TOM CRUISE: Muvi kali zipo na mkwanja upo

Muktasari:
- Staa huyu aliyezaliwa Julai, 3, 1962 huko Syracuse, New York, Marekani, mbali na kuwa muigizaji, pia ni mtayarishaji wa filamu.
NEW YORK, MAREKANI: TOM Cruise ni mmoja wa waigizaji maarufu na wenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya Hollywood.
Staa huyu aliyezaliwa Julai, 3, 1962 huko Syracuse, New York, Marekani, mbali na kuwa muigizaji, pia ni mtayarishaji wa filamu.
Amewahi kutamba na muvi kibao zilizotikisa soko la filamu kama Top Gun, Mission: Impossible na Jerry Maguire.
Hata hivyo, mbali ya mafanikio yake ya filamu, muigizaji huyu pia akaunti yake sio haba kwani ni mmoja kati ya waigizaji matajiri zaidi duniani, msome hapa.

ANAPIGAJE PESA
Kwa mujibu wa tovuti mbalimbali, hadi kufikia mwaka huu, Cruise ni mmoja kati ya waigizaji 10 wenye utajiri mkubwa zaidi na kwa saa anakadiriwa kuwa na ukwasi unaofikia dola 600 milioni.
Utajiri wake unatokana na filamu alizocheza, mikataba ya kibiashara, na uwekezaji binafsi.
Cruise hulipwa kati ya dola 20 milioni hadi dola 100 milioni kwa kila filamu anayoigiza.
Katika Mission: Impossible – Fallout, alipata zaidi ya dola 70 milioni kutokana na mgawanyo wa mapato ya filamu na kiujumla kupitia muvi za Mission Impossible alizoigiza anakadiriwa kupata kiasi kisichopungua dola 200 milioni.
Staa huyu pia ana kampuni yake ya uzalishaji filamu iitwayo, Cruise/Wagner Productions, ambayo inazalisha filamu mbalimbali za kwake na za watu wengine ikiwa ni sehemu ya kujipatia kipato.
Tofauti na waigizaji wengi, Tom Cruise hapendelei sana kuwa balozi wa kampuni kwani hapendelei sana kuwa sura ya bidhaa tofauti tofauti.
Hata hivyo, baadhi ya kampuni za magari kama BMW na Ducati zimemshirikisha kwa kutangaza bidhaa zao kupitia filamu alizocheza kama Mission Impossible, ingawa haijabainishwa zilimlipa kiasi gani.

MSAADA KWA JAMII
Amekuwa akitoa misaada na msaada wa kisaikolojia kwa wanajeshi waliorejea kutoka vitani, pia ni mmoja wa wadhamini wa mashirika ya elimu yanayohusiana na kanisa la Scientology, kama vile Applied Scholastics.
Amesaidia pia kufadhili taasisi zinazopinga matumizi ya dawa za kuondoa misongo ya mawazo.
Wakati wa matetemeko ya ardhi na majanga, amewahi kuchangia kwa kutoa fedha na hata kutumia helikopta zake kusaidia waathirika.

NDINGA
Magari ya kifahari anayomiliki ni: Bugatti Veyron -Dola 1.7 milioni
Porsche 911 - dola- 120,000
Ford Mustang Saleen S281 - dola 65,000
Chevrolet Corvette C1 ya 1958 - dola 100,000
BMW 7-Series - dola 90,000
Pia anamiliki pikipiki nyingi ambazo kiujumla thamani yake inakadiriwa kufikia dola 50,000.

MIJENGO
Ni miongoni mwa waigizaji ambao wanamiliki nyumba za thamani sana. Ana mjengo huko Telluride, Colorado ambayo aliinunua kwa dola 39.5 milioni.
Pia aliwahi kuwa na nyumba eneo la Beverly Hills, California lakini aliiuza kwa dola 40 milioni mwaka 2016.
Taarifa pia zinaeleza ana nyumba nyingine huko Florida na London, England.

MAISHA BINAFSI
Amewahi kuoa mara tatu, ndoa ya kwanza alimuoa Mimi Rogers kuanzia mwaka 1987 hadi 1990, baada ya hapo akamuoa Nicole Kidman kuanzia mwaka 1990 hadi 2001 walipoachana. Huyu alizaa naye watoto wawili ambao ni Isabella Jane Cruise na Connor Cruise.
Alipoachana na Kidman alikaa kwa muda hadi mwaka 2006 ambapo alimuoa Katie Holmes mwaka 2006 akazaa naye mtoto mmoja na akaachana naye mwaka 2012 na tangu hapo hakuwahi kuoa tena.