Msako pointi tatu Championship unaendelea
Muktasari:
- Katika mechi hizo za leo, Gunners FC iliyotoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Songea United ugenini, itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, kuikaribisha Bandari Tanzania, yenye kumbukumbu pia ya kutoka sare ya 1-1, mbele ya KenGold FC.
RAUNDI ya pili ya Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, imeendelea jana kwa mechi mbili kupigwa na nyingine tatu zikipigwa leo, kisha kuhitimishwa kesho Jumapili, huku ushindani ukianza kuonekana mapema kwa vigogo vinavyoshiriki.
Katika mechi hizo za leo, Gunners FC iliyotoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Songea United ugenini, itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini, Dodoma, kuikaribisha Bandari Tanzania, yenye kumbukumbu pia ya kutoka sare ya 1-1, mbele ya KenGold FC.
Gunners FC inashiriki Ligi ya Championship kwa msimu wa pili sasa tangu ilipoanza kushiriki kwa mara ya kwanza msimu wa 2025-2026 na kumaliza ikiwa nafasi ya nane na pointi 38, baada ya kushinda mechi 11, ikitoka sare tano na kupoteza 14. Kwa upande wa Bandari inayoshiriki Championship kwa mara ya kwanza msimu wa 2026-2027, ilimaliza kinara wa kundi A na pointi 32, katika Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 2025-2026, ikishinda mechi 10, sare mbili na kupoteza mbili kati ya 14.
Kwenye Uwanja wa Manungu Complex, mjini, Morogoro, wenyeji Mtibwa Sugar iliyotoka sare ya bao 1-1, dhidi ya maafande wa Transit Camp mechi ya kwanza, itacheza dhidi ya Mbuni FC kutoka jijini, Arusha, iliyotoka kuchapwa na KMC FC mabao 5-1. Moja ya rekodi bora iliyowekwa na Mtibwa Sugar msimu wa 2024-2025, ikishiriki Ligi ya Championship ni ya kucheza mechi 15, kati ya 30, kwenye Uwanja wa Manungu Complex Morogoro na kushinda zote, huku pia ikifunga mabao 38 na kuruhusu sita.
Mtibwa Sugar inakabiliwa na deni kubwa la kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2025-2026, ilipomaliza nafasi ya 15 na pointi 27, kufuatia kushinda mechi sita tu, ikitoka sare tisa na kupoteza 15, ikifunga mabao 25 na kuruhusu 48. Mechi ya mwisho leo, itapigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam, ambapo maafande wa Transit Camp iliyotoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Mtibwa Sugar itaikaribisha TMA FC, iliyochapwa bao 1-0 na Kigamboni United zamani B19 FC. Uhondo wa Ligi ya Championship utaendelea tena kesho Jumapili kwa mechi tatu kupigwa, ambapo Bigman FC iliyoanza msimu huu kwa kuchapwa mabao 2-1 dhidi ya IAA SC ya Arusha itacheza na KMC FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
KMC FC iliyoshuka daraja msimu wa 2025-2026 kwa kushinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza 25 kati ya 30 iliyocheza na pointi tisa, inakutana na Bigman FC, huku ikiwa na kumbukumbu nzuri, baada ya kuichapa Mbuni FC ya Arusha mabao 5-1.
Songea United iliyotoka sare ya bao 1-1 mechi ya kwanza dhidi ya Gunners FC ya jijini Dodoma itakuwa kwenye Uwanja wa Majimaji uliopo mjini Songea mkoani Ruvuma kupambana na Rhino Rangers ya Tabora iliyoichapa Tanzania Prisons bao 1-0.
Rhino ambao ni wageni wapya walimaliza vinara wa kundi B na pointi 35 msimu wa 2025-2026 katika Ligi Daraja la Kwanza baada ya kushinda mechi 11, sare mbili na kupoteza moja kati ya 14 iliyocheza huku ikifunga mabao 31 na kuruhusu tisa. Timu ya Rhino ni mabingwa wa Ligi Daraja la Kwanza kwa msimu wa 2025-2026 baada ya kuifunga Bandari Tanzania iliyopanda kwa kuongoza kundi A na pointi 32 kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya kufungana mabao 2-2 mechi iliyopigwa Juni 17, 2026. Mechi ya mwisho kwa kesho ya kuhitimisha raundi ya pili, itapigwa kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya jijini, Mbeya, ambapo KenGold FC iliyotoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Bandari Tanzania, itakikaribisha kikosi cha IAA SC kutoka Arusha. IAA SC inayoshiriki Championship kwa mara ya kwanza msimu huu wa 2026-2027, baada ya kupanda daraja msimu wa 2025-2026, ilianza vizuri michuano hiyo nyumbani kwa ushindi wa mabao 2-1, dhidi ya kikosi cha Bigman FC kutoka jijini, Tanga.
Timu ya IAA SC ya Arusha ilifuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027, kupitia mechi ya ‘Play-Off’, baada ya kuitoa African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda nyumbani 2-1, kisha ugenini ikatoka sare ya bao 1-1. Kwa upande wa KenGold inasaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu msimu wa 2027-2028, baada ya kikosi hicho kushuka daraja msimu wa 2024-2025, kilipoburuza mkiani mwa nafasi ya 16 na pointi 16, kufuatia kushinda mechi tatu, sare saba na kupoteza 20.
Kwa msimu wa 2023-2024, KenGold ilitwaa ubingwa wa Championship, ikiibuka kinara na pointi 70, ikiungana na Pamba Jiji ya Mwanza iliyomaliza nafasi ya pili na pointi 67, iliyorejea Ligi Kuu baada ya miaka 21, tangu iliposhuka mwaka 2001.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa Songea United, Juma Masoud amesema usajili uliofanyika na maandalizi kwa timu zote msimu huu inaashiria Ligi ya Championship itakuwa ni ngumu, jambo linalothibitishwa na ushindani ulioanza mwanzoni.
“Mechi za kwanza zimeonyesha jinsi Ligi itakavyokuwa ngumu, ushindani ni mkubwa kwa sababu kila timu imefanya usajili mzuri kwa malengo ya kuhakikisha inacheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2027-2028, hivyo, haitokuwa rahisi,” amesema Masoud.