Vigogo Ulaya wapigania saini Kone
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Africafoot, nyota huyo mwenye umri wa miaka 17 amekuwa kivutio kikubwa na anatajwa kuwindwa na klabu hizo kubwa za Ulaya katika vita vya usajili vyenye thamani ya takriban Euro 50 milioni.
BARCELONA na Real Madrid zinachuana na Manchester City pamoja na Paris Saint-Germain kuwania saini ya kiungo wa Villarreal mwenye umri wa miaka 17, Moussa Kone.
Kwa mujibu wa Africafoot, nyota huyo mwenye umri wa miaka 17 amekuwa kivutio kikubwa na anatajwa kuwindwa na klabu hizo kubwa za Ulaya katika vita vya usajili vyenye thamani ya takriban Euro 50 milioni.
Hata hivyo, Villarreal inaelezwa kwamba inafikiria kuongeza bei kutokana na mahitaji yaliyojitokeza kutoka kwa klabu mbalimbali zilizowasilisha nia ya kumtaka mchezaji huyo, miongoni mwazo zikiwamo za Italia ingawa hazijawekwa wazi hadi sasa.
Kulingana na taarifa za Africafoot kuna uwezekano mkubwa mchezaji huyo akaondoka mwisho wa msimu, lakini timu itakayokuwa na uhakika kumnasa itafanikisha dili hilo mapema Januari, 2027 ili amalizapo msimu aweze kuondoka na kwenda kujiunga na kikosi chake kipya kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Mchezaji huyo tayari amekuwa na ushawishi wa kipekee katika eneo la katikati ya uwanja analocheza, ambapo katika timu ya vijana wa chini ya miaka 19 ya Villarreal anapambana vilivyo na wachezaji mahiri, jambo ambalo pia limezishawishi timu zingine kubwa kukiona kipaji chake na kuanza kukifuatilia kwa karibu.
LEVI COLWILL
LIVERPOOL bado wanamuwania beki wa kati wa kimataifa wa England na Chelsea, Levi Colwill, lakini matajiri wa Jiji la London hawana mpango wa kuingia kwenye mazungumzo ya kumuuza na badala yake wanapanga kumpa mkataba mpya.
Hata hivyo, Colwill anafikiria zaidi kuondoka katika kikosi hicho ifikapo mwisho wa msimu ili kukwepa kujikuta katika wakati mgumu wa namba kwani timu hiyo inakusudia kufanya usajili mwingine mkubwa.
ALEJANDRO BALDE
ARSENAL inamfuatilia beki wa kushoto wa kimataifa wa Hispania na Barcelona, Alejandro Balde. Hata hivyo, mabingwa wa Ligi Kuu Hispania (La Liga), Bara, wanapanga kufanya biashara ya kubadilishana wachezaji moja kwa moja, ambapo Balde atahamia Arsenal huku Piero Hincapie akienda Barcelona, bila fedha kuhusika katika dili hilo.
MIKEL MERINO
MIKEL Merino anafikiria kuondoka Arsenal ikiwa hatahakikishiwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara. Kiungo huyo ana hofu ya kupoteza nafasi yake katika kikosi cha timu ya taifa ya Hispania na yupo tayari kutafuta njia ya kuondoka ikiwa italazimika. Kipaumbele chake ni kurejea Ligi Kuu Hispania (La Liga).
ALISSON BECKER
VIGOGO wa Flamengo wamejadili juu uwezekano wa kumsajili kipa wa kimataifa wa Brazil na Liverpool, Alisson Becker mwakani. Kulingana na Sport Witness, Becker mwenye umri wa miaka 34 ameshazungumza pia na menejimenti yake ili kwenda kuanza maisha mapya nyumbani kwao, Brazil. Liverpool haijasema lolote.
GAVI
KOCHA wa Bayern Munich, Vincent Kompany, amemtaja kiungo wa Barcelona, Pablo Martín Paez Gavira maarufu kama Gavi, kuwa ndiye chaguo lake la kwanza katika eneo la kiungo kwenye usajili wa dirisha kubwa la mwakani, mwaka.
Kwa mujibu wa Juan Jesus, Kompany anamtaka Gavi akasaidiane na mkongwe Joshua Kimich katika dimba la kati na mastaa wengine kikosini hapo.
TINO LIVRAMENTO
NEWCASTLE United itajaribu kumuuza beki wa kulia, Tino Livramento, ikiwa hakutakuwa na maendeleo katika mazungumzo ya kuongeza mkataba wake kabla ya majira ya kiangazi yajayo.
Arsenal na Manchester City zote zinamtaka nyota huyo wa timu ya taifa ya England na lolote linaweza kutokea kuanzia sasa hadi mwakani.
ALESSANDRO BASTONI
NYOTA anayetamaniwa zaidi na Barcelona, beki wa Inter Milan, Alessandro Bastoni ameiweka Barca katika mtihani, kwani ikiwa dili la kumsajili staa huyo wa Italia halitawezekana, basi klabu hiyo inawafikiria wachezaji kama Natan wa Real Betis na Youri Baas wa Ajax mwenye umri wa miaka 23. El Nacional inadai mkakati wa kumg'oa Bastoni huko Inter unakwenda vizuri.
NNAMDI COLLINS
BEKI wa kimataifa wa Ujerumani na Eintracht Frankfurt, Nnamdi Collins, mwenye umri wa miaka 22, ameingia katika rada za Chelsea, Liverpool na Manchester United ambazo zimeanza kupimana ubavu kwa ajili ya kumsajili wakati wa dirisha dogo la usajili wa Januari, 2027.
Kwa mujibu wa fussball-news, mchezaji huyo ameshakubaliana maslahi na mojawapo wa timu hizo.
YOUSSOUF FOFANA
TOTTENHAM Hotspur na Juventus zote zinapanga kujaribu kumsajili kiungo wa kimataifa wa Ufaransa na AC Milan, Youssouf Fofana, majira ya kiangazi yajayo baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa mkopo Sevilla.
Kulingana na Ficherio, mchezaji huyo wa Sevilla anafikiria ofa nyingi zilizowasilishwa mezani kwake kabla ya kuamua atatimkia wapi.
CASTELLO LUKEBA
BEKI wa kati wa RB Leipzig, Mfaransa Castello Lukeba anayepigiwa upatu na Barcelona katika nafasi hiyo iwapo itaachana na Alejandro Balde ambaye hana namba ya uhakika kikosini huko Camp Nou kwa sasa.
Lukeba amekuwa katika kiwango bora msimu huu katika Ligi Kuu Ujerumani ambako amecheza zaidi ya dakika 433 msimu huu.