Scholes acharuka...Amorim hatoshi Man United
Muktasari:
- Man United kwa sasa inashika nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu England baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Wolves katika mchezo uliopita. Lakini, mwaka mmoja baada ya kuwa kwenye klabu hiyo, Scholes anaamini kocha huyo Mreno sio mtu sahihi wa kuifikisha Man United inakotaka kufika.
MANCHESTER, ENGLAND: GWIJI wa Manchester United, Paul Scholes ameibuka na kumshambulia kocha wa sasa wa timu hiyo, Ruben Amorim, sio mtu sahihi wa kuinoa klabu hiyo.
Man United kwa sasa inashika nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu England baada ya ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Wolves katika mchezo uliopita. Lakini, mwaka mmoja baada ya kuwa kwenye klabu hiyo, Scholes anaamini kocha huyo Mreno sio mtu sahihi wa kuifikisha Man United inakotaka kufika.
Kiungo huyo wa zamani wa Man United anapinga falsafa za kocha Amorim akisema: “Sidhani kama kocha anaielewa hii klabu. Sidhani kama ni mtu sahihi. Man United ni timu isiyoongoza kufanya jambo na yenye kucheza kwa kuburudisha zaidi ya kila kitu. Kuwafanya mashabiki wawe wananyanyuka kwenye viti vyao muda wote. Mawinga wenye uwezo wa kupiga chenga. Kupiga mashuti golini. Ujuzi ni mwingi. Kwa sasa hakuna hicho kitu.
“Kutoka ile klabu tunayoisemea, hii ni nyingine kabisa. Imewachukua Omar Berrada, Jason Wilcox ambao wanafanya kazi nzuri sana, wanafanya vizuri. Hawa sio Man United. Hawana uwezo wa kununua wachezaji wa Manchester United, hivyo hata kuleta kocha wa Manchester United bado.
“Kama utakwenda Sporting Lisbon na kuwatazama wakicheza, wanatumia mabeki wa tatu. Nje ya hapo, hilo hapana. Man United haijawahi kucheza kwa staili hiyo. Hawawezi kufanya hivyo. Hawawezi na hilo limethibitika mwaka hadi mwaka.
“Na naweza kulimzungumzia kabla hata Sir Alex Ferguson, siku zote mfumo wao ulikuwa 4-4-1-1 au 4-4-2. Kuburudisha watu. Alikuwa akichezesha mabeki wanne dhidi ya West Ham. Kama mtakuwa mnaongoza 1-0, kocha muda wote alikuwa akinyanyuka na kusema ‘mbili, tatu, nne.’
“Nakumbuka siku moja, nadhani tulikuwa tukicheza dhidi ya Chelsea. Tulikuwa tunaongoza 1-0 na tulirudi nyuma kidogo kukaba. Kwa kipindi hicho, Chelsea ilikuwa timu nzuri. Kocha alikasirika kwenye mechi hiyo. Kitu kama hicho hakipaswi kutokea hapa. Unapofunga bao moja, utapaswa kufunga la pili. Unapaswa kumkabaa koo mpinzani wako muda wote. Huyu wa sasa, sidhani kama anafanya hivyo.”
Scholes alichezea timu moja tu katika maisha yake ya soka. Kiungo huyo alinyakua mataji 11 ya Ligi Kuu England akiwa na Man United kwa kipindi cha zaidi ya miaka 20 na kuweka rekodi ya kuwa mchezaji anayeshika namba tatu kwa kucheza mechi nyingi katika historia ya klabu hiyo.
Katika hatua nyingine, kocha Amorim alisema bado hana uhakika kama mastaa wake wa Kiafrika, Noussair Mazraoui, Amad na Bryan Mbeumo watakuwa na uwezo wa kucheza mechi dhidi ya Bournemouth kwenye Ligi Kuu England, kesho Jumatatu kabla ya kwenda kuungana na timu zao za taifa zitakazochuana huko kwenye mashindano ya Afcon 2025.
FIFA ilibainisha Desemba 15 ndiyo siku ambayo klabu zitatakiwa kuwaruhusu wachezaji wao kwenda kujiunga na timu zao za taifa kwa ajili ya Afcon, huku Man United siku hiyo itakuwa na mechi dhidi ya Bournemouth jioni.
"Bado tupo kwenye majadiliano na timu za taifa kuhusu mechi hiyo ya Jumatatu, tunajaribu kujiandaa katika mazingira yote," alisema na kuongeza. "Inavuruga kiasi, lakini kitu kizuri ni hakuna anayefahamu atakwenda kucheza. Tunao wachezaji wanaweza kuendana na mazingira yoyote."
MECHI ZIJAZO ZA MAN UNITED
-Desemba 15 vs Bournemouth (nyumbani)
-Desemba 21 vs Aston Villa (ugenini)
-Desemba 26 vs Newcastle (nyumbani)
-Desemba 30 vs Wolves (nyumbani)
-Januari 4 vs Leeds United (ugenini)