MISS WORLD TANZANIA: Latricia aibuka na mataji matatu, kuiwakilisha Tanzania Vietnam
Muktasari:
- Shindano hilo lililoandaliwa na kampuni ya 361 Afrika chini ya Mkurugenzi Mustafa Hassanali, liliwakutanisha jumla ya warembo 20 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo Latricia aliibuka mshindi kwa kuonyesha uwezo wa kipekee katika vipengele mbalimbali vya ushindani.
MREMBO wa jijini Dar es Salaam, Latricia Ian ameandika historia baada ya kutwaa taji la kwanza kabisa la Miss World Tanzania katika shindano lililofanyika usiku wa kuamkia Aprili 20, 2026, katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki.
Shindano hilo lililoandaliwa na kampuni ya 361 Afrika chini ya Mkurugenzi Mustafa Hassanali, liliwakutanisha jumla ya warembo 20 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo Latricia aliibuka mshindi kwa kuonyesha uwezo wa kipekee katika vipengele mbalimbali vya ushindani.
Mbali na kutwaa taji kuu, Latricia pia aling’ara kwa kushinda mataji mengine mawili muhimu ambayo ni Talent Award (Tuzo ya Kipaji) pamoja na People’s Choice Award (Tuzo ya Chaguo la Watu), hatua iliyodhihirisha ukubwa wa ushawishi wake kwa majaji na umma kwa jumla.
Kwa ushindi huo, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 24 ameondoka na zawadi ya gari aina ya Mercedes-Benz A-Class lenye thamani ya zaidi ya Sh40 milioni, fedha taslimu Sh10 milioni, bima ya safari pamoja na taji, huku jumla ya thamani ya zawadi hizo ikifikia zaidi ya Sh100 milioni.
Tuzo hizo zilikabidhiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, aliyemwakilisha Waziri Paul Makonda.
Aidha, Latricia alivishwa taji hilo na Miss World anayetawala Opal Suchata Chuangsri kutoka Thailand, akishirikiana na Miss World Afrika Hasset Dereje Admassu.
Ushindi wake unaashiria mwanzo mpya kwa mashindano ya Miss World Tanzania, huku macho ya wengi yakielekezwa kuona kama ataweza kuendeleza mafanikio hayo katika jukwaa la dunia nchini Vietnam.
Katika matokeo hayo, Nouru Masoud alishika nafasi ya pili na kushinda tuzo ya Sports Challenge Award, huku Paulina Allute akimaliza katika nafasi ya tatu.
Wengine walioingia tano bora ni pamoja na Silya Mussa (nafasi ya nne) na Diana Rutagalinda (nafasi ya tano).
Washindi wengine wa mataji maalum ni pamoja na Silya Mussa aliyeshinda Beauty with Purpose, Jackline Nyabisi aliyeshinda Head to Head Challenge, Diana Rutagalinda aliyeshinda Clean Cooking Award na Multimedia Challenge, pamoja na Sharon Cesari wa Zanzibar aliyeshinda tuzo ya Best Evening Gown.
Akizungumza baada ya ushindi wake, Latricia amesema haikuwa kazi rahisi kushinda taji hilo kutokana na ushindani na warembo wengine.
Amesema kwake warembo wote ni washindi na anajivunia kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Miss World yatakayofanyika Vietnam kuanzia Agosti 9 hadi Septemba 5, 2026, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 75 ya shindano hilo.
“Mashindano yalikuwa magumu na kwa kweli kila mrembo alikuwa na nia ya kushinda. Mimi nimeshinda na hapa sasa ndiyo mwanzo wa safari yangu mpya katika fani ya urembo,” amesema Latricia.
Amesema anatarajia kufanya vyema katika mashindano ya dunia na hivyo anahitaji sapoti kubwa kutoka kwa Watanzania na wadau wote wa urembo.
“Nitatumia mashindano ya dunia kuonyesha utamaduni wa Tanzania na kuitangaza nchi,” amesema.
“Nimejiandaa kikamilifu kuhakikisha ninafanya vizuri na kuiwakilisha nchi yangu kwa heshima kubwa. Hii ni nafasi ya kipekee kuonyesha uwezo wa Watanzania duniani,” amesema Latricia.
Kwa upande wake, muaandaaji wa mashindano hayo, Mustafa Hassanali amesema mafanikio ya mashindano hayo yametokana na sapoti kutoka kwa wadau mbalimbali, wadhamini na serikali chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan.
Amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inayoongozwa na Waziri Paul Makonda, Katibu Mkuu, Gerson Msigwa na Baraza la Sanaa (Basata) wamempa sapoti kubwa kufanikisha mashindano hayo.
Hassanali amesema kuwa kazi ndiyo imeanza na anatarajia kufanya mashindano hayo kubwa bora huku akiomba msaada zaidi kutoka serikalini kwani mashindano ya Miss World Tanzania ni jukwaa la vijana katika kutafuta fursa mbalimbali.
Msigwa
Akizungumza katika usiku huo, Msigwa ambaye alimwakilisha Waziri Paul Makonda aliwapongeza waandaaji na wadau kwa kunakisha mashindano hayo ambayo mbali ya kuongeza fursa kwa vijana, pia yanaitangaza nchi nje ya mipake yake.
Msigwa amesema kampuni ya Miss World Limited kwa sasa inamtambua Hassanali kuwa mwandaaji wa pekee ambaye mshindi wake anaiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia, baada ya kazi hiyo awali kufanywa na Lino International Agency na The Look.
Amesema bado kuna firsa kubwa kwa waandaaji wengine kuandaa mashindano nchini na kuitangaza nje na kuwataka wadau kuchangamkia fursa hiyo.
“Pia tuna Miss Universe na Miss Grand International, lakini bado kuna mengine ambayo hayana waandaaji, naomba wadau kutumia fursa hiyo kuandaa hapa nchini,” amesema.
Ulikuwa usiku wa Burudani
Usiku huo ulikuwa na kila aina ya burudani ambayo iliwafanya mashabiki kupata thamani halisi ya fedha walizolipia kiingilio.
Kwanza ilianza burudani ya warembo ambao walionyesha ustali mkubwa katika kucheza ngoma mbalimbali za asili ya Tanzania. Warembo hao walianza kucheza ngoma la kabira la Wamasaai, wasukuma, wahaya, miondoko ya Pwani na kuchanganya na sengeli.
Pia JK Commedy naye alichangamisha jukwaa na baadaye Wanne Star aliingia na wimbo wake Asili Yetu ambapo mmoja wa msanii wake alionyesha ustadi mkubwa wa kucheza na nyoka.
Dakika 23 za Ali Kiba
Kabla ya kutangazwa kwa mshindi, mashabiki wa masuala ya urembo waliopata burudani safi ya kutoka kwa mwanamuziki, Ali Kiba ambaye aliingia kwa mtindo wa Mega Mix yenye nyimbo maarufu kama Mahaba, Seduce Me, Aje, Finale na nyinginezo.