Victor Oladipo aomba nafasi ya pili NBA
Muktasari:
- Mchezaji huyo wa zamani wa All-Star na mshindi wa tuzo ya Mchezaji Aliyeboreshwa Zaidi wa Mwaka (Most Improved Player), hajacheza NBA tangu 2023, lakini amedai kwamba anaamini hatimaye amerejea katika hali nzuri kiafya baada ya miaka kadhaa aliyokumbana na majeraha.
MIAMI, MAREKANI: NYOTA wa zamani wa Ligi ya Kikapu Marekani (NBA), Victor Oladipo ametoa ombi kwa mameneja wakuu wa timu za NBA, akitaka kupewa nafasi nyingine katika maisha yake kurejea uwanjani wakati mmoja akionekana kuelekea kwenye kiwango cha kuwa supastaa wa mchezo huo.
Mchezaji huyo wa zamani wa All-Star na mshindi wa tuzo ya Mchezaji Aliyeboreshwa Zaidi wa Mwaka (Most Improved Player), hajacheza NBA tangu 2023, lakini amedai kwamba anaamini hatimaye amerejea katika hali nzuri kiafya baada ya miaka kadhaa aliyokumbana na majeraha.
Katika barua ndefu na yenye hisia kali iliyochapishwa na The Players’ Tribune, Oladipo alieleza safari yake tangu alipochaguliwa katika nafasi ya pili kwa jumla katika NBA Draft 2013 hadi kuwa mchezaji wa All-Star akiwa na Indiana Pacers, pamoja na athari za kimwili na kihisia zilizosababishwa na majeraha yaliyobadili mwelekeo wa maisha yake.
Na sasa akiwa na umri wa miaka 34, Oladipo anataka nafasi nyingine, ambaye alitumia misimu mitatu Orlando kabla ya kuuzwa Oklahoma City Thunder ambako alicheza pamoja na Russell Westbrook, amekuwa akijifua vilivyo akisaka ubora kabla ya kuomba kurejea.
Rekodi zake zinaonyesha kwamba baada ya kuondoka Thunder alihamia Indiana ambako maisha yake yalifikia kileleni katika msimu wake wa kwanza 2017/18. Katika msimu huo alikuwa akifunga wastani wa pointi 23.1, akikusanya ribaundi 5.2 na kutoa asisti 4.3 kwa kila mchezo. Aliteuliwa kuwa mchezaji wa NBA All-Star, akashinda tuzo ya Mchezaji Aliyeboreshwa Zaidi wa Mwaka, na akaisaidia Indiana kuisukuma Cleveland Cavaliers ya LeBron James hadi mchezo wa saba katika raundi ya kwanza ya mchujo (playoffs).
Lakini kupanda kwake kwa kasi kulifuatiwa na anguko, ambapo Januari 2019 alipata jeraha la kupasuka kwa kano ya misuli ya paja kwenye goti la kulia wakati wa mchezo dhidi ya Toronto Raptors ambalo lilihitaji upasuaji na kumuweka nje ya uwanja kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Ingawa baadaye alirejea uwanjani, Oladipo alidai kwamba aliendelea kusumbuliwa kimwili na kiakili, akieleza jinsi alivyokuwa akicheza akiwa na maumivu na kujiuliza kwa nini mwili wake haukuwa ukijibu kwa namna alivyotarajia.
Kufikia wakati Indiana ilipomuuza kwenda Houston Rockets Januari 2021, karibu miaka miwili baada ya kupata jeraha hilo, alikuwa amefikia hatua ya kuvunjika moyo kucheza. “Sikuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kulia,” Oladipo aliwahi kuandika.
JERAHA JINGINE MIAMI HEAT
Oladipo aliendelea na maisha yake ya NBA akiwa na Miami Heat akicheza michezo 42 katika msimu wa 2022/23 na kuisaidia timu hiyo ambayo baadaye ilifika fainali za NBA. Lakini, jeraha jingine kubwa lilifuata ambapo katika mfululizo wa michezo ya mchujo (playoffs) dhidi ya Milwaukee Bucks Aprili 2023 alipapasuka kano kwenye goti la kushoto.
