Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aliyemuua Tupac ahukumiwa miaka 40 jela

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa jarida la People, Davis mwenye umri wa miaka 63 amehukumiwa Jumanne, Oktoba 13, 2026, na Mahakama ya Clark County, Las Vegas, Nevada, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji kwa kutumia silaha hatari Agosti 31, mwaka huu.

Marekani. Duane “Keffe D” Davis, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya rapa maarufu wa Marekani, Tupac Shakur, amehukumiwa kifungo cha miaka 40 hadi maisha jela katika kesi hiyo.

Kwa mujibu wa jarida la People, Davis mwenye umri wa miaka 63 amehukumiwa Jumanne, Oktoba 13, 2026, na Mahakama ya Clark County, Las Vegas, Nevada, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji kwa kutumia silaha hatari Agosti 31, mwaka huu.

Katika kutoa hukumu hiyo, Jaji Carli Kierny alisema Davis hawezi kuchukua maisha ya mtu na kuendelea na maisha yake kana kwamba hakuna kilichotokea. Jaji huyo alisisitiza kuwa mauaji ya Tupac yaliinyima familia yake mtu muhimu na dunia kipaji cha muziki ambacho kingeweza kuendelea kutoa mchango mkubwa.

Davis alikamatwa Septemba 2023, baada ya uchunguzi wa mauaji hayo kudumu kwa miongo kadhaa bila mtu kufikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo.

Chanzo cha mauaji ya Tupac

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, mauaji ya Tupac yalihusishwa na tukio la Septemba 7, 1996, ambapo msanii huyo na watu waliokuwa pamoja naye walimshambulia Orlando “Baby Lane” Anderson, mpwa wa Davis, katika hoteli ya MGM Grand mjini Las Vegas.

Tukio hilo lilitokea baada ya pambano la ndondi kati ya Mike Tyson na Bruce Seldon. Upande wa mashtaka ulidai kuwa Davis alihusika kupanga shambulio la kulipiza kisasi dhidi ya Tupac kufuatia tukio hilo.

Baadaye usiku huo, Tupac alipigwa risasi akiwa ndani ya gari lililokuwa likiendeshwa na Marion “Suge” Knight, mwanzilishi mwenza wa lebo ya muziki ya Death Row Records. Knight pia alijeruhiwa katika shambulio hilo.

Tupac alifariki Septemba 13, 1996, akiwa na umri wa miaka 25, siku sita baada ya kushambuliwa kwa risasi. Kifo chake kilikuwa miongoni mwa matukio yaliyoacha maswali mengi katika tasnia ya muziki wa hip-hop kwa miaka mingi.

Familia ya Tupac yaeleza maumivu

Wakati wa kusikilizwa kwa hukumu, dada wa Tupac, Sekyiwa Shakur, pamoja na kaka yake, Maurice Shakur, walieleza mahakamani maumivu ambayo familia imeendelea kuyapata tangu kifo cha msanii huyo.

Kwa mujibu wa People, Sekyiwa aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa Davis, akieleza namna kifo cha kaka yake kilivyoathiri familia yao. Alimwelezea Tupac kama mtu aliyekuwa na nafasi muhimu katika maisha yake na aliyekuwa na mipango mingi ya kuleta mabadiliko katika jamii.

Kuhusu uchunguzi

Uchunguzi wa mauaji ya Tupac uliendelea kwa miaka mingi bila mtu kufikishwa mahakamani kuhusiana na kifo chake, hadi Davis alipokamatwa Septemba 2023.

Uchunguzi huo ulipata mwelekeo mpya kupitia maelezo ambayo Davis alitoa kwa mamlaka mwaka 2008, pamoja na maelezo yaliyomo katika kitabu chake cha kumbukumbu, Compton Street Legend, kilichochapishwa mwaka 2019.

Hata hivyo, upande wa utetezi ulipinga baadhi ya maelezo yaliyotolewa dhidi ya Davis, huku wakili wake, Michael Sanft, akieleza kuwa anapanga kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Kwa hukumu ya miaka 40 hadi maisha jela, kesi hiyo imefikia hatua muhimu katika jitihada za kupata haki kwa Tupac, ambaye kifo chake kimeendelea kujadiliwa na mashabiki wa muziki duniani kwa takribani miongo mitatu.