Saka apiga hat trick, England ikimaliza mshindi wa tatu Kombe la Dunia 2026
Muktasari:
- Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Miami uliopo Miami katika Jimbo la Florida, Marekani, ilionekana nyepesi zaidi kwa England baada ya kutumia vyema dakika 45 za kipindi cha kwanza ikiongoza kwa mabao 4-0.
MIAMI, MAREKANI: TIMU ya taifa ya England imeibuka mshindi wa tatu wa Kombe la Dunia 2026 baada ya kuhitimisha kampeni kwa ushindi mnono wa mabao 6-4 dhidi ya Ufaransa na kulipa kisasi.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Miami uliopo Miami katika Jimbo la Florida, Marekani, ilionekana nyepesi zaidi kwa England baada ya kutumia vyema dakika 45 za kipindi cha kwanza ikiongoza kwa mabao 4-0.
England ilianza kupata bao la kwanza dakika ya tatu kupitia kwa kiungo Declan Rice, kisha Ezri Konsa akaifungia la pili dakika ya 18, akimalizia pasi ya Rice.
Mechi ikaendelea kuonekana nyepesi kwa England baada ya Bukayo Saka kufunga la tatu akimalizia vyema pasi ya Marcus Rashford, kisha kuongeza la nne na la pili kwake dakika ya 45+1 akitumia pasi ya Eberechi Eze.
Mabao hayo manne yakaipeleka England hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza kifua mbele.
Kipindi cha pili Ufaransa ikarejea kwa nguvu na kupata bao la kwanza dakika ya 48 lililofungwa na mshambuliaji nyota Kylian Mbappe aliyemalizia pasi ya Michael Olise.
Bao hilo likaamsha morali Ufaransa baada ya Bradley Barcola kufunga la pili dakika ya 54 akimalizia pasi ya Mbappe na kurejesha matumaini ya kusawazisha mabao hayo.
Dakika ya 66 Mbappe akafunga bao la tatu kwa Ufaransa akimalizia pasi ya Michael Olise akifikisha mabao 22 katika fainali za Kombe la Dunia na kumpita mshambuliaji nyota wa Argentina, Lionel Messi aliyefunga 21.
Mabao 22 ya Mbappe yanamfanya nyota huyo kufunga mengi zaidi katika historia ya Kombe la Dunia, huku pia akifunga 10, kwenye fainali za 2026 zinazofanyika Marekani, Mexico na Canada, akiongoza mbio za kiatu cha Dhahabu.
Matumaini ya Ufaransa ya kusawazisha yaliingia doa baada ya England kupata penalti ya dakika ya 87 iliyofungwa na Bukayo Saka ikiwa ni bao lake la tatu katika mechi hiyo.
Ousmane Dembele akairudisha tena Ufaransa mchezoni baada ya kufunga bao la nne dakika ya 90+6, huku Jude Bellingham akaifungia England bao la sita dakika ya 90+8 na kuihakikishia kikosi kumaliza mshindi wa tatu.
Ushindi huo kwa England ni wa kisasi kwani mara ya mwisho ilipokutana na Ufaransa ilichapwa mabao 2-1 katika robo fainali ya Kombe la Dunia, ambapo mechi hiyo ilichezwa Desemba 10, 2022 kwenye Uwanja wa Al Bayt, uliopo mji wa Al Khor, Qatar.
Katika mechi hiyo mabao ya Ufaransa yalifungwa na Aurelien Tchouameni dakika ya 17 na Olivier Giroud dakika ya 78, huku bao pekee la England likifungwa na Harry Kane kwa penalti dakika ya 54, kisha akakosa penalti nyingine ya dakika ya 84.
Ufaransa ilitawala mechi zake sita za kwanza za mashindano haya kisha kupoteza kwa kufungwa mabao 2-0, dhidi ya Hispania katika hatua ya nusu fainali iliyopigwa Jumanne ya Julai 14, 2026, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kikosi hicho tangu mwaka 1986.
Timu hiyo maarufu kwa jina la utani la 'Les Bleus', ilipoteza mechi hiyo ya nusu fainali dhidi ya Hispania, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1986, baada ya kushinda nusu fainali nne mfululizo kuanzia mwaka 1998, 2006, 2018 na 2022.
Ufaransa ni miongoni mwa timu bora duniani zenye mafanikio makubwa katika Kombe la Dunia, ambapo imetwaa taji hilo mara mbili, ikianza na mwaka 1998, ilipokuwa mwenyeji wa fainali hizo baada ya kuichapa Brazil kwa mabao 3-0, Julai 12, 1998.
Timu hiyo ikachukua tena taji la Kombe la Dunia la mwaka 2018, lililofanyika Urusi baada ya kuifunga Croatia mabao 4-2, katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Luzhniki, Julai 15, 2018, ukiwa ni ubingwa wa pili baada ya mwaka 1998.
Pia, timu hiyo ilifika fainali mbili na kupoteza zote ikianza na ya mwaka 2006, ilipochapwa kwa penalti 5-3, dhidi ya Italia baada ya sare ya bao 1-1, kisha mwaka 2022, ikachapwa na Argentina kwa penalti 4-2, kufuatia sare ya mabao 3-3.
Katika fainali ya mwaka 2006, iliyofanyika Ujerumani, Julai 9, 2006, moja ya tukio la kukumbukwa ni la aliyekuwa nyota wa Ufaransa, Zinedine Zidane kuonyeshwa kadi nyekundu, baada ya kumpiga kwa kichwa beki wa Italia, Marco Materazzi.
Kwa upande wa England, ilichapwa na mabingwa watetezi wa michuano hii timu ya taifa ya Argentina mabao 2-1, Jumatano ya Julai 15, 2026, yaliyozima ndoto za kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia, tangu mara ya mwisho ilipolichukua mwaka 1966.
England ilitwaa taji hilo mwaka 1966 kwa kuifunga Ujerumani Magharibi mabao 4–2, katika muda wa nyongeza, ambapo mechi hiyo ilipigwa Julai 30, 1966, chini ya aliyekuwa Kocha, Alf Ramsey wakiongozwa na nahodha wa kikosi hicho, Bobby Moore.