Lilikuwa pigo jingine kubwa kwa mchezaji ambaye tayari alikuwa ametumia miaka kadhaa akijaribu kurejea katika kiwango kilichomfanya kuwa miongoni mwa walinzi bora wa ligi. Katika barua yake, Oladipo alisema jeraha hilo lilimlazimisha hatimaye kupunguza kasi ya harakati zake za kutaka kurejea katika kiwango alichokuwa nacho kwanza.
Alidai kwamba ametumia miaka mitatu iliyopita kujijenga upya kimwili na kiakili mchakato ukihusisha matibabu ya kurejesha nguvu, mazoezi na tiba ya kisaikolojia.
Lakini baada ya miaka kadhaa akiwa nje ya NBA, sasa anasema yupo tayari kujaribu tena, akidai: "Ninaamini mwili wangu hatimaye uko sawa.
Ninaamini bado nina kiwango bora cha kikapu na muhimu zaidi, kikapu cha ushindi. Ninaamini naweza kuwa mchezaji mwenye mchango mkubwa ndani ya chumba cha timu ya NBA. Ninachoomba sasa ni nafasi ya kuthibitisha hilo. Kama kuna timu itakayonipa nafasi niko tayari.”
Mwezi Julai, aliandaa Pro Day binafsi huko Las Vegas wakati wa Ligi Ndogo ya Kiangazi (Summer League), akiwapa viongozi, maskauti na makocha wa NBA nafasi ya kumuona na kumtathmini moja kwa moja, ambapo Sacramento Kings ilikuwa miongoni mwa timu zilizoripotiwa kutazama mazoezi yake. Pia alitumia sehemu ya msimu wa 2025/26 kuthibitisha kwamba bado anaweza kushindana, akicheza michezo 33 katika G League na kufikisha wastani wa pointi 13.5, ribaundi 4.6 na asisti 3.9 kwa kila mchezo.
Baadaye Sacramento Kings iliibuka kama moja ya timu zilizoweza kuwa sehemu yake ya kwenda, huku taarifa za Agosti zikidai timu hiyo ilikuwa ikimfikiria Oladipo pamoja na walinzi wengine wenye uzoefu, ikiwa inatafuta mchezaji mkongwe ambaye angeweza kumsaidia kumlea na kumshauri mchezaji mpya Darius Acuff Jr. Hata hivyo, bado hakukuwa na mkataba wa NBA uliokuwa ukimsubiri Oladipo.
Na sasa, hata hivyo, inaonekana mlango mwingine umeanza kufunguka, ambapo Miami Heat inaripotiwa kufuatilia jitihada zake za kurejea NBA na imemruhusu kufanya mazoezi katika Kituo cha Kaseya, kwa mujibu wa taarifa za mchambuzi wa Heat, Ira Winderman.
Oladipo amekuwa akifanya mazoezi katika uwanja wa timu hiyo huku Miami ikiendelea kufuatilia maendeleo yake, na hii haimaanishi kwamba iko tayari kumsajili kwani hakuna dalili kwamba mkataba uko karibu kukamilika.
Hata hivyo, Miami ni sehemu yenye maana kubwa kwa Oladipo katika jitihada zake za kurejea NBA kwani akiwa hapo ndipo alipoumia goti la kushoto katika jeraha la kano lililomaliza msimu wake wa 2022/23 ambao pia ulikuwa wake wa mwisho kucheza NBA.
Zaidi ya miaka mitatu baadaye, amerejea ndani ya kituo cha mazoezi cha timu ya NBA, akijaribu kuthibitisha kwamba jeraha hilo halitakuwa ndilo litakaloamua mwisho wa maisha yake ya kikapu. Lakini, akiwa na miaka 34 kupata nafasi nyingine NBA siyo jambo la uhakika ingawa yupo wazi kwamba hayupo tayari kuruhusu mtu mwingine aamue kwamba safari yake imefika mwisho.
“Labda kuna timu itakayonipa nafasi. Labda hakuna timu itakayofanya hivyo. Hilo kwa kweli liko mikononi mwenu,” alidai katika barua yake kwa mabosi wa timu 30 zinazoshiriki NBA.