Tuchel ajitetea kwa ushindi wa kihistoria
Muktasari:
- Ingawa hakufanikisha ahadi ya kuiletea England nyota ya pili ya ubingwa wa dunia, ameiongoza kutwaa medali ya shaba kwa mara ya kwanza. Kwa Tuchel, ushindi huu ni uthibitisho kwamba anaamini njia yake ndiyo sahihi.
MIAMI, MAREKANI: KOCHA Thomas Tuchel anaweza kuhisi amewajibu wakosoaji wake. Ushindi wa mabao 6-4 dhidi ya Ufaransa katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu Kombe la Dunia umempa England nafasi yake bora zaidi kwenye mashindano hayo tangu ilipotwaa ubingwa mwaka 1966.
Ingawa hakufanikisha ahadi ya kuiletea England nyota ya pili ya ubingwa wa dunia, ameiongoza kutwaa medali ya shaba kwa mara ya kwanza. Kwa Tuchel, ushindi huu ni uthibitisho kwamba anaamini njia yake ndiyo sahihi.
Hata hivyo, kwa upande wa wakosoaji wake, matokeo hayo yamezua maswali mapya badala ya kuyajibu.
Kwao, ushindi huu unaonyesha wazi kile ambacho England ingeweza kufanya kama ingecheza kwa ujasiri dhidi ya Argentina kwenye nusu fainali badala ya kujilinda baada ya kupata bao la kuongoza.
Wanaamini timu ilipaswa kushambulia badala ya kurudi nyuma, jambo walilodai liliigharimu nafasi ya kucheza fainali.
Pia, walitumia kipindi cha pili, ambacho England ililegeza mchezo na kuruhusu Ufaransa kufunga mabao manne, kama ushahidi wa mbinu za kujihami kupita kiasi za Tuchel.
Mashabiki walimzomea
Siku moja kabla ya mchezo, Tuchel amesema mashabiki waliokuwa wanamuunga mkono na waliokuwa wanampinga walikuwa katika uwiano wa asilimia 50 kwa 50.
Lakini hali ilionekana tofauti kabisa Uwanja wa Miami, ambapo alizomewa jina lake lilipoonyeshwa kwenye skrini kubwa kabla ya mechi kuanza.
Hata hivyo, wachezaji wake walijibu kwa kiwango bora kabisa uwanjani.
Msaidizi wake, Anthony Barry, alishindwa kuficha hisia zake wakati wa mapumziko huku England ikiongoza mabao 4-0.
“Nimeshindwa kupata maneno ya kuelezea jinsi ninavyojivunia wachezaji hawa. Wanacheza wakiwa na maumivu makubwa baada ya kilichotokea kwenye nusu fainali. Nimewaona hotelini siku zote hizi wakiwa wamevunjika moyo, lakini bado wameonyesha kupambana dhidi ya wapinzani wa kiwango cha dunia,” amesema Barry.
Swali ambalo halijaisha
Licha ya ushindi huo mkubwa, swali linaendelea kuwa lilelile.
Ikiwa England ilikuwa na uwezo wa kucheza kwa ujasiri, kushambulia kwa kasi na kuonyesha ubunifu dhidi ya Ufaransa, kwa nini haikuonyesha sura hiyo ilipoongoza 1-0 dhidi ya Argentina kwenye nusu fainali? Bukayo Saka alikuwa mfano halisi wa mjadala huo. Dhidi ya Argentina hakupata hata dakika moja za kucheza, lakini mbele ya Ufaransa aliwaka moto, akimsumbua Theo Hernandez kwa dakika zote alizokuwepo uwanjani hadi beki huyo akatolewa mapumziko. Mwishoni mwa mchezo, Saka alikuwa ameondoka na hat-trick.
Tuchel afanya mabadiliko makubwa
Baada ya kukosolewa vikali, Tuchel alifanya mabadiliko saba kwenye kikosi chake, huku nyota kama Harry Kane na Jude Bellingham wakianza benchi.
Wengi waliona uamuzi huo kama njia ya kupunguza presha dhidi yake, lakini wachezaji aliowapa nafasi walimjibu kwa soka la kushambulia, ubunifu na kujiamini.
England ilianza mchezo kwa kasi ya ajabu. Dakika ya tatu tayari ilikuwa mbele baada ya Declan Rice kuiba mpira katikati ya uwanja na kuanzisha shambulizi lililozaa bao la mapema.
Mwisho wa siku, ushindi huo umeleta furaha kwa England, lakini haujafuta mjadala kuhusu uamuzi wa Tuchel kwenye mechi muhimu zaidi ya mashindano hayo dhidi ya Argentina. Medali ya shaba imepatikana, lakini wengi bado wanaamini England ilikuwa na uwezo wa kufika mbali zaidi.