Salah apigwa 'stop' kuendesha gari
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo wa Misri alishindwa kuwajulisha polisi aliyekuwa akiendesha gari hilo la umeme aina ya Spectre lililonaswa na kamera ya mkononi mwezi Machi, katika eneo la Wilmslow, Cheshire.
LONDON, England: MSHAMBULIAJI Mohamed Salah amepigwa marufuku ya kuendesha gari kwa miezi sita na kutozwa faini baada ya gari lake la kifahari aina ya Rolls-Royce lenye thamani ya pauni 400,000 (zaidi ya Sh1.3 bilioni) kukutwa likiendesha kwa mwendo kasi.
Mshambuliaji huyo wa Misri alishindwa kuwajulisha polisi aliyekuwa akiendesha gari hilo la umeme aina ya Spectre lililonaswa na kamera ya mkononi mwezi Machi, katika eneo la Wilmslow, Cheshire.
Tukio hilo lilitokea siku mbili baada ya Salah kutangaza kwa kushtukiza kwamba angeondoka Liverpool mwishoni mwa msimu uliopita.
Salah, mwenye umri wa miaka 34, ambaye anatajwa kuwa mfungaji bora wa muda wote wa kigeni katika historia ya Ligi Kuu England, hakujibu wito wa mahakama mara mbili uliotumwa katika jumba lake la kifahari lenye thamani ya pauni milioni nne.
Mwezi uliopita, mahakama ya mahakimu ya Warrington, Cheshire, ilimhukumu bila kuwepo baada ya kukutwa na hatia ya kushindwa kutaja dereva wa gari hilo chini ya utaratibu wa kisheria unaojulikana kama Single Justice Procedure.
Hata hivyo, shtaka la kuvuka kikomo cha mwendo wa maili 30 kwa saa liliondolewa.
Salah, ambaye sasa anakipiga katika klabu ya Trabzonspor ya Uturuki, alihukumiwa kutokuruhusiwa kuendesha gari kwa miezi sita na kulipa faini ya pauni 660. Pia aliamriwa kulipa gharama za mahakama za pauni 120 pamoja na tozo ya pauni 264 inayolipwa kwa ajili ya waathirika.
Hii si mara yake ya kwanza kukumbana na matatizo ya barabarani. Mwaka 2022, Salah alinaswa akiendesha gari lake aina ya Ferrari F8 Tributo kwa mwendo wa maili 63 kwa saa katika eneo lililowekwa kikomo cha maili 50 kwa saa huko Stockport. Alitozwa faini ya pauni 200 na kupewa pointi tatu za adhabu kwenye leseni yake.
Mwaka 2018, pia alirekodiwa akionekana kutumia simu ya mkononi akiwa anaendesha gari karibu na Uwanja wa Anfield. Hata hivyo, hakushtakiwa baada ya polisi kusema kuwa kulikuwa na “ushahidi usiotosheleza”.