Rekodi za ajabu Kombe la Dunia U-17
Muktasari:
- Tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 1985, yamekuwa na matukio ya kipekee ambayo mengine ni vigumu kuyaamini. Kuna mchezaji aliyefunga bao sekunde tisa tu baada ya filimbi ya mwamuzi kuanza, kipa aliyekaa dakika 572 bila kuruhusu bao na timu iliyofunga mabao 16 katika mchezo mmoja. Hizi ni baadhi ya rekodi zinazovutia katika historia ya mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
IMEZOELEKA kwenye soka kuna rekodi mbalimbali kama za mfungaji bora, golikipa bora, lakini historia ya Kombe la Dunia kwa vijana chini ya miaka 17 ina mambo mengine yanayoweza kukushangaza.
Tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 1985, yamekuwa na matukio ya kipekee ambayo mengine ni vigumu kuyaamini. Kuna mchezaji aliyefunga bao sekunde tisa tu baada ya filimbi ya mwamuzi kuanza, kipa aliyekaa dakika 572 bila kuruhusu bao na timu iliyofunga mabao 16 katika mchezo mmoja. Hizi ni baadhi ya rekodi zinazovutia katika historia ya mashindano hayo yanayosimamiwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
SEKUNDE TISA
Miongoni mwa rekodi za ajabu kwenye historia ya mashindano hayo ilikuwa mwaka 2007 ambapo Brazil kwenye mechi yake ya kwanza ya kundi B iliikaribisha New Zealand katika Uwanja wa Jeju World Cup Stadium, Jeju.
Mashindano hayo yaliyofanyika Korea Kusini ambapo Brazil ilishinda kwa ushindi mnono wa mabao 7-0, Mchezaji wa timu hiyo, Fabinho, aliandika historia kwa kufunga bao sekunde ya tisa tu tangu mchezo kuanza.
Hadi sasa ikiwa mwaka wa 19 sasa rekodi hiyo ya bao la haraka kufungwa kwenye Kombe la Dunia haijavunjwa.
MOROCCO YAANDIKA HISTORIA YA MABAO 16
Mwaka 2025, Morocco iliweka rekodi iliyotikisa historia ya mashindano hayo baada ya kuichapa New Caledonia mabao 16-0 katika hatua ya makundi.
Ushindi huo haukuwa mkubwa tu katika mashindano hayo, bali FIFA ilieleza kuwa ulikuwa ushindi mkubwa zaidi katika historia ya mashindano yote ya soka la wanaume la wachezaji yanayosimamiwa na shirikisho hilo.
KIPA ALIYEDUMU DAKIKA 572
Katika mashindano ya mwaka jana, kipa wa Austria, Daniel Posch, aliweka historia ya kipekee baada ya kukaa dakika 572 bila kuruhusu bao.
Rekodi hiyo ilivunjwa katika fainali dhidi ya Ureno, pale Anisio Cabral alipofunga dakika ya 32. Posch alimaliza mashindano akiwa ameokoa mashuti 20 na kuweka rekodi ya kutoruhusu bao katika mechi sita.
NIGERIA MABAO 26
Mwaka 2013, Nigeria ilifanya vizuri kiasi cha kuandika rekodi ya mabao mengi zaidi yaliyofungwa na timu moja katika mwaka mmoja wa mashindano hayo.
Golden Eaglets ilifunga mabao 26 ilipotwaa ubingwa nchini Falme za Kiarabu. Kelechi Iheanacho alikuwa miongoni mwa nyota walioibeba timu hiyo, akifunga mabao sita na kutoa pasi sita za mabao.
FAINALI YENYE MABAO SABA
Mwaka 2017, England na Hispania ziliweka historia katika fainali iliyokuwa na burudani ya mabao mengi. England ilitoka nyuma na kushinda mabao 5-2, matokeo yaliyofanya fainali hiyo kuwa na mabao saba. Phil Foden na wenzake walitumia ushindi huo kutwaa taji lao la kwanza la U-17.
MABAO 183 KATIKA TOLEO MOJA
India 2017 halikuishia tu kushuhudia fainali yenye mabao mengi, bali lilikuwa pia toleo lililovunja rekodi ya mabao mengi zaidi katika historia ya mashindano hayo kwa mfumo wa timu 24.
Jumla ya mabao 183 yalifungwa katika mechi 52, yakiivunja rekodi ya mabao 172 yaliyofungwa mwaka 2013. Mwaka huo ulionyesha ubora mkubwa kwa washambuliaji waliokuwa na ushindani mkubwa.
BREWSTER NA HAT-TRICK MFULULIZO
Rhian Brewster wa England aliweka rekodi nyingine mwaka 2017 kwa kufunga hat-trick katika mechi mbili mfululizo za hatua ya mtoano.
Alikuwa mchezaji wa kwanza tangu Marcel Witeczek wa Ujerumani Magharibi mwaka 1985 kufanya hivyo. Brewster alifunga bao moja katika fainali dhidi ya Hispania kwenye ushindi wa mabao 5-2. Alimaliza mashindano akiwa na mabao nane, akitwaa Kiatu cha Dhahabu (Golden Boot).
PENALTI 17
Mwaka jana ulikuwa msimu wa ajabu kwenye fainali hizo baada ya kushuhgudia Ireland na Canada zikiingia kwenye mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare katika muda wa dakika 90.
Timu hizo zilifunga jumla ya penalti 17, Ireland ikishinda kwa mikwaju 9-8. FIFA ilieleza kuwa huo ulikuwa mfululizo mrefu zaidi wa penalti katika Kombe la Dunia U-17 tangu mwaka 2013, wakati Mexico ilipoiondoa Brazil kwa mikwaju 11-10.
BRAZIL MECHI 100
Brazil ni miongoni mwa mataifa yenye historia kubwa zaidi katika mashindano hayo. Mwaka 2025, ilifikisha mechi yake ya 100 katika historia ya Kombe la Dunia U-17, ikiwa taifa la kwanza kufikia hatua hiyo.
Takwimu za FIFA zinaonyesha Brazil ilifikisha jumla ya mechi 102 katika mashindano hayo, ikishiriki mara 20 hadi kipindi hicho.
Hizo ni baadhi ya rekodi zinazoonyesha kuwa historia ya U-17 haijajengwa na mabingwa pekee, bali pia matukio ambayo yameacha alama zisizofutika katika soka la vijana.