Takwimu zinavyomuadhibu Ruben Amorim!
Muktasari:
- Man United ilichapwa mabao 3-0 na mahasimu wao Manchester City katika mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika Jumapili uwanjani Etihad.
MANCHESTER, ENGLAND: TAKWIMU za kocha wa Manchester United, Ruben Amorim zinafichua kwamba ndiye wa hovyo kuwahi kutokea kwenye Ligi Kuu England.
Man United ilichapwa mabao 3-0 na mahasimu wao Manchester City katika mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika Jumapili uwanjani Etihad.
Katika siku ya huzuni kubwa uwanjani Etihad kufuatia kifo cha bondia Ricky Hatton, mabao ya Phil Foden na Erling Haaland aliyefunga mara mbili yalitosha kuisambaratisha Man United katika mchezo huo.
Kipigo hicho kilikuja baada ya kile cha 1-0 kutoka kwa Arsenal, sare ya 1-1 dhidi ya Fulham na ushindi wa mbinde wa 3-2 dhidi ya Burnley kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa. Hiyo ina maana Man United imekusanya pointi nne tu katika mechi nne za kwanza kwenye ligi, sasa inashika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi na ina wastani wa -3 ya tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Jambo hilo limeifanya Man United kuachwa pointi nane na vinara Liverpool.
Hata hivyo, mwanzo wa hovyo wa msimu kwa miamba hiyo ya Old Trafford unaendeleza kiwango kilekile kibovu cha Amorim. Sawa, kwa Man United kuvuna pointi nne katika mechi nne inaweza isionekane ni hatari. Hiyo ni kwa sababu, ingawa huu ni mwanzo wa hovyo zaidi tangu msimu wa 1992-93, wakati timu hiyo ikiwa chini ya Sir Alex Ferguson, lakini ilifanikiwa kubeba ubingwa wa kwanza wa Ligi Kuu England. Huo ni kwa upande wa timu ya Man United, lakini kwa takwimu za Opta kuhusu rekodi za Amorim, 40, hizo zinatia shaka kubwa.
Mreno huyo mechi yake ya kwanza kwenye kikosi cha Man United ilikuwa Novemba 24 mwaka jana alipopata sare ya 1-1 dhidi ya Ipswich. Na tangu wakati huo, kwa timu 17 zilizodumu kwenye ligi kwa muda wote huo ukiacha zile zilizoshuka na kupita, Man United hali ni mbaya - inashika nafasi za chini kwenye msimamo. Miamba hiyo imevuna pointi 31 katika mechi 31, huku ikiwa imeshinda nane.
Pointi hizo ni sawa na ilizovuna Tottenham Hotspur, lakini yenyewe ikiwa na wastani wa hovyo wa tofauti ya mabao -13 kwa -4. West Ham (pointi 34), Wolves (36) na Fulham (41). Kwa upande mwingine, timu zilizocheza mechi 31 kwa kipindi cha Amorim, Licerpool inaongoza ikiwa imevuna pointi 68. Inafuatiwa na Arsenal (64), Chelsea (58), Man City (54), Newcastle (53) na Crystal Palace (52).
Licha ya kiwango hicho cha hovyo na kukosolewa kila upande kutokana na timu yake kucheza hovyo uwanjani, Amorim amegoma kubadilisha mtindo wake wa kiuchezaji wa 3-4-3. Msimu uliopita Man United ilimaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, hivyo jambo hilo linamfanya Amorim kuwa kwenye presha kubwa ya kufikia malengo. Amorim ameshuhudia ushindi kwenye mechi nane za Ligi Kuu England, lakini bado ameendelea kung'ang'ania kutumia fomesheni ambayo imeshindwa kuleta matunda uwanjani.
"Si rekodi inayoweza kukubalika hapa Manchester United," alisema Amorim.
"Nakubaliana na hilo, lakini sitabadilika. Nitakapoamua kubadili falsafa zangu nitabadili, lakini kama sitaki, basi itabidi abadilishwe mtu. Tutazungumzia hilo katika kila mechi tunayopoteza. Nitacheza kwa njia zangu na nitaendelea kucheza kwenye njia hizo hadi hapo nitakapotaka mabadiliko."
Alipozungumzia mashabiki ambao wamepoteza imani juu yake, Amorim alisema kilichotokea kimemhuzunisha kuliko wao, aliposema: "Naelewa. Hilo ni kawaida kutokana na matokeo. Nakubaliana nao, lakini mimi sitazami mambo kwenye mlengo wao. Ninachokiona tunafanya vizuri, lakini matokeo hayaonyeshi hivyo.
"Ujumbe wangu kwa mashabiki ni kwamba nitafanya kila kitu. Siku zote nimekuwa nikifikiria kitu gani bora kwa ajili ya klabu. Siku zote utabaki kuwa huo ujumbe wangu. Kwa muda ambao nitakuwa hapa, nitajitahidi kwa uwezo wangu wote. Nataka sana kushinda mechi, hivyo hii hali inaniumiza kuliko wao."
MSIMAMO WA LIGI TANGU AMORIM ATUE MAN UTD
1. Liverpool - mechi 31, pointi 68
2. Arsenal - mechi 31, pointi 64
3. Chelsea - mechi 31, pointi 58
4. Man City - mechi 31, pointi 54
5. Newcastle - mechi 31, pointi 53
6. Crystal Palace - mechi 31, pointi 52
7. Bournemouth - mechi 31, pointi 50
8. Nottm Forest - mechi 31, pointi 50
9. Aston Villa - mechi 31, pointi 50
10. Brighton - mechi 31, pointi 46
11. Everton - mechi 31, pointi 45
12. Brentford - mechi 31, pointi 44
13. Fulham - mechi 31, pointi 41
14. Wolves - mechi 31, pointi 36
15. West Ham - mechi 31, pointi 34
16. Tottenham - mechi 31, pointi 31
17. Man United - mechi 31, pointi 31