Tuchel ampa onyo Maguire, akimfagilia Stones
Muktasari:
- Maguire aling’ara na kuwa mchezaji bora wa mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Uruguay, iliyochezwa kwenye dimba la Wembley Stadium, hali iliyomfanya aonekane kuwa amejiweka katika nafasi nzuri ya kuitwa kwenye kikosi cha Kombe la Dunia.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa timu ya taifa ya England, Thomas Tuchel, amemuonya beki wa Manchester United, Harry Maguire kuwa ana nafasi ndogo ya kuchaguliwa kikosi cha mwisho kitakachowakilisha katika Kombe la Dunia 2026 na huenda akahitaji kuomba wachezaji wenzake wapate majeraha ili apate nafasi hiyo.
Wakati huohuo, Tuchel pia ameonyesha kumpa nafasi kubwa beki wa Man City, John Stones, akidai kuwa anaweza kumchukua kwenda naye Kombe la Dunia hata asipopata nafasi kubwa ya kucheza katika klabu yake.
Maguire aling’ara na kuwa mchezaji bora wa mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Uruguay, iliyochezwa kwenye dimba la Wembley Stadium, hali iliyomfanya aonekane kuwa amejiweka katika nafasi nzuri ya kuitwa kwenye kikosi cha Kombe la Dunia.
Hata hivyo, Tuchel amesema ana mabeki wanne anaowapa kipaumbele zaidi kuliko Maguire kutokana na vigezo vyake.
Tuchel amesema: “Sijabadilisha mawazo yangu kuhusu Maguire, lakini naona kuna wachezaji wengine ninaopenda waanze. Naona wako mbele yake kwa sifa tofauti. Namuona Ezri Konsa ni zaidi yake, namuona Marc Guehi anafaa zaidi, hata Trevoh Chalobah pia bado anampita kwa kuangalia kasi na aina ya uchezaji. Pia yupo John Stones, lakini alikuwa majeruhi, hivyo nafasi yake ndiyo ikachukuliwa na Maguire.”
Hata hivyo, Tuchel alimsifu Maguire kwa kiwango bora dhidi ya Uruguay: “Nilipata kile nilichotarajia katika eneo la kati la safu ya ulinzi. Anacheza vizuri akiwa na mpira, mtulivu, ana nguvu na anaweza akafanya jambo katika mipira ya adhabu.”
Alipoulizwa kama angeingia kwenye kikosi cha Kombe la Dunia sasa, Tuchel amesema: “Kama ningetaja kikosi leo, kutokana na majeraha yaliyopo, angeweza kuwemo. Lakini kama wachezaji wote watakuwa fiti, inaweza kuwa tofauti.”