UEFA, CONCACAF wamkomalia Infantino
Muktasari:
- Katika barua yao kwa Infantino, Rais wa UEFA, Aleksander Čeferin, na mwenzake wa Concacaf, Victor Montagliani, wamependekeza kila chama cha soka cha taifa kipatiwe Pauni 7.5 milioni (takribani Sh bilioni 24) mara moja kutoka kwenye fedha za FIFA.
LONDON, ENGLAND: VITA vya maneno kati ya UEFA na FIFA vimechukua sura mpya baada ya viongozi wa UEFA na Concacaf kumtaka Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kutoa fedha kutoka kwenye akiba ya shirikisho hilo na kugawa kwa vyama vyote 211 vya soka duniani.
Katika barua yao kwa Infantino, Rais wa UEFA, Aleksander Čeferin, na mwenzake wa Concacaf, Victor Montagliani, wamependekeza kila chama cha soka cha taifa kipatiwe Pauni 7.5 milioni (takribani Sh bilioni 24) mara moja kutoka kwenye fedha za FIFA.
Hatua hiyo imekuja wakati UEFA ikiendelea kushinikiza mabadiliko ndani ya FIFA, huku kukiwa na mvutano kuhusu mpango wa FIFA Forward Enterprises, ambao ulihusisha wazo la kuuza sehemu ya maslahi katika mashindano ya FIFA kwa wawekezaji wa nje.
Čeferin na Montagliani, ambao waliwatumia pia viongozi wa mashirikisho mengine manne nakala ya barua hiyo, wamedai FIFA ina akiba ya rekodi inayofikia Pauni 4.5 bilioni, hivyo ina uwezo wa kuongeza fedha kwa ajili ya maendeleo ya soka bila kulazimika kuuza maslahi katika mashindano yake.
Kwa mujibu wa pendekezo hilo, FIFA ingetumia takribani Pauni 1.5 bilioni kutoka kwenye akiba yake ili kuongeza uwekezaji katika maendeleo ya soka duniani.
Katika barua yao, viongozi hao wamesema FIFA tayari ina uwezo wa kutoa fedha zaidi kwa vyama wanachama kutokana na hali yake ya kifedha.
Wamesema: “FIFA tayari ina uwezo wa kutoa zaidi kwa vyama vyake wanachama kupitia mizania yake yenyewe, bila kuuza maslahi katika mashindano yake na bila kuomba chochote kutoka kwa vyama hivyo kwa kubadilishana.”
WATAKA UKAGUZI WA HESABU
UEFA na Concacaf pia zimetaka kufanyika kwa uchunguzi huru wa hesabu za FIFA, huku zikisisitiza kuwa wachunguzi wanapaswa kupewa nafasi ya kufikia takwimu na makadirio yote ya msingi.
Viongozi hao wameeleza kuwa FIFA ina mabilioni ya fedha yaliyokusanywa kama akiba, wakisisitiza kuwa fedha hizo zinapaswa kutumika kwa manufaa ya soka na vyama vyake 211.
“FIFA kwa sasa ina mabilioni ya dola katika akiba iliyokusanywa. Rasilimali hizi ni za soka na zipo kwa ajili ya kulitumikia mchezo huu na vyama vyake 211,” wamesema.
Wakaongeza kuwa suala la tahadhari katika matumizi ya fedha lisitumike kuzuia uchunguzi wa uwezekano wa kutoa sehemu ya akiba hiyo, hasa iwapo kiasi kilichopo kinazidi mahitaji ambayo FIFA inatarajia kuwa nayo kwa siku zijazo.
Barua hiyo ni sehemu ya mvutano unaoendelea kati ya baadhi ya viongozi wa soka barani Ulaya na uongozi wa FIFA kuhusu namna fedha za shirikisho hilo zinavyopaswa kutumika na mipango ya baadaye ya biashara na maendeleo ya soka duniani.
Čeferin na Montagliani wamekuwa miongoni mwa viongozi wanaosisitiza FIFA itumie uwezo wake mkubwa wa kifedha kuwekeza zaidi moja kwa moja katika maendeleo ya soka kupitia vyama vyake wanachama.
WAKATI HUOHUO
Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe, amemualika Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kwenye mkutano wa siku mbili wa kimkakati wa soka la Afrika, hatua inayokuja wakati Infantino akijiandaa kugombea tena urais wa FIFA.
Mkutano huo utafanyika Cape Verde Oktoba 7 na 8 na utawakutanisha viongozi wa vyama 54 vya soka vya Afrika, pamoja na viongozi wa CAF. Infantino amethibitisha kuhudhuria mkutano huo.
Mwaliko huo unakuja katika kipindi ambacho uongozi wa Infantino ndani ya FIFA unakabiliwa na mjadala mkali baada ya mpango wa FIFA wa kuuza sehemu ya umiliki katika mashindano yake kwa wawekezaji binafsi kukumbana na upinzani kutoka mashirikisho kadhaa ya soka duniani.
Infantino amethibitisha nia yake ya kugombea muhula mwingine katika uchaguzi wa urais wa FIFA unaotarajiwa kufanyika Machi 2027. Kwa upande mwingine, hadi sasa hakuna mpinzani aliyethibitishwa rasmi katika uchaguzi huo, ingawa baadhi ya viongozi wa soka Ulaya wamekuwa wakieleza hitaji la kupata mgombea wa kupambana naye.
Afrika ina vyama 54 wanachama wa FIFA, hivyo kura za bara hilo zinaweza kuwa sehemu muhimu katika uchaguzi wa rais wa FIFA, ambao unahusisha vyama 211 wanachama wa Shirikisho hilo la Dunia.