Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nani kutwaa kiatu cha ufungaji bora?

UFUNGAJI Pict

Muktasari:

  • Tangu 2018/19 rekodi za wafungaji bora zinaonyesha jinsi ushindani huo ulivyobadilika, kuanzia mabao 60 yaliyofungwa na Fatuma Mustapha wa JKT Queens hadi mabao 20 yaliyompa Jeanine Mukandayisenga wa Yanga Princess nafasi ya kuwa kinara msimu uliopita.

ACHANA na vita ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara inayotarajiwa msimu huu, ushindani mwingine ni mbio za kuwania kiatu cha ufungaji bora.

Tangu 2018/19 rekodi za wafungaji bora zinaonyesha jinsi ushindani huo ulivyobadilika, kuanzia mabao 60 yaliyofungwa na Fatuma Mustapha wa JKT Queens hadi mabao 20 yaliyompa Jeanine Mukandayisenga wa Yanga Princess nafasi ya kuwa kinara msimu uliopita.

Sasa, wakati timu zikianza safari mpya ya kutafuta ubingwa, swali ni nani atakayeibuka na tuzo hiyo, na je, kuna mshambuliaji mwenye uwezo wa kurejesha rekodi ya mabao mengi iliyowekwa na Fatuma?


FATUMA ANA REKODI

Takwimu zinaonyesha kuwa Fatuma ndiye mwenye rekodi kubwa zaidi katika orodha ya wafungaji bora wa misimu hiyo minane. Msimu wa 2018/19 alifunga mabao 60 akiitumikia JKT Queens, kiwango ambacho bado kinatofautiana kwa kiasi kikubwa na idadi iliyofikiwa na wafungaji bora wa misimu ya hivi karibuni.

Msimu uliofuata, 2019/20, Fatuma aliendelea kuwa kinara kwa kufunga mabao 33. Ingawa idadi hiyo ilikuwa pungufu ya mabao 27 ikilinganishwa na msimu uliotangulia, aliendelea kuthibitisha uwezo wake wa kutikisa nyavu kwa mwendelezo.

Hata hivyo, misimu iliyofuata ilikuwa na majina mapya kama Aisha Masaka wa Yanga Princess aliyefunga mabao 35 mwaka 2020/21, kabla ya Asha Djafari wa Simba Queens kutupia kambani mabao 26 ule wa 2021/22.

UFU 01

MABAO YANAVYOPUNGUA

Katika misimu ya karibuni, idadi ya mabao ya wafungaji bora imekuwa chini ikilinganishwa na rekodi za Fatuma na Masaka.

Msimu wa 2022/23, Jentrix Shikangwa wa Simba Queens alifunga mabao 17, kabla ya Aisha Mnunka wa timu hiyo hiyo kufikisha mabao 20 mwaka 2023/24.

Katika msimu wa 2024/25, Stumai Abdallah wa JKT Queens alimaliza na mabao 28, huku Jeanine Mukandayisenga wa Yanga Princess akimaliza msimu wa 2025/26 akiwa na mabao 20.

Kwa hesabu za misimu minne kuanzia 2022/23 hadi 2025/26, wastani wa mabao ya mfungaji bora ni 21.25 kwa msimu. Hii inaonyesha kuwa mabao 20 yanaweza kuwa kigezo cha kuanzia katika kutathmini ushindani wa msimu huu.

UFU 02

SIMBA, JKT AU YANGA?

Takwimu zinaonyesha kuwa JKT Queens, Simba Queens na Yanga Princess zimekuwa na mchango mkubwa katika kutoa wafungaji bora.

JKT imekuwa na Fatuma, aliyefanikiwa kutwaa tuzo hiyo mara mbili mfululizo, pamoja na Stumai Abdallah. Simba imewahi kubeba kupitia kwa Asha Djafari, Jentrix Shikangwa na Aisha Mnunka, huku Yanga ikibebwa na Masaka na Mukandayisenga.

Kwa mfano, Simba Queens ilifunga mabao 52 katika michezo 22 ya ligi msimu uliopita, huku Yanga Princess ikifunga mabao 56. Takwimu hizo zinaonyesha uwezo wa timu hizo kutengeneza na kutumia nafasi za kufunga.


WALIOONGOZA HAWAPO

Changamoto nyingine katika mbio za msimu ni mabadiliko ya usajili. Mukandayisenga aliyekuwa mfungaji bora 2025/26 kwa mabao 20, alitimka Yanga Princess na kujiunga na Wuhan Jiangda ya China Julai 2026.

Shikangwa ambaye alikuwa mshindani wake wa karibu naye ametimkia FC Masar ya Misri. Mkenya huyo alifunga mabao 16 msimu uliopita. Hivyo washindani wote waliokuwa wanaongoza kwenye chati za ufungaji bora wametimka kwenye ligi.

Stumai naye ana historia ya kutisha mabeki baada ya kufunga mabao 28 msimu wa 2024/25. Endapo ataendelea kuitumikia JKT Queens na kupata nafasi ya kutosha, anaweza kuwa sehemu ya mjadala wa kuwania tuzo hiyo.

UFU 03

HAWA WANAWEZA

Mbali na Stumai nyota wengine waliosajiliwa hivi karibuni wanayo nafasi ya kuibuka wafungaji bora.

Senaf Demise aliyesajiliwa na Simba Queens msimu huu anaingia WPL akiwa na historia ya kufunga mabao mengi katika ligi ya Ethiopia na mashindano ya ukanda wa CECAFA. Rekodi ya mabao 21 katika mechi 20 za ligi mwaka 2019 ambayo ni wastani wa kufunga bao moja kwa mechi, huku mabao sita ya CECAFA mwaka 2024 yakionyesha uwezo wake wa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Mwingine anayetarajiwa kufanya vizuri na kuibuka mfungaji bora ni mshambuliaji wa Yanga, Sandrine Mutuyimana ambaye alijiunga na wananchi akitokea Rwanda ambako aliondoka akiwa anaongoza kwa kufunga mabao 10.

Mbali na huyo kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mesay Temsgen ambaye ni raia wa Ethiopia ameonyesha matumaini ya kuwa anaweza kushindania kiatu.

Hata hivyo rekodi ya Fatuma ya mabao 60 bado ni kipimo kikubwa cha historia ya WPL. Lakini kwa hali ilivyo katika misimu ya karibuni, macho yatakuwa kwa mshambuliaji atakayefikia angalau mabao 20 na kuendelea kuongeza idadi hiyo. Swali ni je msimu huu kiatu kitaenda JKT Queens, Simba Queens, Yanga Princess au timu nyingine itazalisha mfungaji atakayewashangaza wengi? Jibu litapatikana uwanjani, ambako kila bao linaweza kubadili mwelekeo wa mbio hizo.