Prime
SHOO SHOO! Kazini kwa Onana hakuna usalama, hawa wanawindwa
Muktasari:
- Kwenye hilo, kuna orodha ya makipa kibao matata watakuwa wanapatikana tu dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
MANCHESTER, ENGLAND: MAPINDUZI anayotaka kufanya Kocha Ruben Amorim kwenye kikosi cha Manchester United hayaonekani kwenda kukamilika katika ubora unaopaswa hadi hapo atakaposaini kocha mpya.
Kwenye hilo, kuna orodha ya makipa kibao matata watakuwa wanapatikana tu dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Man United ni lazima isajili kipa mpya namba moja. Kwa kusema hivyo, hiyo ina maana Andre Onana anapaswa kuonyeshwa mlango wa kutokea kutokana na makosa mengi anayofanya na kuigharimu timu yake kwenye michuano mbalimbali msimu huu.
Kosa la karibuni kabisa lililofanywa na kipa huyo ni Jumatano iliyopita, wakati alipotoka golini na kupishana na mpira wa kurudishiwa na beki wake wa kushoto, Patrick Dorgu kuwafanya Ipswich Town kufunga bao la dakika ya nne tu ya mchezo kupitia kwa winga, Jaden Philogene.
Kitu kizuri ni mechi hiyo ilimalizika kwa Man United kushinda 3-2 licha ya kucheza pungufu kutokana na kadi nyekundu ya Dorgu. Mwisho wa mechi, Onana alionekana akishangilia kwa nguvu, akiwa amesahau alikaribia kuigharimu timu yake kupata pointi muhimu katika mechi hiyo.
Man United imefanya makosa makubwa kwenye ishu ya kununua makipa kwa miaka kadhaa, Massimo Taibi na Mark Bosnich ni miongoni mwa makipa wao wa hovyo kuwahi kuwasajili, lakini Onana naye anaelekea kwenye kundi hilo la makipa vimeo.
Kocha Amorim hawezi kuifikisha Man United kwenye nchi ya ahadi kwa kuendelea kuwa na Onana golini na imeelezwa Mcamerooni huyo, hajui kujipanga, kunusa hatari, ana pupa, hatishi ndani ya boksi lake na mvivu kuruka.
Man United inahitaji kuwa kwenye mikono salama golini na kwenda hilo, kuna makipa kibao inayoweza kuwasajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi ili kuja kupunguza shida za Onana.
1. Gregor Kobel
Kwa mujibu wa The Independent, Man United inajiandaa kuingia vitani na Chelsea kufukuzia saini ya kipa namba moja wa Borussia Dortmund, Gregor Kobel wakati dirisha litakapofunguliwa. Chelsea inamtaka Kobel akachukue mikoba ya Robert Sanchez kwenye goli lao, lakini skauti wa Man United nao wamekuwa wakimfuatilia kipa huyo kwa muda sasa.
Kobel anasifika kwa kuruka na kudaka mipira juu kwa juu, huku akiwa mzuri kwa mipira ya juu na pasi ndefu zinazofika.
2. Senne Lammens
Desemba mwaka jana, The Telegraph liliripoti Man United ilimwongeza kipa wa Royal Antwerp, Senne Lammens kwenye orodha ya wachezaji ambao itahitaji kuwanasa na imekuwa ikituma skauti wake kwenda kumfuatilia Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 22. Lammens aliibukia kwenye kikosi cha kwnaza cha Antwerp msimu uliopita na tangu wakati huo amekuwa namba moja wa kikosi hicho na ubora wake ni mkubwa. Ubelgiji wanaamini ni mrithi wa Thibaut Courtois.
3. Bart Verbruggen
Kama Man United inataka kusajili kipa kijana, ambaye ameonyesha kitu kwenye Ligi Kuu England, basi hawatakuwa na chaguo jingine bora zaidi ya kumchukua Bart Verbruggen. Daily Star linaripoti kipa huyo mwenye umri wa miaka 22 amekuwa kwenye rada za Man United baada ya kujipambanua na kuwa namba moja kwenye kikosi cha Brighton na timu ya taifa ya Uholanzi. Alikuwa na kiwango bora sana Euro 2024 na ndio msingi wa uimara wa Brighton kwenye safu yao ya ulinzi.
4. Jan Oblak
Jan Oblak kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na miamba hiyo ya Old Trafford kutokana na kiwango chake matata kabisa anachokionyesha huko Atletico Madrid kwa zaidi ya muongo sasa.
Pauni 86 milioni zilizotajwa kwenye mkataba wake kwamba ndicho kiasi cha pesa kitakachotosha kipa huyo kunaswa na timu nyingine, ndicho kitu kinachomfanya Oblak aendelee kubaki Atletico hadi sasa. Lakini, kitu kizuri kinapatikana kwa gharama kubwa na kama Man United inataka kutamba basi imbebe Oblak.
5. James Trafford
Kipa James Trafford ni moja ya wachezaji walioboresha sana viwango vyao kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Baada ya kuwa na msimu mbaya wa kwanza, ambapo aliruhusu mabao 61 katika mechi 28, wakati Burnley iliposhuka daraja chini ya Vincent Kompany, kipa huyo wa kikosi cha England cha U-21 amejipata na kuonyesha kiwango bora sana. Man United itakuwa salama kwa Trafford kuliko hali yao ya sasa chini ya Onana. Yupo kwenye Championship, lakini si kipa wa viwango vya chini.
6. David de Gea
Mashabiki wengi wa Man United wanakubaliana lilifanyika kosa kubwa sana kwa timu yao kuachana na kipa David de Gea. Onana aliyekuja kuchukua mikoba yake huko Old Trafford hana anachofanya na kusababisha mashabiki hao kumkumbuka kipa wao huyo wa zamani, aliyeondoka akiwa huru mwaka 2023. De Gea alikuwa tu mtaani hana timu hadi hapo aliponaswa na Fiorentina na kutamba kwenye Serie A, ambako amekuwa moto kwelikweli. Umri wake miaka 34, hivyo bado ana uwezo mkubwa.
7. Matej Kovar
Matej Kovar hakupewa nafasi Old Trafford. Kipa huyo wa Czech Republic alitokea kwenye akademia ya Man United mwaka 2020, lakini aliachana na timu hiyo baada ya kukaa kwa miaka mitatu bila ya kupewa nafasi kwenye kikosi cha wakubwa. Baada ya kuonyesha kiwango bora kwa mkopo Sparta Prague, alikoshinda ubingwa wa ligi, Bayer Leverkusen ilimwona na kumsajili kwa Pauni 8 milioni mwaka 2023 na ameshinda pia Bundesliga. Kovar alikuwa chaguo la pili la Lukas Hradecky, lakini alicheza mechi 17 na kocha Xabi Alonso alisema kipa huyo ni kiboko.
8. Zion Suzuki
Katika usajili wa dirisha la majira ya baridi, talkSPORT iliripoti Man United ilikuwa inapiga hesabu za kumnyakua kipa Zion Suzuki kwa ada ya Pauni 40 milioni. Kipa huyo amekuwa kwenye kiwango bora sana msimu huu katika kikosi cha Parma licha ya timu kuwa kwenye wakati mgumu. Suzuki aligoma kutua Old Trafford mwaka 2023 wakati akitokea Urawa Red Diamonds, hakutaka kwenda kucheza nyuma ya Onana, lakini kwa sasa anaweza kukubali jambo hilo endapo kama Man United itakwenda na ofa ya kumfanya namba moja.