Vardy awindwa akachezee timu mpya Serie A
Muktasari:
- Straika huyo veterani kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kutemwa na Leicester City. Hata hivyo, licha ya kufikisha umri wa miaka 39, Vardy anaweza kutua huko Italia kwenda kuendelea na soka lake.
STRAIKA, Jamie Vardy amewekwa kwenye mchakato wa kujiunga bure na moja ya timu inayoshiriki mikikimikiki ya Serie A.
Straika huyo veterani kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kutemwa na Leicester City. Hata hivyo, licha ya kufikisha umri wa miaka 39, Vardy anaweza kutua huko Italia kwenda kuendelea na soka lake.
Sky Sports inaripoti Cremonese imefanya mawasiliano na mshambuliaji huyo ili akajiunge kwenye timu yao. Mimba hiyo iliyopata daraja msimu huu ilifanikiwa kuichapa AC Milan 2-1 uwanjani San Siro, Jumamosi iliyopita.
Na wanachoamini ni Vardy atawapa nguvu ya kutosha kwenye safu yao ya ushambuliaji ili wasishuke daraja na kurudi Serie B.
Straika huyo veterani alifunga mabao 200 katika mechi 500 alizochezea Leicester.
Vardy alishuhudia uhamisho wa kwenda Italia mapema kwenye dirisha hili ukikwama baada ya kufikia makubaliano kabisa ya kujiunga na Genoa, kabla ya kocha Patrick Vieira kusitisha dili hilo na kukubaliwa na mabosi wa klabu.
Nicolas Jackson
BAYERN Munich imefikia makubaliano na Chelsea ya kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa klabu hiyo, Nicolas Jackson, 24, dirisha hili. Jackson aliyejiunga na Chelsea akitokea Villarreal mwaka 2023 kwa dau la Pauni 32 milioni, msimu uliopita alifunga mabao 17 katika mashindano yote. Bayern inataka kuongeza machaguo zaidi katika safu yao ya ushambuliaji ili kutopata tabu pale Harry Kane anapokumbwa na majeraha.
Kobbie Mainoo
KIUNGO wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Kobbie Mainoo mwenye umri wa miaka 20, anaweza kuondoka katika viunga vya Old Trafford wiki ya mwisho ya dirisha hili la usajili ikiwa klabu itapokea ofa nzuri. Mainoo ambaye ni zao la akademi ya Man United, anahusishwa sana na Chelsea lakini hadi sasa timu hiyo haijawasilisha ofa ili kumsajili. Kitendo cha kuwekwa benchi ndiyo kinamfanya awaze kuondoka.
Manuel Akanji
CRYSTAL Palace imewasilisha ofa ya Pauni 15 milioni Manchester City kwa ajili ya beki wa klabu hiyo, Manuel Akanji, 30. Akanji aliyejiunga na Man City mwaka 2022 akitokea Borussia Dortmund kwa Pauni 15 milioni, anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji ambao Kocha Pep Guardiola ameruhusu wauzwe. Akiwa Man City ameshinda mataji yote makubwa ikiwemo Ligi ya Mabingwa mwaka 2023.
Rasmus Hojlund
MSHAMBULIAJI wa Manchester United, Rasmus Hojlund, 22, yupo katika hatua nzuri za kujiunga na Napoli dirisha hili baada ya timu hiyo kufikia naye mwafaka katika masuala ya maslahi binafsi. Kwa mujibu wa tovuti ya Gazzetta dello Sport, Hojlund atakamilisha usajili huo kabla ya dirisha hili kufungwa. Hojlund alisajiliwa na Man United kwa Pauni 72 milioni kutoka Atalanta mwaka 2023.
Nico Paz
TOTTENHAM omekumbana na pingamizi la nne kwenye mpango wao wa kutaka kumsajili kiungo wa Como, Nico Paz baada ya kukataliwa ofa ya Pauni 50 milioni. Paz, 20, inadaiwa kuuzwa kwa zaidi ya ofa hiyo ambayo Spurs imeiwasilisha kwa sasa. Paz ni nyota wa zamani wa akademi ya Real Madrid, na kiwango chake alichoonyesha akiwa na Como kimeonekana kuzivutia timu nyingi.
Jorgen Strand Larsen
WOLVES inadaiwa kumpa ofa ya mkataba mpya mshambuliaji wao, Jorgen Strand Larsen, 25, ambaye hivi karibuni Newcastle iliweka mezani Pauni 50 milioni ili kumsajili lakini Wolves ikakataa. Licha ya kumsainisha mkataba mpya, Wolves ipo tayari kuzungumza na kumuuza Larsen ikiwa timu inayomhitaji itatoa ofa inayoanzia Pauni 75 mjlioni.
Kostas Tsimikas
MAOFISA wa Roma wanatarajiwa kufanya kikao na Liverpool siku chache zijazo ili kujadili usajili wa beki wa kushoto Majogoo hao, Kostas Tsimikas, 29. Roma inataka sana huduma ya beki huyu lakini changamoto inaonekana kwenye uwepo wa Marseille katika dili hilo kwani yenyewe pia inaitaji huduma ya Kostas na ipo tayari kutoa ofa sawa na ile ambayo Roma inataka kutoa.