Tottenham yashikilia msimamo kwa Rodrygo
Muktasari:
- Inaelezwa Spurs ipo tayari kulipa zaidi ya Pauni 70 milioni kama ada ya uhamisho ya fundi huyu ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
TOTTENHAM bado inatamani sana kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazil, Rodrygo, mwenye umri wa miaka 24, dirisha lijalo la majira ya baridi.
Inaelezwa Spurs ipo tayari kulipa zaidi ya Pauni 70 milioni kama ada ya uhamisho ya fundi huyu ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.
Rodrygo amekuwa akihusishwa kuondoka Madrid tangu kuanza kwa msimu huu kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza cha timu hiyo na Kocha Xabi Alonso anaonekana hayupo katika mipango yake.
Licha ya mara kadhaa kocha huyo kusisitiza bado anahitaji huduma ya Rodrygo, mara nyingi staa huyo ameonekana kukalishwa benchi na kuingizwa katika dakika za mwisho kwa baadhi ya mechi.
Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza jumla ya mechi 16 za michuano yote na hajafunga bao hata moja zaidi ya asisti nne alizotoa.
Mbali ya Spurs, Rodrygo pia anawindwa na Inter Milan ya Italia lakini kiasi cha pesa kinachohitaji ili kumnunua kinaonekana kikwazo.
Adam Wharton
CRYSTAL Palace ipo katika mazungumzo na kiungo wao wa kimataifa wa England, Adam Wharton, 21, kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya wa kuendelea kutumikia kikosi chao. Mabosi wa Palace wameanza mazungumzo hayo na wawakilishi wa fundi huyu baada ya kuona vigogo wengi wameanza kuinyemelea saini yake kutokana na kiwango alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu. Manchester United na Liverpool zinatajwa kumuwinda dirisha lijalo majira ya kiangazi.
Conor Gallagher
MANCHESTER United inataka kumsajili kiungo wa kati wa Atletico Madrid, Conor Gallagher, 25, dirisha lijalo la majira ya baridi. Mabosi wa Man United wapo tayari kutoa zaidi ya Pauni 50 milioni ili kuhakikisha inamnunua staa huyu. Mbali ya Gallagher, mashetani hao wekundu pia wanahitaji huduma ya kiungo wa Stuttgart ya Ujerumani, Angelo Stiller mwenye umri wa miaka 24. Ynited inataka kuimarisha eneo la kiungo linaloonekana kukosa makali.
Rasmus Hojlund
MANCHESTER United ilikuwa inafikiria kumrudisha mshambuliaji wao, Rasmus Hojlund anayecheza kwa mkopo Napoli, lakini ripoti zinaeleza mpango huo umefeli kwa sababu Rasmus mwenyewe haitaji kurudi na ana furaha kuendelea kusalia Italia. Fundi huyu, 22, alikuwa akionekana kama mbadala sahihi wa Bryan Mbeumo na Amad Diallo ambao hawatokuwa na timu kuanzia Januari mwakani kutokana na michuano ya AFCON.
Scott McTominay
KIUNGO wa Napoli na timu ya taifa ya Scotland, Scott McTominay amempigia chapuo mchezaji aliyekuwa naye wa Manchester United, Kobie Mainoo akimtaka kocha wa Napoli ahakikishe anasajiliwa dirisha lijalo. Hivi karibuni ilidaiwa Napoli inapambana sana ili kuipata saini ya fundi huyu ambaye hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Man United. Scott amekuwa akitamani sana Mainoo atue Napoli, akiamini atasaidia eneo lao la kiungo.
Niclas Fullkrug
STRAIKA wa West Ham, Niclas Fullkrug, , 32, yupo katika rada za AC Milan inayotaka kumsajili dirisha lijalo la majira ya baridi. Niclas amekuwa hapati nafasi kubwa ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha wagonga nyundo hao wa Jiji la London na anataka kuondoka ili kupata changamoto mpya sehemu nyingine. Mabosi wa Milan wanataka kumsajili kwa mkopo wa nusu msimu utakaokuwa na kipengele cha kumnunua mazima.
Endrick
MSHAMBULIAJI wa Real Madrid, Endrick, 19, anaonekana kuwa na asilimia nyingi za kutua Italia dirisha lijalo ambako vigogo wengi wanahitaji saini yake. Awali ilielezwa staa huyu huenda angetua West Ham iliyoonyesha nia ya kumhitaji lakini sasa mambo yamebadilika na ameripotiwa kuchagua kwenda Italia anakowindwa na Juventus, Inter Milan na AC Milan.
Samu Aghehowa
TOTTENHAM inajiandaa kuwasilisha ofa ya takribani Pauni 45 milioni ili kuipiku Chelsea katika vita ya kuiwania saini ya straika wa FC Porto na Hispania, Samu Aghehowa dirisha lijalo la majira ya baridi. Hata hivyo, ripoti zinadai staa huyu, 21, anauzwa kwa takribani Pauni 70 milioni. Samu amekuwa katika kiwango bora tangu ajiunge na Porto akitokea Atletico Madrid.