Utata wa Man United kuuzwa
Muktasari:
- Maofisa wa Man United wameripotiwa kushtushwa na maelezo ya ofisa huyo wa serikali ya Saudi Arabia, Alalshikh kudai klabu hiyo ipo kwenye mijadala kwa ajili ya kuuzwa.
MANCHESTER, ENGLAND: IMEFICHUKA. Uvumi ulioibuliwa na Turki Alalshikh juu ya madai ya kuuzwa kwa Manchester United imeelezwa inaweza kuwa ni jambo linalohusu ujenzi wa Uwanja wa Old Trafford.
Maofisa wa Man United wameripotiwa kushtushwa na maelezo ya ofisa huyo wa serikali ya Saudi Arabia, Alalshikh kudai klabu hiyo ipo kwenye mijadala kwa ajili ya kuuzwa.
Alalshikh aliwahi kuhusishwa na mpango wa kuinunua klabu ya Marseille ya Ufaransa miaka miwili iliipita na amekuwa na mijadala na bilionea Rodolphe Saade, ambaye pia alidaiwa kuwa na mpango wa kuinunua Marseille.
Saade ni mwenyekiti na mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya CMA CGM Group, ambayo hivi karibuni ilinunua kampuni ya usafirishaji ya magari makubwa.
Kampuni hiyo ya usafirishaji ya magari makubwa inamiliki ardhi kwenye eneo la karibu na uwanja wa Old Trafford, mahali ambako mmiliki mwenza wa Man United, bilionea Sir Jim Ratcliffe, amepanga kujenga uwanja mpya utakaoingiza mashabiki 100,000 wanaoketi, pembezoni mwa uwanja wa zamani wa Old Trafford ambao una miaka 115.
Saade amekutana mara kadhaa na Alalshikh, ambaye pia alikuwa mmiliki wa klabu ya Hispania ya Almeria hadi mapema mwaka huu na amekuwa maarufu zaidi huko kwao baada ya kupeleka mapambano ya ngumi Saudi Arabia.
Kiongozi wa kikosi kazi cha ujenzi wa Old Trafford mpya, Lord Seb Coe alisafiri kwenda New York, Marekani, Julai mwaka huu kwenda kuzungumza na wawekezaji ili kusaidia mpango huo wa ujenzi wa uwanja mpya. Man United imefanya makadirio ya gharama za ujenzi wa uwanja mpya kwamba unaweza kufikia Pauni 2 bilioni.
Alalshikh alishtua wengi baada ya posti yake kwenye mtandao wa X kuna uwezekano wa Man United kuuzwa na mazungumzo hayo yapo kwenye hatua za mwisho kukamilika.
Serikali ya Saudi Arabia imekuwa ikishutumia kujisafisha kupitia michezo kwa kuanzia mapambano kadhaa ya masumbwi na inamiliki pia klabu ya soka ya Newcastle United.