Rulani Mokwena ageuza upepo Misri
Muktasari:
- Gazeti la Youm7 limeeleza kuwa kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, Ligi Kuu ya Misri itaingia msimu mpya bila kocha yeyote kutoka Ulaya, jambo lililotafsiriwa kuwa ishara ya kuongezeka kwa imani ya klabu za nchi hiyo kwa uwezo wa makocha wa Bara la Afrika.
CAIRO, MISRI: KOCHA Rulani Mokwena ameanza kujizolea sifa nchini Misri baada ya kutajwa kuwa miongoni mwa makocha wanaoongoza mapinduzi ya soka la nchi humo kuelekea msimu wa 2026/27, huku falsafa ya makocha wa Afrika ikianza kutawala ligi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi.
Gazeti la Youm7 limeeleza kuwa kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, Ligi Kuu ya Misri itaingia msimu mpya bila kocha yeyote kutoka Ulaya, jambo lililotafsiriwa kuwa ishara ya kuongezeka kwa imani ya klabu za nchi hiyo kwa uwezo wa makocha wa Bara la Afrika.
Miongoni mwa makocha wanaopewa jukumu la kuongoza mabadiliko hayo ni Hussein Ammouta aliyechukua mikoba ya Jess Thorup katika Al Ahly, Mohamed Amine Benhachem wa Modern Sport Club na Rulani Mokwena, aliyeteuliwa kuinoa Pyramids FC baada ya kuondoka kwa Mkroatia Krunoslav Jurcic.
Kwa mujibu wa chapisho hilo, hatua hiyo ni ushahidi wa kuongezeka kwa imani ya klabu za Misri katika mbinu na falsafa za makocha wa Afrika, jambo linalotarajiwa kuleta ushindani mpya ndani ya ligi hiyo.
Mokwena, ambaye alijijengea jina akiwa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, ametajwa kuwa mmoja wa makocha bora barani Afrika kutokana na mtindo wake wa soka unaosisitiza umiliki wa mpira, mashambulizi ya kasi na presha dhidi ya wapinzani.
Gazeti hilo linasema Pyramids imeamua kumkabidhi jukumu hilo kwa imani kwamba ataijenga timu yenye uwezo wa kupigania ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri pamoja na kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
"Pyramids FC inamtegemea Rulani Mokwena, mmoja wa makocha bora zaidi barani Afrika katika miaka ya hivi karibuni. Anajulikana kwa falsafa yake ya kushambulia, kumiliki mpira na kufanya presha ya juu, mtindo ambao klabu inalenga kuutumia kupigania ubingwa wa ligi na kufanya vizuri kimataifa," liliandika Youm7.
Mbali na kusifiwa kwa mbinu zake, ujio wa Mokwena umeonekana kuwa sehemu ya mabadiliko makubwa yanayoendelea katika soka la Misri, huku makocha wa Afrika wakipewa nafasi kubwa zaidi kuliko ilivyowahi kutokea katika siku za karibuni.
Wakati huo huo, Pyramids inaendelea na maandalizi ya msimu mpya nchini Uturuki, ambako kikosi hicho kimeweka kambi ya mazoezi. Timu hiyo inatarajiwa kucheza mchezo wake wa mwisho wa kirafiki Jumamosi, Agosti 8, kabla ya kurejea Cairo siku inayofuata kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea msimu mpya.