Bruno mguu mmoja nje Man United
Muktasari:
- Hata hivyo, ofa kutoka Al Hilal inatarajiwa kuwasilishwa kwa Manchester United mwezi Januari, huku vigogo hao wa Saudi Arabia wakiwa tayari kulipa Dola 61 milioni ili kumsajili Fernandes katika dirisha la usajili wa majira ya baridi.
NAHODHA wa Manchester United, Bruno Fernandes, anatarajia kuondoka klabuni hapo na kujiunga na timu nyingine kubwa barani Ulaya ifikapo Januari, mwakani au mapema mara tu baada ya kufunguliwa kwa dirisha kubwa la usajili lijalo.
Hata hivyo, ofa kutoka Al Hilal inatarajiwa kuwasilishwa kwa Manchester United mwezi Januari, huku vigogo hao wa Saudi Arabia wakiwa tayari kulipa Dola 61 milioni ili kumsajili Fernandes katika dirisha la usajili wa majira ya baridi.
Taarifa zinaeleza kwamba nyota huyo wa kiungo wa kimataifa wa Ureno amekuwa katika hali ya sintofahamu tangu alipokosoa mbinu na mikakati ya Kocha Michael Carrick katika ufundishaji jambo ambalo lilimsababishia kuwekwa benchi katika mchezo dhidi ya Bournemouth uliopigwa katika Uwanja wa Oldr Trafford.
Kinachoelezwa kwa sasa ni kwamba, kambi ya mchezaji huyo imeshaanza mazungumzo na klabu mbalimbali Ulaya ili kufikia makubaliano binafsi kabla mchezaji huyo hajawasilisha ombi maalumu kwa uongozi wa Mashetani Wekundi ili aweze kuondoka klabuni.
Wakati hayo yakiendelea taarifa zingine zinadai kwamba vigogo wa Hispania, Atletico Madrid wameulizia juu ya uwezekano wa kumsajili mchezaji huyo ili akaimalishe eneo la kiungo la kikosi chao ambalo limekuwa halina uthabiti katika miezi ya karibuni kutokana na kuandamwa na majeruhi kibao. Hata hivyo, Atletico haijawasilisha ofa yoyote kwa uongozi wa Manchester United kutaka saini ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32. Mkataba wa Bruno unamalizika Juni 30, 2027.
Marcus Rashford
MSHAMBULIAJI wa Manchester United na England, Marcus Rashford anadaiwa kwamba anaweza kufikiria kuondoka katika timu hiyo moja kwa moja iwapo atapata nafasi ndogo ya kucheza baada ya kurejea kutokana na majeraha aliyokumbana nayo hivi karibuni. Taarifa za ndani zinaeleza kwamba Rashford hata kabla ya majeraha alikuwa anapima upepo kabla ya kuwasilisha ombi la kusepa.
Gavi
KOCHA wa Aston Villa, Unai Emery, anatarajiwa kujaribu kumshawishi kiungo wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania Pablo Martín Paez Gavira maarufu Gavi kutua katika kikosi anachokinoa. Gavi anadaiwa kwamba hana furaha katika kikosi cha Barcelona kutokana na ugumu wa upatikanaji wa namba katika kikosi cha kwanza.
Estevao
CHELSEA wameondoa uwezekano wa kumruhusu winga wa kimataifa wa Brazil, Estevao Willian Almeida de Oliveira Goncalves maarufu Estevao kuondoka klabuni hapo kufuatia taarifa kuhusu kuvutiwa kwake na Barcelona au Manchester United. Badala yake, The Blues watapambana kuhakikisha kwamba wanampa mchezaji huyo mkataba mpya.
Nicolo Tresoldi
MANCHESTER City na Chelsea zote zimegongana zikimfuatilia mshambuliaji wa kimataifa wa Ujerumani na Club Brugge, Nicolo Tresoldi. Timu hizo mbili za England ziko mbele ya AC Milan na Juventus katika mbio za kuwania saini ya mchezaji huyo mzaliwa wa Italia ambaye amekuwa katika kiwango bora siku za karibuni.
Conor Gallagher
LICHA ya taarifa za Tottenham Hotspur kudai kwamba kiungo wake wa kimataifa wa England, Conor Gallagher anafuatiliwa na timu kibao ikiwano Eveton, lakini vipaumbele vya Everton katika usajili viko sehemu nyingine, ambapo inataka kusajili mshambuliaji mpya na beki wa pembeni.
Javi Rodriguez
BEKI wa kati wa kimataifa wa Hispania na Celta Vigo, Javi Rodriguez, mwenye umri wa miaka 23, anadaiwa kuwa katika rada ya timu tano ikiwamo nne za Ligi Kuu Engalnd ambazo ni Bournemouth, Everton, Fulham na Newcastle United, huku PSG ya Ufaransa nayo ikiitaka saini yake. Inaelezwa kwamba licha ya chama lake kutokuwa katika fomu, lakini kiwango chake kunazikuna timu kibao Ulaya.
Alejandro Balde
LIVERPOOL na AC Milan zinataka kupimana ubavu na Manchester United katika mbio za kumsajili beki wa kushoto wa kimataifa wa Hispania na Barcelona, Alejandro Balde. Beki huyo ambaye amekuwa hana namba ya uhakika siku za karibuni huko Barca, anavutiwa kuondoka ili kwenda kusaka timu itakayompa nafasi kikosini.
Lamine Camara
WAKATI Chelsea sasa ikiwa imeelekeza nguvu katika kumsajili kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, upande wa Liverpool wanataka kutumia fursa hiyo kwa kufanya jaribio la kumsajili Lamine Camara wa Monaco mwezi Januari. Camara alikaribia kuhamia Stamford Bridge katika dirisha lililopita la usajili na amekuwa akitamani kufanya hivyo siku zijazo.
Riccardo Calafiori
KOCHA wa Real Madrid, Jose Mourinho, amewasilisha kwa uongozi jina la beki wa kushoto wa Arsenal, Riccardo Calafiori kama kipaumbele chake cha juu katika kuimarisha nafasi hiyo. Hata hivyo, taarifa kutoka Arsenal zinadai kwamba haina mpango wa kusikiliza ofa yoyote kuhusu mchezaji huyo kwa sasa.
Brahim Diaz
FENERBAHCE wamewasilisha ofa kwa uongozi wa Real Madrid ili kumsajili kiungo Brahim Díaz, ambayo haihusishi ada ya uhamisho, badala yake, timu hiyo ya Uturuki itatoa haki yake ya asilimia 20 ya kupata sehemu ya fedha za mauzo ya Arda Guler anayeitumikia Real Madrid. Guler alitua Madrid akitokea katika timu hiyo.