Savinho anavyopitia misuli ya Spurs, Man United
Muktasari:
- Mchezaji huyo ambaye ada yake inakadiriwa kufikia Pauni 60 milioni, amekuwa katika rada ya timu mbalimbali Ulaya dirisha hili la usajili kutokana na kutopata nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha Man City, ambako pia amekuwa akipitia maisha magumu sababu ya majeraha.
WINGA wa Brazil na Tottenham Hotspur, Savio Moreira de Oliveira maarufu Savinho, mwenye umri wa miaka 22 anadaiwa kuwa katika hatua za lalasalama za kupitia ofa kutoka Manchester United na Tottenham Hotspur.
Mchezaji huyo ambaye ada yake inakadiriwa kufikia Pauni 60 milioni, amekuwa katika rada ya timu mbalimbali Ulaya dirisha hili la usajili kutokana na kutopata nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha Man City, ambako pia amekuwa akipitia maisha magumu sababu ya majeraha.
Timu za Hispania ikiwamo Real Betis, Atletico Madrid na Athletic Bilbao zimeshawasiliana na wakala wake kuulizia iwapo zinaweza kuinasa saini yake, lakini kila moja haijaendelea na mazungumzo isipokuwa Spurs na Manchester United zilizoamua kupimana ubavu. Savinho mwenyewe anadaiwa keshaweka wazi kwamba anataka kuondoka Spurs. Mkataba anamaliza 2031.
Elliot Anderson
MANCHESTER United bado wana nia ya kumsajili kiungo wa England na Nottingham Forest, Elliot Anderson, 23 ili awe badala sahihi wa viungo wanaoondoka kikosini mwisho wa mwezi huu, Manuel Ugarte na Casemiro.
Anderson aliyepo Marekani na kikosi cha timu ya taifa hilo. Nottingham ilishakataa ofa za awali za Man City na Man United zinazofikia Pauni 80 milioni ambazo ziliwasilishwa mara tu baada ya kumalizika msimu wa mashindano 2025/26.
Marc Cucurella
ATLETICO Madrid na Barcelona zinaonekana kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kumsajili beki wa kushoto wa Hispania na Chelsea, Marc Cucurella, mwenye umri wa miaka 26.
Mchezaji huyo anadaiwa kusaka changamoto mpya baada ya miaka minne katika Uwanja wa Stamford Bridge.
Hata hivyo, lengo kubwa la kutaka kusepa linasukumwa na kutoridhishwa na uongozi hasa sera ya usajili wa mastaa wengi vijana. Cucurella anamaliza mkataba Chelsea Juni 30, 2029.
Lamine Camara
KIUNGO wa Senegal na AS Monaco, Lamine Camara, mwenye umri wa miaka 22 anadaiwa kuingia katika rada za Newcastle United ambayo imeelekeza nguvu zake kwake kwa ajili ya msimu ujao.
Camara anatakiwa Newcastle kwa sababu timu hiyo inahofia kukimbiwa na viungo wake Sandro Tonali au Joe Willock, wote wenye miaka 26, ambao wamekuwa wakishawishiwa na timu mbalimbali kuhamia.
Pio Esposito
MASKAUTI wa Manchester United wanamfuatilia kwa karibu mshambuliaji chipukizi wa Inter Milan, Pio Esposito, mwenye umri wa miaka 20, na majuzi walifanya hivyo pia alipokuwa akiichezea Italia katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Ugiriki.
Esposito, mchezaji anayekuja juu kwa kasi anawindwa pia na AC Milan pamoja na Atalanta kwa ajili ya msimu ujao. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika Juni 30, 2030.
Goncalo Inacio
BEKI wa kati wa kimataifa wa Ureno wa Sporting CP, Goncalo Inacio, mwenye umri wa miaka 24, yupo kwenye orodha ya Liverpool kwenda kuwa mbadala wa beki anayeondoka, Ibrahima Konate ambaye yupo katika hatua za mwisho mwisho kujiunga na Real Madrid.
Inacio ambaye ni panga pangua katika eneo la ulinzi la Sporting CP anadaiwa kuomba kuondoka kikosini ili kwenda kusaka changamoto mpya katika timu nyingine.
Rodrygo Goes
MANCHESTER City wanatafakari kufanya majaribio ya kuwasajili winga wa Brazil na Real Madrid, Rodrygo, mwenye miaka 25, pamoja na winga wa Senegal anayekipiga Everton, Iliman Ndiaye, mwenye miaka 26. Kabla ya dirisha la Januari, mwaka huu, Man City ilihusishwa zaidi na usajili wa Rodrygo ambaye alikuwa hapati nafasi mara kwa mara katika kikosi cha Real Madrid.
Randal Kolo Muani
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Ufaransa wa Paris Saint-Germain, Randal Kolo Muani, mwenye umri wa miaka 27, ambaye alicheza kwa mkopo Tottenham Hotspur msimu uliopita, anataka kujiunga na Juventus, ambako aliwahi kucheza kwa mkopo kwa miezi sita 2025.
Katika matakwa yake, nyota huyo ameutaka uongozi wa PSG usikilize zaidi ofa kutoka Italia badala ya England ambako hana mapenzi nako.