Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fury, Joshua kupigana usiku wa manane?

Muktasari:

  • Hiyo inafuatia ombi lililowasilishwa katika Baraza la Jiji la Cardiff, likieleza kuwa mabondia hao wanatarajiwa kuingia ulingoni baada ya saa sita usiku, huku uwanja ukipendekezwa kuendelea kuwa wazi hadi saa 9:30 alfajiri.

CARDIFF, WALES: PAMBANO linalosubiriwa kwa hamu kati ya mabondia wa uzito wa juu, Tyson Fury na Anthony Joshua, linaweza kuanza saa 7 usiku wa manane kwenye Uwanja wa Principality, Cardiff, Wales, Desemba mwaka huu.

Hiyo inafuatia ombi lililowasilishwa katika Baraza la Jiji la Cardiff, likieleza kuwa mabondia hao wanatarajiwa kuingia ulingoni baada ya saa sita usiku, huku uwanja ukipendekezwa kuendelea kuwa wazi hadi saa 9:30 alfajiri.

Kwa mujibu wa BBC, kampuni ya Millennium Stadium Plc imeomba kubadilisha leseni ya matumizi ya uwanja ili kuruhusu pambano hilo kufanyika usiku wa manane, kwa tukio maalumu la mara moja.

Fury amedokeza kuwa atajaribu kumshawishi Rais wa Marekani, Donald Trump, kuungana naye wakati akiingia ulingoni.

“Nitampa mwaliko rafiki yangu wa zamani, Trump, kisha tutaona kama atapatikana. Huenda isiwe rahisi kutokana na majukumu yake ya sasa akiwa Rais wa Marekani,” alisema Fury.

Ombi hilo pia linataka muziki wa moja kwa moja uendelee hadi saa 9:00 alfajiri, huku burudani hiyo ikitarajiwa kufanyika kabla ya mabondia kuingia ulingoni.

Inapendekezwa pia paa la uwanja lifungwe wakati wote wa tukio hilo, huku ulinzi ukiimarishwa.

Mamlaka nyingine pamoja na wananchi wana nafasi ya kuwasilisha pingamizi hadi Novemba 3, kabla ya baraza kufanya kikao cha kuyajadili. Inaelezwa kuwa kibali hicho kinaweza kutolewa iwapo hakutakuwa na pingamizi.

Awali, kulikuwa na sintofahamu kuhusu pambano hilo kufanyika nchini Uingereza au New York, Marekani.

Hata hivyo, promota Eddie Hearn alifanya juhudi kubwa kuhakikisha pambano hilo linafanyika Cardiff, huku kampuni ya utiririshaji wa maudhui ya Netflix ikitaka lipangwe muda utakaowezesha watazamaji wa Marekani kulifuatilia katika saa zinazofaa.

Kwa sasa, Fury anaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda pambano hilo. Bondia huyo maarufu kwa jina la Gypsy King amedai kuwa amefanikiwa kupunguza uzito kutoka takribani mawe 28, sawa na kilo 178, hadi kufikia umbo alilonalo sasa.

Uzito na umbo la Fury vimekuwa vikibadilika kwa kiasi kikubwa kwa miaka kadhaa. Januari mwaka huu, alijitaja kuwa mtu aliyekuwa mnene, akitumia pombe kupita kiasi na kula vyakula visivyo na afya, aliporejea kutoka kustaafu kwa mara ya tano.

Hata hivyo, safari hii anaonekana kuwa makini zaidi katika maandalizi yake.

Kila bondia anatarajiwa kulipwa pauni75 milioni, sawa na dola za Marekani milioni kadhaa, kwa pambano hilo.

Ripoti ya Daily Mail Sport ya Septemba ilieleza kuwa mabondia hao wangeweza kutozwa kodi ya takribani asilimia 30 ya malipo yao iwapo pambano lingefanyika Marekani, ikilinganishwa na asilimia 20 nchini Uingereza.

Hali hiyo ilimkera zaidi Joshua, ambaye angekabiliwa na ongezeko la kodi la pauni7.5 milioni. Bondia huyo, bingwa wa dunia mara mbili, alisisitiza mkataba wake uheshimiwe kwa kuwa ulielekeza pambano hilo lifanyike nchini Uingereza.

Hearn mwanzoni alipendekeza Uwanja wa Wembley kuwa mwenyeji, lakini uwepo wa paa katika Uwanja wa Principality na utayari wa Serikali ya Wales kuruhusu shughuli kuendelea hadi usiku wa manane vilichangia kuipa Cardiff nafasi ya kuandaa pambano hilo.