Arsenal, Man United na vichapo vya aibu
Muktasari:
- Arsenal imejikuta katika wakati mgumu baada ya kutolewa kwa penalti 5-3 na Fleetwood Town, timu inayoshiriki Ligi Daraja la Nne England, katika mchezo wa Kombe la Ligi.
LONDON, ENGLAND: SOKA lina mambo yake, na moja ya yanayolifanya kuvutia ni uwezo wa timu ndogo kuwang'oa vigogo katika mashindano ya kombe.
Arsenal imejikuta katika wakati mgumu baada ya kutolewa kwa penalti 5-3 na Fleetwood Town, timu inayoshiriki Ligi Daraja la Nne England, katika mchezo wa Kombe la Ligi.
Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 kabla ya Fleetwood kuibuka mshindi kwa penalti na kufuzu robo fainali, matokeo yaliyotajwa kuwa miongoni mwa mishtuko mikubwa katika historia ya mashindano hayo.
Fleetwood inashika nafasi ya 19 katika daraja la nne la soka England, ilitangulia kupata bao dakika ya 21 kupitia Aaron Loupalo-Bi. Arsenal ilisawazisha kipindi cha pili kupitia Viktor Gyokeres, lakini haikuweza kupata bao la ushindi. Hali ikawa mbaya zaidi kwa wageni baada ya kiungo kijana Max Dowman kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 86. Katika mikwaju ya penalti, kipa Jay Lynch aliokoa mkwaju wa Bruno Guimaraes kabla ya Conor Haughey kufunga penalti ya ushindi.
Tukio hilo limeongeza jina la Fleetwood katika orodha ya timu ndogo zilizowahi kuzishtua klabu kubwa katika Kombe la FA na Kombe la Ligi England. Hizi ni baadhi ya mechi zilizotikisa mashindano hayo.
GRIMSBY 2-2 MAN UNITED (12-11 KWA PENALTI, KOMBE LA LIGI, 2025)
Grimsby Town, inayoshiriki Ligi Daraja la Nne, iliishangaza Manchester United kwa ushindi wa penalti 12-11 baada ya sare ya mabao 2-2.
PLYMOUTH 1-0 LIVERPOOL (KOMBE LA FA, 2025)
Liverpool ilitolewa na Plymouth Argyle, iliyokuwa mkiani mwa Championship, baada ya kocha Arne Slot kufanya mabadiliko 10 katika kikosi chake kufuatia mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Ligi.
Dakika nane baada ya mapumziko, Plymouth ilipata penalti baada ya Harvey Elliott kuunawa mpira. Ryan Hardie alifunga kwa mkwaju wenye nguvu na kuipa timu yake ushindi. Kipa wa Liverpool, Caoimhin Kelleher, aliokoa shuti la Hardie lililotaka kuongeza bao la pili, huku Conor Hazard akifanya kazi kubwa kulinda lango la Plymouth hadi mwisho. Liverpool baadaye ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huo.
CHELSEA 2-4 BRADFORD CITY (KOMBE LA FA, 2015)
Bradford City, iliyokuwa madaraja 49 chini ya Chelsea, ilifanya maajabu Stamford Bridge dhidi ya timu iliyokuwa kileleni mwa Ligi Kuu England. Chelsea ilionekana kuwa na ushindi mkononi baada ya Gary Cahill na Ramires kufunga na kuifanya iwe mbele kwa mabao 2-0.
Hata hivyo, Bradford ilikataa kukubali matokeo. Jon Stead alipunguza tofauti kabla Filipe Morais kusawazisha. Andy Halliday akaipatia Bradford bao la tatu, kisha Mark Yeates akafunga la nne na kuikamilishia Chelsea kipigo cha kushtua chini ya kocha Jose Mourinho.
OLDHAM 3-2 LIVERPOOL (KOMBE LA FA, 2013)
Liverpool iliingia katika mchezo huo ikiwa na nyota kama Luis Suarez, Raheem Sterling na Daniel Sturridge, lakini ikashindwa na Oldham Athletic ya Ligi Daraja la Tatu.
Matt Smith aliifungia Oldham bao la kwanza kwa kichwa akimalizia krosi ya Youssouf M'Changama. Suárez alisawazisha, lakini Smith akatumia kosa la kipa Brad Jones kuifungia Oldham bao la pili. Reece Wabara akaongeza la tatu kwa kichwa kabla Joe Allen kuifungia Liverpool bao la pili. Hata kuingia kwa Steven Gerrard hakukuweza kuizuia Liverpool kutolewa.
BRADFORD CITY 1-1 ARSENAL (3-2 KWA PENALTI, KOMBE LA LIGI, 2012)
Bradford City, iliyokuwa Ligi Daraja la Nne, iliiondoa Arsenal katika robo fainali ya Kombe la Ligi baada ya sare ya bao 1-1 na ushindi wa penalti 3-2.
Garry Thompson aliwapa wenyeji bao la kuongoza kwa shuti la kuunganisha mpira kabla Thomas Vermaelen kusawazisha kwa kichwa akimalizia krosi ya Santi Cazorla dakika mbili kabla ya muda wa kawaida kumalizika. Katika mikwaju ya penalti, Arsenal ilishindwa kutamba na Bradford ikasonga mbele.
MAN UNITED 0-3 YORK CITY (KOMBE LA LIGI, 1995)
Manchester United ya kocha Sir Alex Ferguson ilipata pigo kubwa baada ya kufungwa mabao 3-0 nyumbani na York City. Licha ya United kuwa na wachezaji kama David Beckham, Lee Sharpe na Ryan Giggs, York ilionyesha uimara kupitia Paul Barnes, aliyefunga mabao mawili, moja likiwa la penalti. Tony Barras akaongeza bao la tatu kwa kichwa.
WREXHAM 2-1 ARSENAL (KOMBE LA FA, 1992)
Arsenal iliingia katika mchezo huo ikiwa mabingwa watetezi wa Ligi Daraja la Kwanza England na ikiwa nafasi ya pili kwenye ligi, huku Wrexham ikiwa imemaliza msimu uliopita nafasi ya 24 katika Ligi Daraja la Nne.
Arsenal ilitangulia kupata bao kupitia Alan Smith na ilionekana kuelekea ushindi ikiwa zimesalia dakika 10 tu. Hata hivyo, Mickey Thomas alifunga kwa mpira wa adhabu wa umbali wa takribani mita 23 kabla Steve Watkin kuipatia Wrexham bao la ushindi dakika mbili baadaye.