Uwanja mpya wa Man United ni kizungumkuti
Muktasari:
- Awali ilikadiriwa kuwa uwanja huo ungegharimu takribani Pauni 2 bilioni wakati mpango huo ulipotangazwa mwaka mmoja uliopita, lakini mchakato wa kununua ardhi karibu na Old Trafford umeonekana kuwa kikwazo kikubwa.
MANCHESTER, ENGLAND: MPANGO wa Manchester United wa kujenga uwanja mpya unakabiliwa na changamoto kubwa ambazo zinaweza kufanya gharama za mradi huo kupanda hadi kufikia Pauni 3 bilioni.
Awali ilikadiriwa kuwa uwanja huo ungegharimu takribani Pauni 2 bilioni wakati mpango huo ulipotangazwa mwaka mmoja uliopita, lakini mchakato wa kununua ardhi karibu na Old Trafford umeonekana kuwa kikwazo kikubwa.
Inadaiwa kuwa Man United iliwasilisha ofa ya takribani Pauni 50 milioni kwa mmiliki wa eneo hilo, kampuni ya usafirishaji ya Freightliner Group, lakini kiasi hicho kimeonekana kuwa ni kidogo kwa mmiliki huyo anayehitaji takribani Pauni 400 milioni.
Inaelezwa kuwa serikali inaweza kutumia utaratibu wa compulsory purchase order ili kulazimisha uuzwaji wa ardhi hiyo na kuamua bei yake rasmi. Hata hivyo, hata kama hilo litafanyika, inakadiriwa kuwa ujenzi wa uwanja huo unaweza kuchukua angalau miaka kumi kukamilika.
Vyanzo vya ndani vinaamini kuwa mmiliki mwenza wa klabu hiyo, Jim Ratcliffe, atalazimika kutafuta walau Pauni 1 bilioni zaidi ili kufanikisha mradi huo mkubwa.
Mtaalamu mmoja wa miradi ya viwanja aliambia gazeti la The Sun kwamba gharama za uwanja huo tayari zimevuka Pauni 3 bilioni na zinaweza kuendelea kupanda kadri muda unavyokwenda.
“Miradi mikubwa kama hii haiwezi kushuka gharama. Kinyume chake, gharama huongezeka kadri muda unavyozidi kwenda. Pia kuna kampuni chache sana duniani zenye uwezo wa kujenga viwanja vikubwa vya kiwango hiki,” alisema.
Aliongeza kuwa hata katika mchakato wa haraka zaidi, ujenzi wa uwanja huo unaweza kuchukua takribani miaka 10 kukamilika.
Wakati huohuo, mtaalamu huyo alionya kuwa baadhi ya kauli za Ratcliffe kuhusu uhamiaji England zinaweza kufanya iwe vigumu kwa klabu hiyo kupata usaidizi wa serikali na mamlaka za mipango miji katika mchakato huo mgumu wa kuidhinisha mradi.