Tyson afunguka pambano la Mayweather
Muktasari:
- Pambano hilo la kushtua kati ya magwiji hao wa ndondi lilitangazwa Septemba mwaka jana na ilionekana linaweza kufanyika mapema mwaka huu, lakini kwa sasa inaonekana kupoa na hakuna dalili za kutokea hivi karibuni.
NEW YORK, MAREKANI: BONDIA mkongwe, Mike 'Iron' Tyson ametoa taarifa muhimu kuhusu pambano linalosubiriwa kwa hamu kati yake na Floyd Mayweather.
Pambano hilo la kushtua kati ya magwiji hao wa ndondi lilitangazwa Septemba mwaka jana na ilionekana linaweza kufanyika mapema mwaka huu, lakini kwa sasa inaonekana kupoa na hakuna dalili za kutokea hivi karibuni.
Shaka kuhusu pambano hilo kuota mbawa iliibuka mapema mwezi huu baada ya taarifa zilizoeleza kuwa Mayweather yuko mbioni kupambana na bingwa maarufu wa kickboxing kutoka Ugiriki, Mike Zambidis.
Hata hivyo, bingwa ambaye hakuwahi kupoteza pambano, Mayweather amesisitiza kuwa lazima atapambana tu na Tyson, hivyo watu wanatakiwa wawe wavumilivu.
Tyson, ambaye mara ya mwisho alipanda ulingoni Novemba 2024 katika pambano dhidi ya Jake Paul, aliliambia jarida la TMZ: "Ndiyo, bado linafanyika. Unadhani litaota mbawa? Hapana."
Tyson amesema alikuwa ameamua kuachana na ndondi hadi pale Mayweather alipoanza kumtafuta na kumtaka apambane naye.
"Nilikuwa najishughulisha na mambo yangu, yeye ndiye aliyenitafuta."
Tyson alipambana na Paul miezi mitano tu baada ya kulazwa hospitalini kutokana na ugonjwa wa vidonda vya tumbo.
Hata hivyo, nyota huyo mwenye umri wa miaka 59 anasema kwa sasa anajisikia mwenye afya njema sana.
"Ninajisikia vizuri sana. Hili ni pambano ambalo hata dunia haikudhani lingeweza kutokea. Hata hivyo, ngumi zimeingia katika zama mpya ambapo kuna mambo mengi yasiyotabirika!"