Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TOP 5: Waliondoka kwa kuzinguana, wakaenda kukiwasha klabu mpya

Muktasari:

  • Huenda amefurahia hilo baada ya panda shuka nyingi katika kikosi cha Man United hali iliyosababishwa aondolewe kabisa kikosini na kocha Ruben Amorim.

MANCHESTER, ENGLAND: KATIKA dirisha la usajili la majira ya baridi lililomalizika, staa wa Manchester United, Marcush Rashford alikamilisha uhamisho wa kujiunga na Aston Villa kwa mkopo wa nusu msimu.

Huenda amefurahia hilo baada ya panda shuka nyingi katika kikosi cha Man United hali iliyosababishwa aondolewe kabisa kikosini na kocha Ruben Amorim.

Hata hivyo, kuna uwezekano wa furaha yake kuendelea na pia ikashindwa kuendelea kutokana na kile atakachokifanya akiwa na Villa.

Kuna baadhi ya mastaa walioondoka kwa kukosa nafasi au kupishana na uongozi wa timu hiyo kisha wakaenda kuonyesha kiwango bora na wengine wakafeli. Hawa hapa mastaa watano walioondoka timu hiyo miaka ya hivi karibuni na kwenda kuonyesha kiwango bora walikoenda.


CRISTIANO RONALDO

Mwanamume ambaye hahitaji utambulisho, Ronaldo alirejea Manchester United kwa mara ya pili  katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 2021.

Mashetani Wekundu waliwashinda majirani zao, Man City, katika mbio za kumsajili na ilionekana kwamba angeenda kuwa mkombozi katika safu ya ushambuliaji ya Man United.

Hata hivyo, baada ya kuanza vizuri, msimu uliofuatia haukuwa mzuri kwake kwani alikumbwa na matatizo ya kifamilia na akaingia pia katika mgogoro na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Erik ten Hag.

Baada ya hapo alifanya mahojiano na mtangazaji Piers Morgan ambayo yaliibua mambo mengi kiasi cha kusababisha mkataba wake usitishwe.

Ronaldo alitua Al Nassr ya Saudi Arabia ambako amekuwa mchezaji tegemeo wa timu hiyo akifunga mabao 87 katika mechi 95 za michuano yote.


ANTHONY ELANGA

Alijiunga na Manchester United akiwa na umri wa miaka 11 na mashabiki walikuwa na hamu ya kumuona winga huyo mwenye kipaji akicheza katika kikosi cha wakubwa. 

Alicheza mara mbili mwishoni mwa msimu wa 2020-21 wa Ligi Kuu kabla ya kujipatia nafasi zaidi katika msimu uliofuatia.

Hata hivyo, nafasi yake kila siku zilipozidi kwenda na baada ya misimu miwili alihamia Nottingham Forest kwa uhamisho wa Pauni 15 milioni. 

Elanga, ambaye sasa ana umri wa miaka 22 na mechi 19 kwa timu ya taifa ya Sweden, aligeuka kuwa nyota wa timu hiyo inayozidi kushangaza watu kila uchao kutokana na kiwango chake katika ligi.

Alicheza karibu kila mechi ya Ligi Kuu msimu wa 2023-24 na ameshiriki katika kila mechi msimu huu, huku Forest wakiwa wa tatu kwenye msimamo wa ligi.

Elanga alitoa pasi tatu za mabao katika ushindi wa 7-0 dhidi ya Brighton mwishoni mwa wiki. 


ANGEL GOMES

Baada ya kujiunga na akademi ya Man United akiwa na umri wa miaka sita pekee, Mashetani Wekundu walikuwa na matarajio makubwa kwake kwa siku za usoni, lakini mambo hayakuwa hivyo, kwani alicheza mechi tano tu za ligi kabla ya kuuzwa kwenda Lille ya Ufaransa mwaka 2020.

Tangu wakati huo, Gomes amecheza mechi 132 katika kikosi cha Lille na hivi karibuni alikuwa sehemu ya kikosi cha England chini ya aliyekuwa kocha wa muda, Lee Carsley. 


SCOTT McTOMINAY

Watu walishangazwa wakati Erik ten Hag alipomruhusu kiungo huyu kuondoka na kujiunga na Napoli, ambako alikutana na raia mwenzake wa Scotland, Billy Gilmour. 

McTominay, 28, alikuwa katika kiwango bora wakati anauzwa lakini Ten Hag aliona haendani na mipango yake.

Katika mauzo yake Man United ilipata Pauni 25 milioni ambazo kwa sasa zinaonekana kuwa ndogo kutokana na kiwango ambacho fundi huyo amekionyesha tangu atue Napoli.

Mashabiki wa timu hiyo wamempa jina la ‘Maradona  mpya’ kutokana na kiwango chake msimu huu akiwa amecheza mechi 22 za michuano yote na kufunga mabao sita.


CHRIS SMALLING

Huduma ya miaka 10 ya Chris Smalling ndani ya Manchester United ilimalizika 2019 baada ya kuichezea timu hiyo katika mechi 300 na kuisaidia kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu England, FA Cup, Kombe la Ligi na Europa League. Aliondoka baada ya kuonekana haendani na matakwa ya kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye hakuwa anampa nafasi kubwa ya kucheza. Kuondoka kwake ilionekana kama ni anguko kwake kwani muda huo mbali ya kutocheza Old Trafford pia hakuwa anaitwa timu ya taifa ya England.

Hata hivyo, mambo yalikuwa tofauti katika kikosi cha Roma ambako alionyesha kiwango cha juu kwa miamba hiyo ya Italia na baada ya mkataba wake wa mkopo kumalizika alisajiliwa jumla 2020 ambapo aliendelea kung’ara zaidi chini ya Jose Mourinho akiisaidia Roma kushinda Europa Conference League na kufika fainali ya Europa League. 

Hata hivyo, Smalling mwenye umri wa miaka 35, hakupata nafasi nyingine katika kikosi cha England licha ya kiwango chake bora akiwa na Roma kwani aliendelea kung’ara nchini Italia kabla ya kujiunga na Al-Fayha ya Saudi Arabia.