifudifudi na ukiwa umeungua vibaya kiasi cha kutambulika kwa shida.
Kifo cha Katompa kimewashtua raia wa DR Congo na jamii pana ya Waafrika, huku kikifufua tena hofu kuhusu usalama wa wahamiaji nchini Afrika Kusini. Tukio hilo pia limezua wasiwasi kuwa vitendo vya uhasama dhidi ya wageni vinaendelea, huku baadhi ya watu wakidai vinaonekana kuvumiliwa kimya kimya na mamlaka za nchi hiyo.
Bondia huyo aliyenza kupanda ulingoni rasmi Julai 20, 2018, amepigana mapambano sita, akishinda manne yote kwa KO, huku akipoteza mawili yote kwa KO.
Akiwa anacheza kwa staili ya orthodox, bondia huyo mzaliwa wa Mbuji-Mayi nchini DR Congo, alikuwa akiishi eneo la Gauteng, Afrika Kusini.
Kabla ya kuripotiwa kifo chake, mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Novemba 8, 2025 alipopoteza pambano dhidi ya Tamba Merlin lililofanyika Kigali, Rwanda.
Licha ya taarifa za kifo cha bondia huyo kusambaa kwa kasi, mamlaka za Afrika Kusini bado hazijathibitisha juu ya tukio hilo.