Real Madrid yatenga mzigo wa maana kwa Rice, Barcola
Muktasari:
- Ikiwa uhamisho huu utatimia, wachezaji hawa wataingja katika orodha ya mastaa waliosajiwa kwa pesa nyingi sana Madrid na La Liga kwa jumla.
REAL Madrid inaripotiwa kuwa tayari kutumia hadi Euro 250 milioni ili kumsajili kiungo wa kati wa Arsenal na timu ya taifa ya England, Declan Rice, 26, pamoja na winga wa Paris Saint-Germain na timu ya taifa ya Ufaransa, Bradley Barcola, 23, dirisha lijalo majira ya kiangazi.
Mastaa hawa kwa sasa ni miongoni mwa viungo bora Ulaya na viwango vyao vimekuwa vikizivutia timu nyingi kutaka kuwasajili.
Ikiwa uhamisho huu utatimia, wachezaji hawa wataingja katika orodha ya mastaa waliosajiwa kwa pesa nyingi sana Madrid na La Liga kwa jumla.
Ripoti za wiki iliyopita zilifichua Arsenal inahitaji kiasi kisichopungua Euro 150 milioni ili kumuuza Rice, huku PSG ikihitaji zaidi ya Euro 100 milioni ili kumwachia Bradley. Inaelezwa mastaa hawa wanatamani pia kutua Madrid lakini hawatolazimisha kuondoka na badala yake watasubiri kuona timu zote mbili zikifia makubaliano.
Illiman Ndiaye
TOTTENHAM imemweka winga wa Everton, Iliman Ndiaye, 25, katika vipaumbele vyao vya usajili dirisha lijalo. Hata hivyo, klabu nyingine kubwa kama Newcastle United , Juventus , AC Milan na Atletico Madrid pia zinamfuatilia kwa karibu mchezaji huyo wa kimataifa wa Senegal na zinaweza kutuma ofa Januari. Ndiaye ambaye alijiunga na Everton mwaka 2024 kutoka Olympique Marseille, amekuwa katika kiwangi bora tangu kuanza kwa msimu huu.
Jonathan David
CHELSEA na Tottenham Hotspur zinaangalia uwezekano wa kufanya usajili wa mshambuliaji wa Juventus Jonathan David, 25, katika dirisha lijalo la Januari. David, ambaye hapo awali aliwika akiwa na Lille ya Ufaransa kabla hajajiunga na Juventus amekuwa katika wakati mgumu tangu kuanza kwa msimu huu, anatamani sana kuondoka ili kubadilisha mazingira na kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Alessandro Bastoni
LIVERPOOL ipo tayari kutoa ofa ya Euro 100 milioni ili kumsajili beki wa kati wa Inter Milan, Alessandro Bastoni, 26. Hata hivyo, Bastoni ambaye ana uwezo wa kucheza kama beki wa kushoto katika mfumo wa watatu au wa wanne mwishoni mwa wiki iliyopita aliweka wazi anajisikia furaha kuendelea kuichezea Inter na hana mpango wa kuondoka. Lakini msimamo huo unaweza kubadilika kutokana na dau hilo nono la Liverpool.
Daniel Munoz
BARCELONA inadaiwa kumfuatilia kwa karibu beki wa kulia wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Colombia, Daniel Munoz, ili kuongeza nguvu kwenye safu yao ya ulinzi. Tovuti ya Mundo Deportivo imefichua Munoz, 29, alikuwa katika mipango ya kocha wa Barca tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini walishindwa kufanikisha mchakato wa kumpata kutokana na masuala ya kifedha.
Etta Eyong
MSHAMBULIAJI wa Levante, Etta Eyong, anafuatiliwa kwa karibu na vigogo wa Hispania, Real Madrid na Barcelona wanaohitaji kumsajili katika dieisha lijalo la majira ya baridi. Eyong amekuwa akionyesha kiwango bora katika Ligi Daraja la Kwanza Hispania tangu kuanza kwa msimu huu. Hakuna timu ambayo imeanza rasmi mazungumzo na wawakilishi wake ili kumsajili lakini yanatarajiwa kuanza hivi karibuni.
Ferlan Mendy
ATLETICO Madrid imepanga kumsajili beki wa Real Madrid, Ferland Mendy, 30. Ripoti zinaeleza Mendy, raia wa Ufaransa amekuwa akitamani kuondoka Madrid tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha klabu hiyo. Mendy alijiunga na Real Madrid mwaka 2019 kutoka Olympique Lyon.
Alexsandro Ribeiro
WEST Ham United imemweka katika orodha ya mastaa inayowahitaji beki wa Lille na Brazil Alexsandro Ribeiro, 26. Mabosi wa West Ham wapo tayari kutumia zaidi ya Pauni 30 milioni kuhakikisha mchezaji huyu anatua Januari mwakani. West Ham inataka kuimarisha safu yao ya ulinzi baada ya kuwa na changamoto za majeraha hali iliyosababisha ianze vibaya sana msimu huu.