Shabiki Man United aliyemsusia nywele Amorim aibuka tena
Muktasari:
- Ilett, ambaye ameapa kutokata nywele zake hadi Manchester United ishinde mechi tano mfululizo, alikutana ana kwa ana na aliyekuwa kocha wa klabu hiyo katika mkutano wa soka nchini Ureno na mara hii walipiga stori flani za kishkaji.
PORTO, URENO: SHABIKI maarufu wa Manchester United, Frank Ilett, amekutana na mmoja wa watu waliochangia nywele zake kuwa ndefu kupita kiasi, Ruben Amorim, lakini safari hii ikiwa ni mara ya pili baada ya awali kukutana Italia.
Ilett, ambaye ameapa kutokata nywele zake hadi Manchester United ishinde mechi tano mfululizo, alikutana ana kwa ana na aliyekuwa kocha wa klabu hiyo katika mkutano wa soka nchini Ureno na mara hii walipiga stori flani za kishkaji.
Shabiki huyo, anayefahamika kwa jina la ‘The United Strand’ kwa wafuasi wake milioni 1.5 kwenye Instagram, hajakata nywele zake tangu Oktoba 5, 2024, lakini safari hii anatarajia kuzikata kwani haoni matumaini iwapo chama lake litarudi kwenye ari ya ushindi katika siku za karibuni.
Ilett anaeleza kuwa Amorim, kama ilivyokuwa walipokutana awali, safari hii pia aliomba radhi kwa masaibu anayopitia shabiki huyo baada ya kushindwa kuiongoza United kupata ushindi katika mechi tano mfululizo kwenye mechi 63 alizokuwa akiinoa timu hiyo.
“Ni vizuri kukutana na Ruben Amorim. Aliponiona, alionyesha nywele zangu kwa kidole na kusema, ‘Samahani kwa hilo!’ Bado ninampenda!,” Ilett aliandika kwenye Instagram.
Kwa sasa, Amorim ndiye kocha wa AC Milan, ambayo inashika nafasi ya tano katika Ligi Kuu Italia (Serie A) na haikupoteza katika mechi zake tano za mwanzo. Hata hivyo, Mreno huyo amekosolewa kwa kiasi fulani baada ya maandalizi ya msimu ambayo hayakuwa ya kuridhisha na kufungwa mabao 2-0 na Benfica katika Ligi ya Europa.
Ilett, ambaye kwa sasa anaishi Hispania na ameshiriki katika matangazo ya kampuni ya Paddy Power, anasisitiza kuwa siyo milionea kama baadhi ya watu wanavyodhani kutokana na tukio lake hilo. Badala yake, amekuwa akiwahimiza mashabiki kuchangia Little Princess Trust, shirika la hisani linalotoa wigi bure kwa watoto na vijana waliopoteza nywele kutokana na saratani au hali nyingine za kiafya.
“Kwa hakika, mimi siyo milionea kama baadhi ya watu wanavyodhani. Kumekuwapo na mazungumzo mengi kuhusu kupata mamilioni ya fedha, lakini sivyo ilivyo. Malipo yake siyo makubwa kama baadhi ya watu wanavyofikiria. Hata hivyo, hiyo haikuwa sababu iliyonifanya nianze jambo hili,” aliliambia The Sun na kuongeza:
“Changamoto kubwa imekuwa kutoweza kuona vizuri. Kwa bahati nzuri, ninavaa miwani kwa sababu fremu zake zinasaidia kidogo kuinua nywele zangu za mbele. Kwa sasa, muda mwingi siwezi kuona vizuri. Nywele hizi zinahitaji kuondolewa.”
Msimu uliopita, Ilett alikaribia kupata nafasi ya kukata nywele zake baada ya Manchester United kushinda mechi nne mfululizo, kabla ya West Ham kuilazimisha sare mwezi Februari, ambapo alirusha moja kwa moja kupitia mtandao wa Kick wakati akiitazama mechi hiyo, na huzuni yake ilionekana wazi kwa kila mtu.
“Tutajaribu tena kushinda tano zinazofuata,” mmoja wa marafiki zake alisema baada ya mechi kumalizika, huku Ilett akiwa ameketi kimya akitafakari, akitazama mbele kwa mshangao na kufunika mdomo wake kwa vidole. Kufikia wakati huo, karibu watu 180,000 walikuwa wakitazama matangazo hayo mubashara. “Kadiri nywele zinavyozidi kuwa ndefu, ndivyo zinavyokuwa bora zaidi kwa shirika la hisani,” anasema, akirejerea ahadi yake ya kuzitoa nywele zake kwa Little Princess Trust zitakapokatwa.
“Sitaki jambo hili linihusu mimi tu.”
Hata hivyo, watu ndani ya Manchester United hawajaonyesha hadharani ukarimu mkubwa kwa Ilett, ambapo nahodha wa timu hiyo, Bruno Fernandes, aliwahi kukaririwa akisema: “Ninapaswa kujishughulikia mwenyewe, siangalii mambo ya watu wengine. Siangalii kama wanahitaji kwenda kwa kinyozi au la, hilo siyo jambo muhimu kwangu.”
Lakini, kocha Michael Carrick anasema: “Ndiyo, naweza kusema kuwa ninafahamu kuhusu jambo hilo. Kwa kweli, watoto wangu ndio walionifanya nilifahamu zaidi kuhusu hilo.
“Kwa upande wa kitaalamu, jambo hilo halitaingizwa katika mazungumzo yangu na wachezaji. Ninaelewa kinachoendelea kuhusu suala hilo na linanifanya nitabasamu, lakini mwishowe halitakuwa na athari yoyote.”