Townsend afungukia ajali yake
Muktasari:
- Townsend, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Prachuap ya Thailand, alikumbwa na tukio hilo la kutisha wakati wa mapumziko ya mchezo dhidi ya Pattani.
LONDON, ENGLAND; NYOTA wa zamani wa Ligi Kuu England na timu ya taifa, Andros Townsend, amefichua kuwa alidhani kifundo cha mguu kingevunjika baada ya kukanyagwa na mashine ya kusawazisha uwanja wakati wa mapumziko ya mchezo nchini Thailand.
Townsend, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Prachuap ya Thailand, alikumbwa na tukio hilo la kutisha wakati wa mapumziko ya mchezo dhidi ya Pattani.
Video ya tukio hilo ilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, ikimuonyesha mchezaji huyo akikanyagwa na mashine hiyo iliyokuwa ikiendeshwa kusawazisha uwanja.
Licha ya tukio hilo la kutisha, Townsend alinusurika bila kupata majeraha makubwa. Alipata mikwaruzo na maumivu madogo tu, kisha baadaye akaweza kuingia uwanjani kama mchezaji wa akiba.
Akizungumza katika kipindi cha Piers Morgan Uncensored, Townsend alisema hakuliona tukio hilo likija.
“Sikuliona likija. Ilikuwa ni wakati wa mapumziko na tulikuwa tunaenda kufanya mazoezi ya kujiandaa kwa kipindi cha pili. Niliona mashine mbili za kusawazisha uwanja, moja kila upande wa uwanja.
“Nakumbuka nilijiuliza, ‘Sijawahi kuona kitu kama hiki katika maisha yangu ya soka, wanafanya nini?’ Lakini tuliitwa kwenda kufanya mazoezi ya kujiandaa, hivyo sikufikiria sana kuhusu hilo.
“Kitu kilichofuata nilichokiona ni mimi kuwa chini kabisa ya mashine hiyo. Kwa bahati nzuri, sikupata madhara makubwa.”
Townsend alisema bado anashindwa kuamini tukio hilo kila anapoliona kwenye video.
“Kila ninapoliona, huwa najisikia vibaya na kushangaa. Nilipowatumia watoto wangu video hiyo, walidhani ni picha iliyotengenezwa kwa AI.
“Ilinibidi kuwaeleza kwa takribani dakika 10 kwamba tukio hilo lilikuwa la kweli.”
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 alisema video hiyo inatisha kuitazama kwa sababu inamfanya afikirie madhara ambayo angeweza kuyapata.
“Ni jambo baya kulitazama tena na kuona kile ambacho kingeweza kutokea. Kwa bahati nzuri, nilianguka chini kwa wakati sahihi, hivyo hakuna kitu kilichovunjika wakati mashine iliponipita.
“Na leo nipo hapa nikicheka na kusimulia tukio hilo.”
Townsend yuko katika msimu wake wa kwanza akiwa na Prachuap, baada ya kushuka daraja msimu uliopita akiwa na klabu ya Thailand, Kanchanaburi Power.
Baada ya tukio hilo, wachezaji mbalimbali walimpa pole na kumtakia afya njema. Kiungo wa zamani wa Crystal Palace, Nya Kirby, mwenye miaka 26, alimtumia ujumbe mfupi akisema: “Pona haraka, kaka.”
Townsend sasa atalazimika kusubiri hadi Jumapili, Oktoba 11, kwa mchezo unaofuata wa Prachuap dhidi ya Chiangrai United.