Sarakasi za CAF ubingwa wa AFCON 2025
Muktasari:
- Uamuzi huo umetolewa baada ya Kamati ya Rufani ya CAF kuridhia rufaa iliyowasilishwa na Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF), ikipinga uamuzi wa awali wa Kamati ya Nidhamu ya CAF kuhusu tukio lililotokea katika fainali hiyo.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kupitia Kamati yake ya Rufani, limeibua mabadiliko makubwa katika matokeo ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, baada ya kuamua kuwa Senegal imepoteza mchezo huo kwa njia ya mezani na Morocco kupewa ushindi wa mabao 3-0.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Kamati ya Rufani ya CAF kuridhia rufaa iliyowasilishwa na Shirikisho la Soka la Morocco (FRMF), ikipinga uamuzi wa awali wa Kamati ya Nidhamu ya CAF kuhusu tukio lililotokea katika fainali hiyo.
Katika uamuzi wake, Kamati ya Rufani imeeleza kuwa mwenendo wa timu ya taifa ya Senegal ulikiuka Ibara ya 82 ya kanuni za mashindano ya AFCON, hivyo kwa kuzingatia Ibara ya 84, timu hiyo imetangazwa kupoteza mchezo huo kwa njia ya mezani na matokeo kurekodiwa kuwa Morocco 3-0 Senegal.
Kamati hiyo pia imefuta uamuzi wa awali uliotolewa na Kamati ya Nidhamu ya CAF na kuridhia rasmi malalamiko ya FRMF dhidi ya Shirikisho la Soka la Senegal (FSF).
Mbali na uamuzi huo kuhusu matokeo ya fainali, Kamati ya Rufani pia imetoa uamuzi kuhusu rufaa mbalimbali zilizohusu matukio mengine yaliyojitokeza katika mchezo huo.
Kuhusu mchezaji wa Morocco, Ismael Saibari, Kamati hiyo imethibitisha kuwa alikiuka Ibara ya 82 na 83(1) ya Kanuni za Nidhamu za CAF, lakini imepunguza adhabu yake kuwa kifungo cha mechi mbili za CAF, ambapo mchezo mmoja umesimamishwa. Pia, imefuta faini ya dola 100,000 iliyokuwa imetolewa dhidi yake.
Katika tukio lililohusisha wavulana waliokuwa wakikusanya mipira pembeni mwa uwanja (ball boys), Kamati ya Rufani imethibitisha kuwa FRMF inawajibika kwa mwenendo wao wakati wa mchezo huo, lakini imepunguza faini ya shirikisho hilo hadi dola 50,000.
Hata hivyo, rufaa ya Morocco kuhusu kuingiliwa kwa eneo la mapitio ya video ya mwamuzi (OFR/VAR) imekataliwa na faini ya dola 100,000 iliyotolewa awali imethibitishwa.
Kwa upande wa tukio la matumizi ya mwanga wa leza kuelekezwa uwanjani, Kamati hiyo imeridhia kwa sehemu rufaa ya Morocco na kupunguza faini iliyokuwa imetolewa hadi dola 10,000.
Kamati ya Rufani imehitimisha kuwa maombi mengine yote yaliyowasilishwa katika rufaa hizo hayakukubaliwa.