Tajiri Saudi Arabia afichua siri Manchester United kuuzwa
Muktasari:
- Wamiliki wakuu wa Man United, familia ya Glazer, walikataa ombi la Sheikh Jassim Al-Thani wa Qatar mwaka jana aliyetaka kuinunua jumla klabu hiyo na badala yake wakauza hisa za asilimia 27.7 tu kwa bilionea Sir Jim Ratcliffe kwa kiasi cha Pauni 1.25 bilioni.
MANCHESTER, ENGLAND: TAJIRI na kiongozi wa sekta ya michezo na burudani wa Saudi Arabia, Turki Al-Sheikh, ameweka wazi kwamba Manchester United ipo karibu kuuzwa kwa tajiri mpya.
Al-Sheikh, ambaye inaelezwa kuwa yuko kwenye mazungumzo na Man United kuhusu kuialika timu hiyo kucheza mechi ya kirafiki nchini Saudia, alituma ujumbe kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) jana Jumatano usiku akieleza kwamba mazungumzo yamefikia hatua nzuri na muda sio mrefu mmiliki mpya anaweza akatangazwa.
Wamiliki wakuu wa Man United, familia ya Glazer, walikataa ombi la Sheikh Jassim Al-Thani wa Qatar mwaka jana aliyetaka kuinunua jumla klabu hiyo na badala yake wakauza hisa za asilimia 27.7 tu kwa bilionea Sir Jim Ratcliffe kwa kiasi cha Pauni 1.25 bilioni.
Al-Sheikh, ambaye ni mkuu wa Mamlaka ya Burudani ya Umma ambayo pia inasimamia matukio makubwa ya michezo duniani kuletwa Saudi Arabia, aliandika: "Habari bora niliyopokea leo ni kwamba Manchester United ipo katika hatua za mwisho kukamilisha dili la kuuzwa kwa mwekezaji mpya, natumai atakuwa bora kuliko wamiliki wa zamani.”
Hadi sasa haijathibitishwa madai ya Al-Sheikh kama yana ukweli wowote, au kama alikuwa anapiga dongo tu kwa Glazer na Ratcliffe.
Ujumbe huo ulifuatiwa na taarifa kwamba Man United inaweza kupata zaidi ya Pauni 10 milioni ikiwa itakubali kucheza mechi huko Saudi Arabia.
Man United kwa sasa haina hali nzuri ya kiuchumi na inapambana kuhakikisha inapata pesa kwa njia mbalimbali ikiwamo kucheza mechi za kirafiki katikati ya msimu huu.
Kupoteza mechi ya fainali ya Europa League dhidi ya Tottenham msimu uliopita kuliigharimu takriban Pauni 100 milioni, pamoja na Pauni 10 milioni za malipo kutoka kwa adidas.
Man United ilipata Pauni 8 milioni kutokana na ziara yake ya maandalizi ya msimu iliyoifanya kule Kuala Lumpur, Malysia na Hong Kong, China na inataka kwenda Saudi ili kuongeza zaidi mapato.
Katika ratiba ya awali inaeleza huenda Man United ikashiriki mashindano ya timu tatu ambapo itacheza dhidi ya klabu kubwa mbili za Saudi, Al-Nassr na Al-Hilal.
Kwa mujibu wa makadirio, United inaweza kupata karibu Pauni 5 milioni kwa kila mchezo, na inaweza kupata zawadi zaidi ikiwa itashinda mechi hizo.
Vilevile kuna uwezekano ikacheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya kikosi cha wachezaji nyota wa Saudi Arabia (Saudi All-Star), kama ilivyofanya Paris Saint-Germain Januari 2023.