Tatu zapigana vikumbo kwa Manuel Akanji
Muktasari:
- Akanji alijiunga na Man City mwaka 2022 akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya karibu Pauni 15 milioni na ameshinda mataji makubwa ikiwemo Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
BAYER Leverkusen na Galatasaray zinataka kuingia katika vita dhidi ya Crystal Palace kwa ajili ya kumsajili beki wa kati wa Manchester City, Manuel Akanji, 30, katika dirisha hili.
Akanji alijiunga na Man City mwaka 2022 akitokea Borussia Dortmund kwa ada ya karibu Pauni 15 milioni na ameshinda mataji makubwa ikiwemo Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Staa huyu ni miongoni mwa wachezaji ambao Man City inataka kuwauza katika dirisha hili na katika nafasi yake kumekuwa na ushindani mkubwa wa namba kutoka kwa Ruben Dias, Josko Gvardiol na John Stones.
Palace inataka kumnunua beki huyu kwa sababu haina uhakika kama itaendelea kubaki na nahodha wake Marc Guehi ambaye anahusishwa sana na Liverpool.
Kocha wa Palace, Oliver Glasner anaamini kama Guehi akiondoka, Akanji anaweza kuwa mbadala sahihi wa staa huyo.
Mkataba wa Akanji unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, wakati ule wa Guehi na Palace ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu ujao.
Antony
MANCHESTER United wamefikia makubaliano ya awali na Real Betis juu ya kumrejesha winga wao wa kimataifa wa Brazil, Antony, 25, katika timu hiyo. Dili hilo linatarajiwa kuwa la mkopo lakini lenye kipengele cha kumnunua moja kwa moja mwishoni mwa msimu.
Antony alisajiliwa na Man United kwa ada ya Pauni 86 milioni kutoka Ajax mwaka 2022, lakini hajawahi kufikia kiwango kilichotarajiwa katika maisha yake United.
Jakub Kiwior
FC Porto ipo karibu kukamilisha usajili wa beki wa Arsenal na timu ya taifa ya Poland, Jakub Kiwior, 25, katika dirisha hili la majira ya kiangazi. Kiwior alisajiliwa kutoka Spezia kwa ada ya karibu Euro 20 milioni mwaka 2023 lakini amekuwa akipata muda mdogo wa kucheza chini ya Mikel Arteta. Porto inamchukulia kama chaguo la kuongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi baada ya kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wakongwe.
Harvey Elliott
CRYSTAL Palace inajiandaa kuanza mazungumzo na Liverpool kuhusu kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Harvey Elliott, 22, ili kuipata saini yake katika dirisha hili.
Palace inamwona fundi huyu kama mbadala wa Eberechi Eze, 27, ambaye amejiunga na Arsenal.
Elliott, aliyesajiliwa na Liverpool mwaka 2019 kutoka Fulham, ni miongoni mwa wachezaji walioomba kuondoka katika dirisha hili.
Maximillian Beier
BRENTFORD inataka kumsajili mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Max Beier, 22, kwa ajili ya kuboresha safu ya ushambuliaji.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa mwaka 2029, msimu uliopita alicheza mechi 46 za michuano yote na kufunga mabao 10. Staa huyu ni miongoni mwa walioonyesha kiwango bora kwa msimu uliopita lakini msimu huu mambo yanaonekana kuwa magumu.
Garnacho
WINGA wa Manchester United na timu ya taifa ya Argentina, Alejandro Garnacho, 21, amekataa ofa mpya kutoka timu moja ya Saudi Arabia na ameendelea kusisitiza kwamba timu pekee anayohitaji kujiunga nayo ni Chelsea.
Mazungumzo kati ya Man United na Chelsea kuhusu dili la staa huyo bado yanaendelea kwa sasa na kinachokwamisha ni masuala ya ada ya uhamisho.
Adam Wharton
REAL Madrid inataka kumsajili kiungo wa Crystal Palace, Adam Wharton, 21, kama mbadala wa Dani Ceballos, 29, ambaye kuna uwezekano akaondoka katika dirisha hili. Wharton alijiunga na Palace Januari 2024 akitokea Blackburn Rovers kwa ada ya karibu Pauni 18 milioni na tangu wakati huo amekuwa mmoja kati ya mastaa tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Palace.
Soungoutou Magassa
WEST Ham United iko karibu kukamilisha usajili wa kiungo wa Kifaransa, Soungoutou Magassa, 21, kutoka AS Monaco kwa ada ya takribani Pauni 17.3 milioni katika dirisha hili.
Magassa ambaye anaichezea timu ya taifa ya vijana ya Ufaransa anatamani sana kucheza Ligi Kuu England kwa msimu ujao. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2029.