Mourinho aweka rekodi LaLiga, ampiku Guardiola
Muktasari:
- Kocha huyo raia wa Ureno sasa anajivunia kuwa na asilimia kubwa zaidi ya ushindi kuliko makocha wote waliowahi kufundisha mechi zaidi ya 100 katika historia ya mashindano hayo, akiwa na asilimia 77.
MADRID, HISPANIA: NI takwimu tu, namba moja rahisi, lakini kutokana na mazingira aliyokutana nayo Jose Mourinho wakati wa kipindi chake cha kwanza cha ukocha katika Ligi Kuu Hispania (LaLiga), ina uzito mkubwa.
Kocha huyo raia wa Ureno sasa anajivunia kuwa na asilimia kubwa zaidi ya ushindi kuliko makocha wote waliowahi kufundisha mechi zaidi ya 100 katika historia ya mashindano hayo, akiwa na asilimia 77.
Takwimu hizo zinamuweka mbele ya baadhi ya makocha wenye majina makubwa, akiwamo Carlo Ancelotti aliyekuwa kocha wa Real Madrid mwenye asilimia 71, Xavi Hernandez (Barcelona 69), Zinedine Zidane (Real Madrid 67) na Luis Enrique (Barcelona 66). Hata hivyo, kubwa zaidi ni kwamba amempita Pep Guardiola aliyeanzia kufundisha Barcelona.
Kocha huyo Mhispaniola alishinda mechi 116 kati ya 152 alizofundisha, sawa na asilimia 76.3, huku Mourinho akiwa na ushindi 97 katika mechi 126.
"Takwimu hizi zinaniambia kwamba tunapaswa kushinda mechi inayofuata," alisema Mourinho, akipunguza uzito wa mafanikio hayo, huku akitambua kuwa hali inaweza kubadilika tena kwa haraka.
"Kwa sababu... katika maisha, hata namba nzuri, zile zenye maana fulani... watu huzisahau. Hatuishi kwa kutegemea takwimu za zamani, tunaishi katika wakati uliopo. Sikuwa na habari kuhusu hilo. Ni wazi kwamba jambo hili ni chanzo cha fahari kwangu, kwa sababu Ligi Kuu Hispania imekuwa na makocha wengi wa viwango vya juu katika historia yake. Na kuwa miongoni mwao kwa takwimu hizo ni jambo la kujivunia."
Zaidi ya umuhimu wake kwa ujumla, takwimu hizo zina maana ya pekee kwa Mourinho kutokana na ukweli kwamba wakati wa kipindi chake cha kwanza akiwa Real Madrid alilazimika kukabiliana na moja ya timu bora zaidi za Barcelona katika historia, iliyokuwa ikifundishwa na Guardiola.
Mapambano yao ya kimkakati ndani ya uwanja yakawa ya kihistoria, kama yalivyokuwa makabiliano yao mbele ya waandishi wa habari. Guardiola aliwahi kujibu kauli za Mourinho mbele ya vipaza sauti kwa kusema: "Mourinho ndiye bosi wa kweli, ndiye anayejua mambo mengi zaidi kuliko mtu yeyote duniani. Na sitaki kushindana naye hata kwa dakika moja."
Sasa kocha huyo raia wa Ureno ana hoja nzito ya kujivunia, kwani takwimu zinaonyesha kuwa mbinu zake za ufundishaji wakati huo na sasa zimekuwa zikizaa matunda.
FLICK ANAITISHIA NAFASI YA MOURINHO
Ukirejea katika hali ya sasa, wakati Mourinho alipokuwa akipambana na kikosi bora cha Barcelona cha Guardiola katika kipindi chake cha kwanza Real Madrid, sasa anakabiliana na timu inayofundishwa na Hansi Flick ambaye ameshinda mataji mawili ya mwisho ya LaLiga.
Kocha huyo Mjerumani anaelekea kuwazidi makocha wenzake wote katika LaLiga akiwa na kiwango cha kuvutia cha asilimia 79.3 ya ushindi baada ya kushinda mechi 69 kati ya 87 alizofundisha.
Hata hivyo, bado hawezi kuingizwa katika orodha hiyo kwa sababu hajafikisha kigezo cha kufundisha angalau mechi 100.
Wakati huohuo, Mourinho anaendelea kupanda katika vitabu vya historia ya Real Madrid. Akiwa amefundisha mechi 194 katika mashindano yote akiwa na klabu hiyo anashika nafasi ya sita katika orodha ya makocha waliowahi kuifundisha kwa mechi nyingi zaidi.
Kwa sasa, amebakiza mechi nne pekee ili kumpita kocha mwingine maarufu, Leo Beenhakker, ambaye aliifundisha Real Madrid katika mechi 197. Mbele yake katika orodha hiyo wapo Vicente del Bosque (246), Zidane (263), Ancelotti (353) na Miguel Munoz, ambaye anaonekana kuwa na rekodi isiyofikika kirahisi ya mechi 605.
ASILIMIA KUBWA USHINDI LALIGA ANGALAU MECHI 100
Jose Mourinho (Real Madrid 77.0%)
Pep Guardiola (Barcelona 76.3%)
Carlo Ancelotti (Real Madrid 71.1%)
Xavi Hernández (Barcelona 69.6%)
Zinedine Zidane (Real Madrid 67.8%)
Luis Enrique (Barcelona 66.4%)