Tatu za England zaendelea kumgombania Rodrygo
Muktasari:
- Staa huyo ambaye ana mkataba Real Madrid hadi Juni 2028, ana kipengele kinachoeleza kwamba anaweza kuuzwa kwa Euro 1 bilioni, ingawa haionekani ikiwa kuna timu inayoweza kulipa kiasi hicho na mara kadhaa imeripotiwa Madrid itakuwa tayari kupokea Pauni 70 milioni.
MANCHESTER City, Arsenal na Liverpool zinavutiwa na winga wa Real Madrid, Rodrygo Goes, 24, lakini hadi sasa hazijawasilisha ofa.
Staa huyo ambaye ana mkataba Real Madrid hadi Juni 2028, ana kipengele kinachoeleza kwamba anaweza kuuzwa kwa Euro 1 bilioni, ingawa haionekani ikiwa kuna timu inayoweza kulipa kiasi hicho na mara kadhaa imeripotiwa Madrid itakuwa tayari kupokea Pauni 70 milioni.
Hata hivyo, hakuna timu yoyote iliyowasilisha ofa ili kumsajili na timu hiyo imeendelea kusisitiza kwamba haina mpango wa kumuuza ingawa tetesi zinasambaa kwamba anahitaji kuondoka ili kupata nafasi zaidi ya kucheza kwani haoni kama yupo kwenye mipango ya kocha Xabi Alonso.
Msimu uliopita chini ya kocha Carlo Ancelotti alicheza mechi 54 za michuano yote akafunga mabao 14 na kutoa asisti 11. Msimu huu La Liga kacheza mechi moja.
Gianluig Donnarumma
KIPA wa PSG, Gianluigi Donnarumma, 26, yupo katika hatua za mwisho kutua Manchester City ambayo imeshafanya naye makubaliano binafsi na sasa inamalizana na PSG juu ya ada ya uhamisho. Staa huyo wa kimataifa wa Italia, msimu uliopita alikuwa sehemu ya wachezaji tegemeo katika kikosi hicho ambapo alikisaidia kushinda Ligue 1 na Ligi ya Mabingwa. Mabosi wa PSG wanamuuza kwa Euro 50 milioni
Savinho
TOTTENHAM Hotspur imewekA nguvu kwa winga wa Manchester City na timu ya taifa ya Brazil, Savinho, 21, baada ya kiwango bora akiwa Girona alikokuwa akicheza kwa mkopo. Kocha wa Spurs, Thomas Frank anamuona kuwa chaguo sahihi baada ya kumkoasa Eberechi Eze, 27, aliyetua Arsenal. Savinho alifunga mabao tisa na asisti 10 La Liga msimu uliopita.
Nico Paz
TOTTENHAM Hotspur imepeleka ofa mpya ya Pauni 43 milioni Como ili kuipata saini ya kiungo wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Argentina, Nico Paz, 20, katika dirisha hili Hata hivyo, mabosi wa Como wanataka kiasi kisichopungua Pauni 60 milioni ili kumuuza nyota huyo. Paz ambaye aliwahi kucheza timu ya vijana ya Real Madrid, mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.
Lucas Paqueta
ASTON Villa na Tottenham Hotspur zinamfuatilia kwa karibu kiungo mshambuliaji wa West Ham United na Brazil, Lucas Paqueta, 27. Paqueta ambaye alinunuliwa kutoka Lyon kwa Pauni 51milioni mwaka 2022 ana mkataba wa kuendelea kuitumikia West Ham hadi 2027. Msimu uliopita alicheza mechi 36 za michuano yote na kufunga mabao matano.
Senne Lammens
KIPA wa Royal Antwerp na timu ya taifa ya Ubelgiji, Senne Lammens, 23, yupo katika hatua nzuri kujiunga na Manchester United katika dirisha hili la usajili kwenye dili ambalo linatarajiwa kuwagharimu Mashetani Wekundu kiasi kisichopungua Pauni 17 milioni. Man United inamuona kipa huyo kama mbadala wa Andre Onana ambaye anahusishwa kuondoka mwisho wa msimu huu. Mkataba wake wa sasa unamalizika 2027.
Alexander Isak
LIVERPOOL inatarajiwa kurudi na ofa mpya Newcastle United kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Sweden, Alexander Isak, 25, katika dirisha hili. Isak amekuwa akilazimisha kuondoka Newcastle katika dirisha hili na hadi sasa bado hajajiunga na kikosi ikiwa ni sehemu ya kulazimisha kuondoka. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika 2028.
Maghnes Akliouche
AS Monaco ipo tayari kumuachia kiungo wake mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Maghnes Akliouche , 23, lakini kwa ofa itakayoanzia Pauni 47.5 milioni katika dirisha hili la usajili wa majira ya kiangasi. Mchezaji huyo ambaye msimu uliopita alifunga mabao 11 na kutoa asisti tisa katika Ligue 1, aliichezea timu ya taifa ya Ufaransa kwa mara ya kwanza mwaka huu. Mkataba wake unaisha mwakani.