Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtihani mzito Pochettino anapoikabili Liverpool

Muktasari:

  • Pochettino amekabidhiwa mikoba ya Michael Carrick wakati United ikiwa nafasi ya 18 kwenye msimamo baada ya mechi 10, ikiwa na pointi nane kutokana na ushindi mmoja, sare tano na vipigo vinne. Kocha huyo raia wa Argentina anahitaji matokeo ya haraka kuinusuru timu hiyo inayokabiliwa na hatari ya kushuka daraja.

LIVERPOOL, England: Kocha mpya wa Manchester United, Mauricio Pochettino, leo Jumapili anaanza kibarua chake kwa mtihani mzito wa kuikabili Liverpool katika mchezo wa Ligi Kuu England utakaopigwa kwenye Uwanja wa Anfield.

Pochettino amekabidhiwa mikoba ya Michael Carrick wakati United ikiwa nafasi ya 18 kwenye msimamo baada ya mechi 10, ikiwa na pointi nane kutokana na ushindi mmoja, sare tano na vipigo vinne. Kocha huyo raia wa Argentina anahitaji matokeo ya haraka kuinusuru timu hiyo inayokabiliwa na hatari ya kushuka daraja.

Kwa mujibu wa takwimu za Opta, Liverpool inapewa nafasi kubwa ya kushinda ikiwa na asilimia 57.3 katika majaribio 10,000 ya utabiri, huku United ikiwa na asilimia 20.5 na uwezekano wa sare ukiwa asilimia 22.2.

Hata hivyo, United inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu nzuri baada ya kushinda mechi zote mbili dhidi ya Liverpool msimu uliopita, ikiwamo ushindi wa mabao 2-1 Anfield uliomaliza mfululizo wa mechi tisa bila ushindi uwanjani hapo.

Liverpool, inayofundishwa na Andoni Iraola, inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 18, ikiwa nyuma ya vinara Arsenal kwa pointi tisa. Ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Crystal Palace kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa umeongeza matumaini ya kurejea kwenye mbio za ubingwa.


LIVERPOOL KUKAZA ANFIELD

Licha ya nafasi yake nzuri kwenye msimamo, Liverpool imekuwa na wakati mgumu nyumbani, ikishinda mchezo mmoja pekee kati ya mitano ya ligi iliyocheza Anfield msimu huu, ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Brighton.

Hata hivyo, safu yake ya ushambuliaji imekuwa na makali, Alexander Isak akifunga mabao saba ya ligi msimu huu, huku Florian Wirtz akifunga dhidi ya Crystal Palace na baadaye kuifungia Ujerumani mabao matatu wakati wa mapumziko ya kimataifa.

Cody Gakpo naye ni mchezaji muhimu wa kuangaliwa kutokana na rekodi yake dhidi ya United. Mholanzi huyo amefunga mabao matano dhidi ya Mashetani Wekundu, mengi kuliko aliyofunga dhidi ya timu nyingine yoyote, huku akifunga katika mechi tatu zilizopita alizokutana nao.


POCHETTINO ATABADILISHA MAMBO?

Pochettino anakabiliwa na kazi kubwa ya kuirejesha United kwenye ushindani baada ya kutoshinda mechi nane mfululizo za Ligi Kuu, ikiwa imetoka sare tano na kupoteza tatu.

Timu hiyo pia haijaweka rekodi ya kutoruhusu bao katika mechi zake 10 za mwanzo za ligi msimu huu, huku ikiwa imeruhusu mabao 30 katika mashindano yote, idadi inayolingana na Crystal Palace.

Rekodi ya Pochettino dhidi ya Liverpool nayo si nzuri, akiwa hajashinda mechi zake nane zilizopita dhidi ya timu hiyo, akipoteza sita na kutoka sare mbili akiwa na Tottenham na Chelsea. Kwa jumla, ameshinda mechi tatu pekee kati ya 19 alizokutana na Liverpool.

Hivyo, mchezo wa leo utakuwa kipimo muhimu cha kwanza cha uwezo wake wa kubadilisha mwenendo wa United, hasa katika kurekebisha safu ya ulinzi na kurejesha ushindani dhidi ya wapinzani wao wa jadi.


WACHEZAJI WA KUWAFUATILIA

LIVERPOOL – GAKPO

Gakpo amefunga mabao matano dhidi ya United katika Ligi Kuu, yakiwamo mabao katika kila moja ya mechi zake tatu zilizopita dhidi yao. Msimu huu ana bao moja na asisti tatu, ingawa hajachangia bao katika mechi tano zilizopita za ligi.


MAN UNITED – BRUNO

Nahodha Bruno Fernandes ndiye tegemeo la United katika kutengeneza nafasi na kufunga mabao. Amefikisha michango 149 ya mabao katika Ligi Kuu, akifunga 75 na kutoa asisti 74.

Pia amefunga penalti 28 katika ligi hiyo, akifuatiwa na Alan Shearer (56), Frank Lampard (43), Mohamed Salah (35), Harry Kane (33) na Steven Gerrard (32).