Mgogoro wa AFCON 2025, magwiji wa soka waishambulia CAF
Muktasari:
- Gwiji wa Misri, Ahmed Hossam 'Mido', alikosoa vikali uamuzi huo na kuuita kuwa doa kubwa katika historia ya mchezo huo barani Afrika.
UAMUZI wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuinyang’anya Senegal ubingwa wa AFCON 2025 na kuikabidhi Morocco, umeibua mjadala mkubwa, huku magwiji wa soka duniani wakitoa maoni kinzani kuhusu sakata hilo.
Gwiji wa Misri, Ahmed Hossam 'Mido', alikosoa vikali uamuzi huo na kuuita kuwa doa kubwa katika historia ya mchezo huo barani Afrika.
“Hii ni kashfa kubwa zaidi katika historia ya soka. Watu hawa wote lazima waondoke leo, si kesho!” Amesema Mido.
Mido amesisitiza kuwa, Senegal walistahili ushindi wao walioupata uwanjani na kudai kuwa uamuzi wa mezani unaichafua taswira ya soka la Afrika kimataifa.
Kwa upande wake, nyota wa zamani wa England na Manchester United, Wayne Rooney, naye aliungana na wakosoaji akisema: “Ni wazimu. Kama ningekuwa mchezaji wa Morocco nisingekubali. Senegal walishinda kihalali kabisa.”
Rooney ameeleza kushangazwa na hatua ya kubadilisha matokeo licha ya mechi kumalizika uwanjani.
Msanii maarufu duniani, Akon, naye hakuficha hisia zake aliposema: “Nitawaelezea nini wanangu? Kwamba Senegal walikuwa mabingwa halafu ushindi wao unachukuliwa? CAF wanakosea sana.”
Akon aliongeza kuwa, uamuzi huo unaua morali ya mashindano na kuharibu heshima ya soka la Afrika.
Aliyekuwa nahodha wa Nigeria, John Mikel Obi, alitoa kauli kali zaidi akidai kuwepo kwa ufisadi.
“Hii ni rushwa ya wazi. Hakuna sheria inayoruhusu bingwa anyang’anywe kombe baada ya kushinda uwanjani,” amesema Obi.
Hata hivyo, si wote waliokosoa. Rais mstaafu wa Liberia na mshindi wa Ballon d’Or, George Weah, aliunga mkono uamuzi huo akisisitiza umuhimu wa kufuata sheria.
“Sheria ipo wazi sana. Ukiondoka uwanjani na kurudi tena, tayari umepoteza mechi. Morocco wametumia sheria iliyopo kudai haki yao na wameipata,” amesema.
CAF ilieleza kuwa uamuzi huo ulitokana na kifungu cha 84 cha kanuni za mashindano, kinachotafsiri kitendo cha timu kugomea mchezo kama kupoteza kwa ‘forfeit’, kufuatia tukio la wachezaji wa Senegal kutoka nje ya uwanja kwa dakika kadhaa kupinga penalti.
Kwa sasa, Senegal imewasilisha rufaa katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kupinga uamuzi huo, huku dunia ya soka ikisubiri uamuzi wa mwisho.