Vietnam yajenga uwanja mkubwa wa kushangaza
Muktasari:
- Uwanja huo unaoitwa VinFast Trong Dong, unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 135,000, huku wafanyakazi wakifanya kazi muda wote kwa lengo la kukamilisha ujenzi wake ifikapo Julai 2027.
HANOI, VIETNAM: UWANJA mkubwa zaidi wa soka duniani unaendelea kujengwa kwa kasi mjini Hanoi, Vietnam, huku picha mpya zikionyesha namna eneo hilo linavyoanza kubadilika na kuwa moja ya viwanja vya kuvutia zaidi duniani.
Uwanja huo unaoitwa VinFast Trong Dong, unatarajiwa kuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 135,000, huku wafanyakazi wakifanya kazi muda wote kwa lengo la kukamilisha ujenzi wake ifikapo Julai 2027.
Awali, uwanja huo ulitarajiwa kukamilika katika majira ya kiangazi ya mwaka 2028, lakini kasi ya ujenzi imeongeza matumaini ya kukamilika mapema zaidi.
Jina la uwanja huo limetokana na ngoma ya shaba ya jadi ya Vietnam, maarufu kama Trong Dong, huku muundo wake ukiwa umeandaliwa kuakisi umbo la ngoma hiyo.
Uwanja huo unatarajiwa kuwa na paa kubwa zaidi linaloweza kufunguka na kufungwa kikamilifu, huku michoro ya usanifu ikionyesha kuba kubwa la duara lenye rangi ya dhahabu litakaloufanya uwanja huo kuwa wa kipekee.
Picha mpya kutoka eneo la ujenzi zimeonyesha minara mikubwa yenye urefu wa takribani mita 80 ikianza kujengwa katika maeneo mbalimbali ya uwanja, huku magreda na korongo kubwa zikiendelea kufanya kazi.
Ujenzi huo ni sehemu ya mpango mkubwa wa kutengeneza Jiji la Michezo la Olimpiki, ambalo linatarajiwa kuwa mwenyeji wa matukio mbalimbali ya kimataifa.
Kwa mujibu wa Reuters, mradi huo unahusisha eneo la takribani ekari 22,200 pembezoni mwa Hanoi.
Uwanja huo utakapokamilika ukiwa na uwezo wa mashabiki 135,000, utakuwa mkubwa kuliko uwanja wowote wa soka duniani na zaidi ya mara mbili ya uwezo wa Uwanja wa Emirates wa Arsenal.
Kwa sasa, rekodi ya uwanja mkubwa zaidi duniani inashikiliwa na Rungrado 1st of May Stadium ya Pyongyang, Korea Kaskazini, wenye uwezo wa kuchukua takribani mashabiki 114,000.
Ukubwa huo utafuatiwa na Camp Nou ya Barcelona wenye uwezo wa sasa wa 99,354, ingawa baada ya ukarabati unaoendelea kukamilika, uwezo wake unatarajiwa kufikia 105,000.
Uwanja wa FNB (Soccer City) wa Johannesburg, Afrika Kusini, uliotumika kuandaa fainali ya Kombe la Dunia 2010, unashika nafasi ya tatu ukiwa na uwezo wa mashabiki 94,736.
Nafasi ya nne inashikiliwa na Uwanja wa New Administrative Capital wa Misri, wenye uwezo wa 93,940, huku Uwanja wa Wembley, England ikiwa ya tano kwa uwezo wa mashabiki 90,000.
Wakati huohuo, Grand Stade Hassan II wa Morocco unaoendelea kujengwa kwa ajili ya Kombe la Dunia 2030, unatarajiwa kuwa na uwezo wa mashabiki 115,000 utakapokamilika, hivyo pia utaingia kwenye orodha ya viwanja vikubwa zaidi duniani.