Supercomputer yaivua ubingwa Arsenal
Muktasari:
- Utabiri huo umetolewa na mfumo wa takwimu wa BETSiE, unaotumia supercomputer kuchambua mwenendo wa timu na kukadiria matokeo ya msimu. Kwa mujibu wa utabiri huo, Manchester City itatwaa ubingwa kwa pointi 83, moja zaidi ya Arsenal inayotarajiwa kumaliza na pointi 82.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imetabiriwa kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa mwisho wa Ligi Kuu England msimu huu, licha ya kuendelea kuwania ubingwa kwa ushindani mkali na Manchester City.
Utabiri huo umetolewa na mfumo wa takwimu wa BETSiE, unaotumia supercomputer kuchambua mwenendo wa timu na kukadiria matokeo ya msimu. Kwa mujibu wa utabiri huo, Manchester City itatwaa ubingwa kwa pointi 83, moja zaidi ya Arsenal inayotarajiwa kumaliza na pointi 82.
Hata hivyo, Arsenal iliendelea kuonyesha ushindani baada ya kuifunga Everton mabao 2-0 mwishoni mwa wiki, matokeo yaliyoifanya kufikisha pointi sawa na City. Mabingwa hao watetezi walipoteza pointi kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya kufungwa mabao 2-1 na Aston Villa Jumamosi, lakini wakaendelea kuongoza ligi kwa tofauti ya mabao.
BETSiE inaitabiria Liverpool kumaliza nafasi ya tatu kwa pointi 67, huku Chelsea ikitarajiwa kushika nafasi ya nne kwa pointi 65. Brighton inakamilisha tano bora kwa pointi 61.
Manchester United na Tottenham, ambazo zimekuwa na mwanzo mgumu wa msimu, zinakadiriwa kumaliza nafasi ya sita na saba, kila moja ikiwa na pointi 54. Tofauti ya mabao matatu pekee ndiyo inayotajwa kutenganisha timu hizo katika makadirio hayo.
Aston Villa, Newcastle United na Brentford zinatarajiwa kukamilisha orodha ya timu 10 bora.
Katika upande wa pili wa msimamo, vita ya kunusurika kushuka daraja inatarajiwa kuwa mikali, huku tofauti ya pointi sita pekee ikitenganisha timu inayokadiriwa kumaliza nafasi ya 20 na ile ya 17.
Kwa mujibu wa utabiri huo, Coventry City inatarajiwa kumaliza mkiani kwa pointi 36, ikifuatiwa na Hull City yenye pointi 37 na Sunderland inayokadiriwa kupata pointi 40. Timu hizo tatu zinatajwa kuwa katika hatari ya kushuka daraja na kwenda Championship.
Ipswich Town na Fulham zinakadiriwa kunusurika kwa pointi 42 kila moja. Crystal Palace inatarajiwa kumaliza na pointi 44, huku Nottingham Forest ikikadiriwa kupata pointi 45.
Hata hivyo, hayo ni makadirio ya mfumo wa takwimu na si matokeo ya mwisho. Msimamo halisi utategemea matokeo ya mechi zitakazobaki hadi mwisho wa msimu.