Afrika inavyoingia kibabe Kombe la Dunia U-17
Muktasari:
- Mataifa 10 yatakayobeba bendera ya Afrika katika Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17, ni Tanzania, Mali, Morocco, Senegal, Ivory Coast, Cameroon, Misri, Algeria, Uganda na Msumbiji.
AFRIKA inaingia kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa vijana U-17 ikiwa na idadi kubwa ya wawakilishi, pia ikiwa na historia tofauti za mafanikio na changamoto zinazoweza kuamua safari yao na kuweka rekodi mpya.
Mataifa 10 yatakayobeba bendera ya Afrika katika Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17, ni Tanzania, Mali, Morocco, Senegal, Ivory Coast, Cameroon, Misri, Algeria, Uganda na Msumbiji.
Mashindano hayo yatakayofanyika Qatar kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13, 2026 ambayo yameingizwa katika mfumo mpya wa timu 48, jambo linaloipa Afrika nafasi kubwa zaidi ya kuonyesha vipaji vyake duniani.
Hata hivyo, kati ya mataifa hayo 10, yapo yenye uzoefu mkubwa katika mashindano hayo, mengine yakiwa na kumbukumbu ya kufika mbali zaidi, huku Tanzania na Msumbiji zikishiriki kwa mara ya kwanza.
MALI INAONGOZA
Ukizungumzia uzoefu wa Afrika katika michuano hiyo, Mali ni moja ya timu linalopaswa kupewa heshima kubwa.
Taifa hilo limecheza Kombe la Dunia U-17 mara sita kabla ya fainali za mwaka huu, likiwa na rekodi ya kufika fainali mwaka 2015 nchini Chile, ambako lilikutana na Nigeria na kupoteza kwa mabao 2-0.
Pamoja na kushindwa kutwaa ubingwa, Mali ilionyesha uwezo mkubwa wa kizazi chake, huku ikitengeneza jina katika soka la vijana.
Mwaka 2023 nchini Indonesia, ilifika hatua ya nusu fainali na kumaliza nafasi ya tatu baada ya kuifunga Argentina mabao 3-0.
Historia hiyo inaifanya Mali kuwa miongoni mwa wawakilishi wa kutazamwa.
Safari hii imepangwa Kundi G pamoja na New Zealand, Ubelgiji na Vietnam, ikiwa na jukumu la kuonyesha kuwa mafanikio yake ya nyuma yanaweza kuwa msingi wa kutengeneza historia nyingine.
IVORY COAST, MOROCCO
Ivory Coast ni miongoni mwa mataifa yenye historia ndefu katika mashindano hayo, ikiwa imeshiriki mara nne kabla ya mwaka huu. Kumbukumbu kubwa kwa taifa hilo ni mwaka 1987 nchini Canada, lilipofanikiwa kufika hatua ya nusu fainali na kumaliza nafasi ya tatu.
Kwa upande wa Morocco, inaingia Qatar ikiwa na uzoefu wa mashindano hayo mara mbili kabla ya mwaka huu, huku mafanikio yake yakiwa kufika robo fainali katika matoleo yaliyopita.
Morocco imekuwa ikionyesha maendeleo katika soka la vijana, hasa kutokana na uwekezaji wake katika programu za kukuza vipaji na miundombinu. Timu hiyo imepangwa Kundi H pamoja na Hispania, China na Fiji.
Senegal ambao ni mabingwa watetezi wa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana AFCON,timu hiyo inaingia katika mashindano hayo ikiwa bingwa wa Afrika, lakini haikuwa na mafanikio makubwa katika toleo lililopita la mashindano ya dunia.
Mwaka 2025 iliongoza kundi lake bila kufungwa bao, lakini safari yake iliishia hatua ya 32 bora baada ya kufungwa na Uganda. Senegal imepangwa Kundi F itakalokutana na Croatia, Cuba na Tajikistan.
CAMEROON, MISRI NA ALGERIA
Cameroon ni miongoni mwa mataifa yenye utamaduni wa soka la vijana barani Afrika, ikiwa imeshiriki mara mbili katika fainali hizo. Hata hivyo, safari yake ya Qatar ni nafasi nyingine ya kuongeza mafanikio yake baada ya uzoefu wa matoleo yaliyopita.
Imepangwa Kundi K pamoja na Mexico, Romania na Venezuela, kundi ambalo linahitaji maandalizi makubwa kutokana na ushindani wa timu hizo.
Misri nayo ina historia ya kushiriki mashindano hayo mara mbili kabla ya mwaka huu. Taifa hilo limekuwa na mchango mkubwa katika soka la Afrika, lakini sasa linahitaji kuonyesha kuwa linaweza kubadili uzoefu wake kuwa matokeo makubwa zaidi duniani.
Misri ipo Kundi A pamoja na wenyeji Qatar, Panama na Ugiriki
Algeria nayo inashiriki mara ya pili katika mashindano hayo, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2009 nchini Nigeria, lakini safari yake haikuwa nzuri kwani ilitolewa hatua ya makundi.
Algeria inarejea kwenye Kombe la Dunia U-17 baada ya miaka 17 , ambako ilipoteza mechi zote tatu za hatua ya makundi ikianza kwa kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Nigeria kabla ya kuruhusu kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Argentina na Ujerumani.
Mwaka huu imepangwa Kundi J pamoja na Marekani, Montenegro na Chile.
UGANDA, MSUMBIJI NA TANZANIA
Uganda hii inakuwa mara yao ya pili kushiriki baada ya mwaka 2025 kufika hatua ya 16 bora. Hilo linaifanya isiwe mgeni kabisa katika mazingira ya mashindano hayo, tofauti na baadhi ya wawakilishi wengine wa Afrika.
Safari hii imepangwa Kundi B pamoja na Korea Kusini, New Caledonia na Ecuador.
Msumbiji ni moja ya mataifa yanayotarajia kuandika historia mpya, baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza kupitia tiketi ya mechi za mchujo za AFCON U-17 Morocco 2026. Ilipata nafasi hiyo kwa kuifunga Ethiopia kwa penalti 5-4 baada ya sare ya bao 1-1.
MFUMO MPYA, NAFASI ZAIDI
Tofauti na mashindano yaliyopita kushirikisha timu 24, mashindano ya mwaka huu yatahusisha mataifa 48 yaliyogawanywa katika makundi 12 ya timu nne.
Timu mbili bora kutoka kila kundi zitafuzu hatua ya 32 bora, zikiungana na timu nane bora zilizomaliza nafasi ya tatu.
Mfumo huo unaongeza nafasi za mataifa ya Afrika kuendelea na safari hata pale yanaposhindwa kumaliza katika nafasi mbili za juu.