Ureno bila Ronaldo yachezea kipigo
Muktasari:
- Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, ameifungia Ureno mabao 146 katika mechi 234 tangu alipoanza kuitumikia timu hiyo mwaka 2003. Rekodi hizo zinamfanya kuwa mchezaji mwenye mechi na mabao mengi zaidi katika historia ya soka la kimataifa.
LISBON, URENO: DENMARK imeipa Ureno kipigo kizito cha mabao 4-1 katika mchezo wake wa kwanza tangu nahodha na mshambuliaji nyota, Cristiano Ronaldo atangaze kustaafu soka la kimataifa, huku aliyekuwa mshambuliaji wa Manchester United, Rasmus Hojlund akiibuka shujaa kwa kufunga mabao mawili.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, ameifungia Ureno mabao 146 katika mechi 234 tangu alipoanza kuitumikia timu hiyo mwaka 2003. Rekodi hizo zinamfanya kuwa mchezaji mwenye mechi na mabao mengi zaidi katika historia ya soka la kimataifa.
Nyota huyo pia ameshinda tuzo ya Ballon d’Or mara tano, inayotolewa kwa mchezaji bora wa dunia.
Hata hivyo, wiki iliyopita alitangaza kupitia video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa anastaafu kuichezea timu ya taifa, licha ya kocha Jorge Jesus baadaye kusema angejumuishwa kwenye kikosi cha mechi za Ligi ya Mataifa ya Ulaya dhidi ya Denmark na Wales.
Septemba mwaka huu, Ronaldo aliondoka kambini Ureno baada ya kufahamishwa kuwa hataanza kikosi cha kwanza katika mchezo wa awali dhidi ya Denmark, kitendo kilichomfanya kutozwa faini ya pauni 215 na kufungiwa kwa siku 30.
Mchezo wa Jumamosi uliofanyika Braga, Ureno, ulitawaliwa na heshima kwa Ronaldo kutoka kwa mashabiki na wachezaji wa timu hiyo.
Wachezaji wa timu zote mbili pamoja na watoto walioambatana nao wakati wa kuingia uwanjani walivaa jezi zenye jina la Ronaldo na namba saba mgongoni.
Mashabiki nao walitengeneza maandishi ya jina la Ronaldo katika sehemu ya juu ya jukwaa moja na neno ‘GOAT’ (mchezaji bora wa muda wote) katika sehemu ya chini.
Pia kulikuwa na bango lililokuwa na ujumbe wa kumshukuru nahodha huyo, huku ujumbe kama huo ukionyeshwa kwenye ubao wa matangazo dakika ya saba ya mchezo.
Hata hivyo, sherehe hizo hazikudumu kwa muda mrefu baada ya Denmark kuutawala mchezo na kupata ushindi mnono.
Kiungo wa zamani wa Southampton na Tottenham, Pierre-Emile Hojbjerg, alianza kuiandikia Denmark bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti dakika za mwisho za kipindi cha kwanza, baada ya Ruben Dias kuunawa mpira.
Hojlund, ambaye kwa sasa anakipiga Napoli ya Italia, ameongeza mabao mawili ndani ya dakika nane za kipindi cha pili, kabla ya beki wa Fulham, Joachim Andersen, kufunga bao la nne kwa kichwa dakika ya 75 na kuifanya Denmark kuongoza kwa mabao 4-0.
Ureno ilipata bao la kufutia machozi dakika ya tatu ya muda wa nyongeza kupitia kiungo Bernardo Silva, aliyemalizia mpira karibu na lango baada ya shuti la Joao Neves kuokolewa.
Kabla ya kipigo hicho, Ureno ilikuwa imeshinda mechi zake nne za mwanzo katika Ligi ya Mataifa ya Ulaya na tayari ilikuwa imejihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali.
Sasa inahitaji kuepuka kichapo dhidi ya Wales katika mchezo utakaochezwa Cardiff, kesho Jumanne, Novemba 17, ili kumaliza kileleni mwa kundi lake.
Kwa upande mwingine, Denmark itakuwa mwenyeji wa Norway siku hiyo ikiwa na faida ya pointi tatu katika nafasi ya pili.