Ushawishi wa Faouzi CAF wazua hofu sakata la AFCON 2025
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya viongozi wanaamini nguvu ya Lekjaa imekuwa ikiongezeka kupitiliza, hasa kutokana na kushika nyadhifa nyeti ikiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa CAF, Rais wa Shirikisho la Soka Morocco na mjumbe wa FIFA, hali inayompa ushawishi mkubwa kwenye maamuzi ya soka barani humo.
Gazeti maarufu la Ufaransa, L'Équipe limeibua mjadala mzito barani Afrika baada ya kuripoti kuwa ushawishi mkubwa wa Faouzi Lekjaa ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) unazua hofu kwa marais wengi wa vyama vya soka Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya viongozi wanaamini nguvu ya Lekjaa imekuwa ikiongezeka kupitiliza, hasa kutokana na kushika nyadhifa nyeti ikiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa CAF, Rais wa Shirikisho la Soka Morocco na mjumbe wa FIFA, hali inayompa ushawishi mkubwa kwenye maamuzi ya soka barani humo.
Mjadala huo umechochewa zaidi na sakata la AFCON 2025, ambapo Morocco ilitangazwa bingwa baada ya Senegal kunyang’anywa ushindi kufuatia uamuzi wa Bodi ya Rufaa ya CAF.
Katika fainali hiyo, Senegal awali ilishinda uwanjani, lakini baadaye matokeo yakabatilishwa kwa mujibu wa kanuni za mashindano kufuatia wachezaji wake kutoka uwanjani kupinga maamuzi ya waamuzi, hatua iliyotafsiriwa kama kugomea mchezo.
Tukio hilo limeibua hasira na mijadala mikubwa, huku Rais wa Shirikisho la Soka Cameroon, Samuel Eto'o, akidaiwa kuwasilisha malalamiko rasmi kwa Rais wa CAF, Patrice Motsepe, akielezea wasiwasi juu ya mwenendo mzima wa maamuzi ndani ya shirikisho hilo.
Akizungumzia suala hilo, Motsepe alikiri kuwepo kwa changamoto za muda mrefu kuhusu uadilifu na imani kwa waamuzi, akisisitiza CAF inaendelea kuchukua hatua kuimarisha mifumo ya haki, uhuru wa vyombo vya kimahakama na kuondoa dhana ya upendeleo.
Wakati huo huo, sauti za wakosoaji zimeendelea kuongezeka duniani. Miongoni mwao ni Wayne Rooney na Ahmed Hossam Mido waliopinga vikali uamuzi huo, wakidai unadhoofisha uaminifu wa soka la Afrika. Msanii Akon naye alionyesha kusikitishwa, huku John Mikel Obi akidai kuwepo kwa viashiria vya rushwa.
Hata hivyo, si wote waliopinga, kwani George Weah aliunga mkono uamuzi huo akisisitiza kuwa kanuni lazima ziheshimiwe bila kujali matokeo ya uwanjani.
Kwa sasa, Senegal imepeleka rufaa katika mahakama ya usuluhishi ya soka (Court of Arbitration for Sport) kupinga uamuzi huo, huku hatma ya ubingwa wa AFCON 2025 ikiendelea kusubiri uamuzi wa mwisho, katika sakata linalozidi kufungua mjadala mpana kuhusu uongozi, uwazi na ushawishi ndani ya soka la Afrika.
Orodha ya vyeo vya Faouz
Rais wa FRMF (Morocco) tangu 2014.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa CAF.
Rais wa Kamati ya Fedha ya CAF
Mjumbe wa Baraza la FIFA.
Waziri wa Bajeti nchini Morocco.
Mwenyekiti wa kamati iliyoshinda uenyeji wa Kombe la Dunia 2030.